Uwekezaji wa kifedha, njia zinazovutia vijana, ikiwemo kufadhili mawazo bunifu waliyonayo, utafiti ni miongoni mwa vitu vinavyotajwa kuwa vinavyoweza kuifanya Tanzania kufikia mauzo ya kahawa yenye thamani ya Dola za Marekani 1 bilioni ifikapo mwaka 2030.
Lengo hili la kukuza mauzo linaenda sambamba na kuongeza uzalishaji kufikia tani 300,000 katika kipindi hicho, huku uvutiaji wa vijana katika sekta hiyo ikitajwa kuwa moja ya njia inayoweza kufanya malengo haya kufikiwa.
Mauzo haya yanayolengwa yatakuwa ni ongezeko kutoka dola za Marekani 295.5 milioni ya thamani ya sasa ambayo inaiweka Tanzania katika nafasi ya nne katika uzalishaji wa kahawa ndani ya bara la Afrika.
Haya yanaelezwa na wadau mbalimbali, wakati ambao tayari nchi 25 za uzalishaji wa kahawa Afrika zimeweka azimio la kuhakikisha hadi kufikia mwaka 2035 asilimia 50 ya kahawa yote inayozalishwa ndani ya Bara hili iwe inaongezwa thamani kabla ya kusafirishwa masoko ya nje.
Azimio hilo linaenda sambamba na uongezaji wa uzalishaji wa kahawa hadi kufikia asilimia 20 ya soko lililopo duniani, ikiwa ni baada ya kiwango cha uchangiaji katika soko kwa kahawa ya Afrika kuonekana kushuka kutoka asilimia 25 miaka ya 1960 hadi kufikia asilimia 11.2 kwa sasa.
Hiyo ni kutokana na nchi hizi kutumia fedha nyingi katika kuingiza kahawa iliyoongezewa thamani baada ya kuuza kahawa ghafi kwa bei ndogo.
Hata hivyo, ili kufikia malengo yaliyowekwa na Tanzania, ni lazima kuongeza uzalishaji ili kuwezesha kupatikana kwa malighafi nyingi itakayoingia sokoni na kuviwezesha viwanda kupata malighafi ya kutosha.
Maeneo mengine ambayo yanaweza kufanyiwa kazi ili kufikia lengo hilo ni kuongeza ufadhili wa kifedha kwa wazalishaji ili kurahisisha uzalishaji kulingana na maeneo wanayofanyia kazi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kahawa ya Amir Hamza Ltd, Amir Hamza anasema licha ya kuwa na fursa ya kutoa ajira kwa vijana, kikwazo kikubwa ni rasilimali fedha.
“Bila pesa ni ngumu kuongeza thamani na utafiti. Pia utafiti unaofanyika Tanzania ni ule wa kilimo, hakuna wa mitambo au mashine na teknolojia ya kuzalisha kahawa iliyoongezwa thamani,” anasema Hamza.
Anasema kukosekana kwa fedha pia kunafanya kutokuwapo kwa mashine na mitambo iliyotengenezwa nchini, jambo linalofanya waongezaji thamani kuendelea kununua kutoka nje ya nchi ambazo ndiyo wanunuzi wa kahawa ghafi.
“Sasa mashine hii inapokuja nchini ukiitumia kuzalisha kahawa nzuri itauzwa kwa Sh4,000, Sh5,000 hadi Sh7,000, Mtanzania wa kawaida hawezi kumudu na badala yake ataendelea kunywa ya shilingi 100 barabarani ambayo ladha yake haiendani na ile ambayo vijana wanahitaji,” anasema Hamza.
Anasema ikiwa hili litaangaliwa vizuri, kahawa itakuwa inaongezwa thamani na kuwavuta watu wengi kuitumia, jambo ambalo litainua sekta ya kahawa nchini.
Jambo hilo liliungwa mkono na Mtaalamu wa biashara na kilimo, Dk Emmanuel Magesa ambaye anasema kuna umuhimu wa kuwapo kwa mifumo ya msaada wa kupata fedha kwa wakulima wadogo.
“Upatikanaji wa mikopo na ufadhili nafuu bado ni changamoto kubwa kwa wakulima wa kahawa barani Afrika. Bila msaada wa kifedha, kuongeza uzalishaji inakuwa vigumu,” anasema.
Mchambuzi wa soko la kahawa, Fatuma Juma anasema ili Tanzania na nchi za Afrika zinazozalisha kahawa zifikie lengo walilojiwekea, ni vyema kuzingatia ufanyaji wa biashara kati yao kwa ufanisi.
Mbali na kile kinachofanywa na Serikali moja kwa moja, sekta ya benki ni moja ya eneo ambalo linaangaliwa zaidi na wazalishaji ili kufikia malengo haya, hasa katika uwezeshaji mikopo.
Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Ushirika Nchini (COOP BANK), Godfrey Ng’urah anasema moja ya malengo yao ni kuhakikisha kilimo hiki kinakuwa cha kisasa chenye tija na bora.
Ili kuwezesha kuongeza uzalishaji, anasema ndani ya miaka mitano wametoa Sh15 bilioni kwa wanachama 74,000 ambao wanalima kahawa, huku vyama 2,000 vikinufaika na mikopo hiyo ili kuboresha kilimo chao.
Kupitia hilo waliweza kuchangia kuboresha upatikanaji wa pembejeo kwa wakati wakulima, jambo ambalo liliwawezesha wakulima kufikia masoko kwa urahisi, ambalo pia limeleta msisimko katika bei na kuifanya kupanda msimu hadi msimu.
“Hii ni kwa sababu wanawezeshwa kwa mitaji ya pembejeo, viuatilifu, kuweza kufanya maandalizi ya shamba na kuvuna kwa uhakika, huku wakihakikishiwa masoko kwa mfumo wa stakabadhi ghalani,” anasema.
