Songea. Mahakama Kuu, imeamuru watu wawili iliyowatia hatiani kwa mauaji, akiwemo aliyemchinja mama yake na kutenganisha kichwa na kiwiliwili, kuwekwa katika taasisi ya watu wenye tatizo la afya ya akili (mental Institution) kama wakosaji wendawazimu.
Hukumu hizo za kesi mbili tofauti za jinai, zimetolewa leo Alhamisi Februari 27, 2025 na Jaji Emmanuel Kawishe wa Mahakama Kuu kanda ya Songea, baada ya Mahakama kuridhika kuwa wakati wakifanya mauaji hayo ya kikatili na hadi sasa ni wendawazimu.
Katika kesi ya kwanza namba 19251, ilielezwa na upande wa Jamhuri Julai 15, 2023, katika kijiji cha Lituhi B wilayani Nyasa katika Mkoa wa Ruvuma, Veronica Mapunda, alimuua mama yake mzazi, Sofia Banda kwa kumchinja kwa panga.
Alipofikishwa mahakamani Agosti 19, 2024 na kusomewa shitaka lake na kutakiwa ama kukanusha au kukiri kufanya mauaji hayo, ilibainika alikuwa hawezi kufuatilia utaratibu huo kutokana na hali yake ya kiakili aliyokuwa nayo.
Kutokana na mazingira hayo, upande wa utetezi ukaiarifu mahakama kuwa katika kesi hiyo, wataegemea utetezi kuwa mteja wao ni mwendawazimu na kuiomba mahakama itoe amri apelekwe taasisi ya Isanga ili kuchunguzwa akili wakati anatenda kosa hilo.
Kwa kuwa ombi hilo halikupingwa, mahakama ilitoa amri hiyo apelekwe Isanga kwa ajili ya uchunguzi na baada ya taasisi hiyo kukamilisha uchunguzi wake, Hospitali ya Taifa ya Watu wenye matatizo ya afya ya akili ya Mirembe, iliwasilisha kortini ripoti yake.
Baada ya ripoti hiyo kupokelewa mahakamani, mshtakiwa alirudishwa tena mahakamani kusomewa shitaka lake, lakini upande wa mashtaka ukawasilisha ombi la kubadili hati ya mashitaka kutoka mauaji ya kukusudia kuwa ya kutokukusudia.
Hata hivyo, baada ya kusomewa shitaka hilo jipya katika lugha ya Kiswahili anayoielewa, mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo na aliposomewa maelezo ya kosa na kutakiwa kujibu kama ni sahihi, alijibu kuwa hafahamu chochote kuhusiana na mauaji hayo.
Katika kutimiza majukumu yake, upande wa mashitaka, ukiongozwa na mawakili wa Serikali, Frank Sarwat, Agness Simba na Suzan Sanga kuthibitisha kosa hilo, ambapo shahidi muhimu katika kesi hiyo alikuwa wa tatu, Dafrosa Ndimbo.
Shahidi huyo alieleza marehemu ni jirani yake na kueleza siku ya tukio, akiwa bafuni anaoga, mtoto wa marehemu aitwaye Junio Haule alifika nyumbani na kumjulisha mtoto wa shahidi huyo kuwa mshtakiwa alikuwa anamkatakata mama yake kwa panga.
Haraka alienda eneo la tukio na kuona mwili wa marehemu ukiwa sakafuni ukitokwa na damu nyingi na kichwa kilikuwa kimetenganishwa na kiwiliwili na ndipo alipopiga kelele za kuomba msaada kutoka kwa majirani, huku mshtakiwa akiranda randa eneo hilo.
Licha ya umati mkubwa wa watu, mshtakiwa hakujali chochote na alikuwa akitoka jikoni na kuja eneo la tukio na kurudi jikoni kisha akaenda bafuni kuoga na ndipo viongozi wa kijiji waliwasiliana na polisi wakiongozana na daktari aliyechunguza mwili wa marehemu.
Shahidi huyo aliiambia Mahakama kuwa mshtakiwa alikuwa na matatizo ya akili na kwamba kuna wakati aliwahi kumkata mtoto wake Junio sehemu za siri kwa kutumia mkasi, ambapo mwili wa marehemu ulichunguzwa na mshtakiwa kukamatwa.
Mashahidi wengine alikuwa ni polisi na daktari aliyechunguza mwili huo na baada ya Jamhuri kufunga ushahidi wake, wakili Simba aliyekuwa akimtetea mshtakiwa, aliiomba Mahakama izingatie ombi lao la kuegemea katika ushahidi mteja wao ni kichaa.
Wakili huyo alisema ni wazi kabla na wakati anatenda kosa hilo alikuwa ni mgonjwa wa akili na alipokamatwa, alipelekwa hospitali ya rufaa ya Ruvuma na ilibainika anasumbuliwa na ugonjwa wa akili uitwao Schizophrenia.
