Washington. Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine anatarajiwa kuanza ziara yake nchini Marekani kesho Ijumaa Februari 28, 2025 huku Rais Donald Trump akianika sababu za ziara ya kiongozi huyo.
Taarifa ya Zelensky kufanya ziara Marekani imetolewa na Rais Trump wakati wa mkutano wa kwanza wa baraza la mawaziri katika muhula wake wa pili uliohudhuriwa na mawaziri, wakiwemo Waziri wa Biashara wa Marekani, Howard Lutnick na Waziri wa Mambo ya Nje, Marco Rubio.
Mkutano huo umefanyika Ikulu usiku wa kuamkia leo Alhamisi Februari 27, 2025, ambapo Trump amezungumzia lengo la ziara ya Rais Zelensky katika kusaka amani nchini Ukraine.
Akizungumzia mzozo wa Russia dhidi ya Ukraine, Rais Trump amesema Russia imeendelea na operesheni yake ya kijeshi inayoambatana na uvamizi wa ardhi ya Ukraine tangu Februari 2022.
Pia, Trump alithibitisha kuwa Rais Zelenskyy atafanya ziara yake nchini Marekani kesho Ijumaa, ili kusaini makubaliano yenye thamani ya Dola za Marekani zaidi ya Bilioni 350 (zaidi ya Sh908 trilioni) ambazo Marekani itapata kama fidia kupitia madini adimu kutoka Ukraine.
“Tutashirikiana sana na Ukraine kuhusu madini adimu. Tunayahitaji sana. Wana madini bora adimu,” Trump alisema, akiongeza makubaliano hayo yataipatia Marekani utajiri mkubwa.
Hata hivyo, Trump alikanusha makubaliano hayo yatailazimisha Marekani kutoa msaada wa kiusalama kwa Ukraine inapojaribu kujikinga dhidi ya mashambulizi ya Russia.
“Kweli, sitatoa dhamana za kiusalama zaidi ya kiasi fulani. Tutawaachia Ulaya wafanye hivyo,” amesema Trump.
Amesema uwepo wa raia wa Marekani katika ardhi ya Ukraine wanaoendesha shughuli ya uchimbaji madini, unaweza kuwa kizuizi kwa mashambulizi yajayo ya vikosi vya Russia.
“Ni makubaliano mazuri pia kwa Ukraine kwa sababu watatupata sisi kule, na tutafanya kazi huko. Tutakuwa kwenye ardhi yao na kwa njia hiyo kuna aina fulani ya usalama wa moja kwa moja kwa sababu hakuna mtu atakayetaka kuleta fujo wakati sisi tuko pale,” amesema.
Kipindi cha pili cha Trump hadi sasa kimeonyesha kuwa anajitambulisha kama mpatanishi wa amani, japokuwa katika mzozo wa Ukraine na Gaza, amejaribu kudai haki za Marekani juu ya ardhi na rasilimali.
Kuhusu Gaza, Trump amependekeza mara kadhaa kuwa Marekani inaweza kulichukua na kumiliki eneo hilo lenye vita, na kuwahamisha kabisa wakazi wake ambao ni raia wa Kipalestina.
Jumatano, kabla ya mkutano wa baraza la mawaziri akaunti yake ya mitandao ya kijamii ilitoa video iliyotengenezwa kwa akili bandia (AI) ikionyesha Gaza ikiwa imegeuzwa kuwa eneo la mapumziko, lenye mandhari ya kuvutia linaloitwa ‘Trump City’.
Licha ya ahadi zake za kurejesha amani duniani, Trump alikiri kwenye mkutano huo kuwa huenda asiweze kutimiza hilo nchini Ukraine.
“Siwezi kukuhakikishia hilo. Unajua, makubaliano ni makubaliano. Mambo mengi ya ajabu hufanyika kwenye makubaliano, sivyo? Lakini nafikiri tutakuwa na makubaliano,” alisema.
Mwandishi mmoja alimuuliza baadaye ikiwa Rais wa Russia, Vladimir Putin atalazimika kutoa unafuu kwa Ukraine kwenye mzozo huo kama sehemu ya mazungumzo ya amani.
“Ndio, atafanya hivyo. Atalazimika,” alijibu Trump.
Wakati Trump anajibu suala la Russia kulegeza kamba ya mashambulizi yake dhidi ya Ukraine kwenye mzozo huo, alirejea na kuanza kuilaumu Ukraine kwa kuichokoza Russia ili kutafuta kujiunga na Jumuiya ya Kujilinda ya Nato.
“Nato, sahau hilo. Nafikiri hiyo ndiyo sababu kubwa ya jambo hili lote kuanza,” Trump amesema.
Wakati huohuo, Trump alitangaza nia yake ya kuanzisha alichokiita ‘kadi ya dhahabu’ ambayo itakuwa ni mbadala wa “Green card”, ambavyo ni vitambulisho maalumu vinavyotolewa kwa wakazi wa kudumu wa Marekani.
Ameita mpango huo wa “kadi ya dhahabu”, kuwa raia kutoka mataifa mengine wenye nia ya kupatiwa uraia wa Marekani watatakiwa kulipa Serikali ya Marekani dola milioni 5 (Sh13 bilioni) ili kupatiwa uraia wa taifa hilo.
Jumatano, alitangaza kuwa “kadi ya dhahabu” haitawapa tu wahamiaji haki ya kuishi na kufanya kazi Marekani, bali pia itakuwa njia ya haraka kupata uraia.
“Ni kama ‘green card plus’, na ni njia ya kupata uraia,” Trump alisema.
Lakini wakosoaji wamehoji juu ya hofu yao kuwa mpango huo utatoa mwanya wa udanganyifu ama utafanya mfumo wa uhamiaji kuwa wa kibaguzi, kwa kuwapa huduma hizo tu matajiri waliokithiri.
Hata hivyo, Trump alitetea mpango huo, akidai utasaidia kuvutia wafanyakazi wenye vipaji kutoka nje. Alielezea mtazamo wake ambapo kampuni kubwa za teknolojia kama Apple zitawalipia wafanyakazi wao wa kigeni “kadi za dhahabu”, akilinganisha mpango huo na bonasi za usajili kwa wanamichezo.
“Apple au kampuni nyingine wataenda na labda watanunua tano, kisha watachukua watu watano,” amesema.
Trump pia alitabiri kuwa mapato yatokanayo na “kadi za dhahabu” hayataisaidia tu Marekani kulipa madeni yake, bali pia yatachochea ajira nchini.
“Nakwambia, watu wanaoweza kulipa dola milioni tano, watazalisha ajira. Watatumia pesa nyingi kwenye ajira. Na watalazimika kulipa kodi juu ya hilo pia.
“Na sijui, labda itauzwa sana. Nahisi kweli itauzwa sana. Ni dili kubwa.”
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.