Anasema kama benki inatambua ili kufanikisha hayo, fedha zinahitajika kwa kiasi kikubwa, hivyo kama benki ya ushirika imekuwa ikiwahakikishia wakulima uhakika wa mitaji wanapohitaji ili kuboresha kile wanachokifanya.
Ili kuvutia vijana wengi kuingia katika kilimo kama malengo ya mkutano yanavyosema, Ng’urah anasema benki hiyo imetengeneza mifumo ambayo itawawezesha kushiriki katika namna ambayo wanataka, si lazima walime.
Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa wakulima wengi wa mazao ya kimkakati, ikiwemo kahawa, pamba, korosho, katani ni wale wenye umri wa miaka 50 hadi 58, hali inayoleta changamoto juu ya uendelevu wake, hasa kizazi hicho kitakapofikia tamati. “Kwa sababu vijana hawana mitaji, dhamana na rekodi ya biashara sisi tumekuwa tukiweka nguvu katika kufadhili miradi ya kibunifu kwa sababu tunajua hatutawaleta vijana katika kilimo kama hatutaweza kufadhili bunifu hizi,” anasema Ng’urah.
Anasema kwa sababu ubunifu wao ndiyo sababu ya wao kupata mitaji, basi wanahakikisha aina ya bidhaa wanayoleta, andiko wanaloleta wanasaidiwa kulifanyia maboresho ili liweze kuwasaidia kupata mitaji na kuanzisha kile wanachotaka.
“Watu hawa hawawezi kuwa na mashamba, dhamana, lakini wanaweza kuwa na mawazo yanayoweza kufadhiliwa na benki, kutekelezeka na sisi tunaamini katika hilo, kwani kama benki lazima tuwape kipaumbele vijana wabunifu,” anasema.
Anasema jambo hilo linaenda sambamba na kufadhili uongezaji wa thamani ya mazao katika mnyororo wa thamani.
“Huenda vijana wasingependa kulima moja kwa moja mashambani, lakini wanaweza kuongeza thamani ya mazao yanayotoka mashambani. Tuwafadhili kwa teknolojia, kwa viwanda vidogovidogo, mashine au vitu mbalimbali wanavyoweza kutumia kuongeza thamani ya kahawa, anaweza asilime, lakini anaweza kuipika, kuifungasha na kufungua maduka na kumsaidia mkulima kupata soko,” anasema.
Hiyo ni kwa sababu vijana sasa wanaenda sambamba na mabadiliko ya sayansi na teknolojia na mara zote wanataka kuona kitu wanachokifanya kinaonekana katika mitandao mbalimbali, ikiwemo ya kijamii kama Instagram, Facebook na Youtube na kuwa na uwezo wa kuifuatilia popote anapokuwa.
“Lazima tuwasaidie kwa namna ambayo teknolojia itawawezesha kwenye kile anachokifanya, akija katika mawazo hayo tunawasaidia kwa kuwapa mitaji ya kifedha,” anasema.
Hata hivyo, anasema ili kufikia lengo lililowekwa, ni vyema kama nchi kuangalia nafasi yake katika dunia na kutengeneza sera za makusudi ambazo zinaweza kuisaidia sekta ya kahawa na kuhakikisha kuwa inayouzwa ni ile iliyoongezewa thamani.
“Tunaweza kuja na sera za makusudi kuwa kahawa yetu haiendi nje ya nchi kama haijaongezwa thamani na sisi tutakuwa wa kwanza kusaidiana na serikali katika hili,” anasema.
Soko la nje linaangaliwa zaidi kwa sababu takwimu za Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) zinaeleza kuwa zaidi ya asilimia 93 ya kahawa inayozalishwa nchini inategemea soko la nje, huku asilimia saba pekee ikitumika ndani ya nchi.
Katika mkutano wa wazalishaji wa kahawa uliofanyika Februari 21 na 22 mwaka huu, mataifa 25 yanayozalisha kahawa barani Afrika yalikubaliana pamoja na mambo mengine, kuhamasisha vijana kushiriki katika kilimo cha zao hilo.
Akisoma makubaliano hayo, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema lengo la kwanza ni kuhakikisha angalau asilimia 50 ya uzalishaji wote wa kahawa barani Afrika unaongezewa thamani ndani ya Bara.
“Lengo hili ni mpaka kufikia mwaka 2035, hii itahakikisha kuwa kahawa hii itauzwa ikiwa imeongezewa thamani,”
Eneo lingine walilokubaliana ni kuunga mkono utafiti katika kuongeza thamani ya kahawa ili kuwezesha ubunifu na maendeleo ya bidhaa mpya, kuzalisha teknolojia mpya za mbinu bora za kilimo.
“Hii itasaidia kuvumbuliwa aina mpya za kahawa zenye mavuno mengi, ubora wa hali ya juu na ustahimilivu dhidi ya hali mbaya za hewa, wadudu na magonjwa.”
Kadhalika nchi hizo zilikubaliana kuunga mkono uwekezaji katika kuongeza thamani ya kahawa na bidhaa zake pamoja na kuhamasisha matumizi ya kahawa ndani ya nchi eneo lingine ambalo lililoguswa, likifuatiwa na kubuni na kutumia teknolojia mpya katika mnyororo wa thamani wa kahawa.
Vilevile viongozi walikubaliana kuwa Serikali za Afrika ziunge mkono mipango ya kuongeza matumizi ya kahawa ndani ya nchi na kuwezesha wananchi wao kufanya kazi katika ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi ili kuwekeza katika kuongeza thamani ya kahawa na afya na ustawi wa watu wa Afrika.