Wakili huyo alisema hata ripoti kutoka Hospitali ya Mirembe ya Novemba 20, 2024 inathibitisha kuwa anasumbuliwa na maradhi hayo na kuiomba Mahakama kupokea ripoti za hospitali zote mbili.
Jaji Kawishe katika hukumu yake, alisema hakuna ubishi Sofia Simba ni marehemu na kifo chake hakikuwa cha asili na kilisababishwa na kuvuja damu nyingi, kulikosababishwa na majeraha na kukatwa kichwa na kutenganishwa na kiwiliwili.
Kulingana na Jaji, ripoti zote mbili za uchunguzi zinathibitisha kuwa mshtakiwa ana matatizo ya akili na kurejea kile alichokuwa akikifanya baada ya kufanya mauaji hayo na hata alipohojiwa polisi, alikuwa haelewi nini kilikuwa kinaendelea.
Jaji alisema kulingana na ushahidi uliotolewa, mwenendo ulioonyeshwa na mshtakiwa kabla ya tukio hilo ya kuwa huwa anakwenda katika nyumba za watu usiku bila sababu yoyote, na ripoti ya daktari vinathibitisha tatizo la afya ya akili alilo nalo.
Kutokana na mazingira hayo, Jaji alisema kwa kuwa mshtakiwa ameshtakiwa kwa kuua bila kukusudia, kosa ambalo adhabu yake ni kifungo cha maisha, mahakama inaamuru mshtakiwa awekwe katika taasisi ya watu wenye tatizo la akili kama mkosaji kichaa.
Katika kesi nyingine ya jinai namba 16696 ya 2024, ilielezwa Mei 19, 2023, mshtakiwa Seleman Kalwanya ambaye ni mkazi wa kijiji cha Mtonya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, alimuua Elias Robert bila uhalali wowote.
Kama ilivyokuwa katika kesi ya Veronica, Kalwanya naye aliposomewa shitaka lake ilibainika kuwa hawezi kufuatilia nini kinaendelea kutokana na tatizo la kiakili, hivyo naye mahakama ikaamuru apelekwe Isanga na baadaye Mirembe kwa uchunguzi.
Baada ya ripoti uchunguzi kupokelewa na mshtakiwa kusomewa tena shitaka lake na kutakiwa kukubali au kukanusha alijibu tu “Nakubali kusimama,” hali iliyoonyesha anajibu vitu ambavyo havihusiani na kile anachoulizwa.
Upande wa mashitaka ukasoma maelezo ya kosa lakini mshtakiwa hakuweza kufuatilia, ndipo wakili Lazaro Simba anayemtetea akasema wao wataegemea utetezi kuwa mteja wake kabla na wakati anafanya mauaji alikuwa na matatizo ya afya ya akili.
Upande wa mashitaka uliita shahidi mmoja tu, Inspekta Msaidizi wa Polisi, Yesaya Mwakalebela ambaye ndiye alikuwa mpelelezi aliyeeleza kuwa Mei 20,2023 akiwa ofisini kwake, alipokea taarifa ya kuuawa kwa mtoto huko Namtumbo.
Haraka alikwenda eneo la tukio na huko alikutana na Hadija Selemani ambaye ni bibi wa mtoto aliyeuawa ambaye alisimulia tukio zima na kueleza kuwa jioni ya Mei 19, 2023, alikuwa jikoni na mjukuu wake aitwaye Elias Charles Robert ambaye sasa ni marehemu.
Alieleza ghafla, mshtakiwa alimchukua mjukuu wake na kumpigiza sakafuni ambapo shahidi huyo alipiga kelele za kuomba msaada lakini majirani walichelewa kufika eneo la tukio, ambapo mtoto alikuwa amejeruhiwa vibaya kutokana na tukio hilo.
Walimpeleka Zahanati ya Mtonya ambapo walipewa rufaa kwenda Hospitali ya Namtumbo ambako alifariki akipatiwa matibabu na shahidi huyo akaeleza kuwa wakiwa eneo la tukio walifanikiwa kumkamata mshtakiwa wa mauaji hayo.
Alipomuhoji bibi wa mtoto pamoja na watu wengine katika eneo la tukio, walimweleza kuwa mshtakiwa ni mgonjwa wa akili na anategemea dawa lakini kutokana na hali mbaya ya kifedha, aliacha kunywa dawa na ugonjwa ukarejea.
Kama ilivyokuwa katika kesi ya Veronica, upande wa utetezi uliegemea utetezi wa kuwa mshtakiwa ni mgonjwa wa akili na Jaji akasema ushahidi uliotolewa pamoja na ripoti za kitabibu, zinathibitisha kuwa ana matatizo ya afya ya akili.
Kutokana na mazingira hayo, Jaji alisema kwa kuwa mshtakiwa ameshtakiwa kwa kuua bila kukusudia, kosa ambalo adhabu yake ni kifungo cha maisha, Mahakama inaamuru awekwe katika taasisi ya watu wenye tatizo la akili kama mkosaji kichaa.