Dar es Salaam. Wataalamu wa lishe nchini Tanzania wamesema licha ya umuhimu wao katika jamii, bado hawatambuliki rasmi kama sehemu ya kada ya afya, jambo linalosababisha wapate malipo duni katika utendaji wao.
Pia wamesema hakuna bodi maalumu inayosimamia utendaji wa wanataaluma wa lishe nchini, hali inayosababisha watu wasio na taaluma hiyo kufanya kazi kama wataalamu wa lishe.
Mwenyekiti wa Chama cha Wataalamu wa Lishe Tanzania (TNDA), Maria Samlongo ametoa kauli hiyo leo Februari 27, 2025, wakati wa mkutano mkuu wa tatu wa chama hicho, uliofanyika Dar es Salaam.
“Kutotambulika kwa kada ya lishe kama sehemu ya kada za afya kumesababisha wataalamu kuathirika katika miundo ya mishahara na baadhi ya masilahi wakati wa utekelezaji wa majukumu. Lishe ni sekta muhimu kwa Taifa, lakini hadi sasa taaluma hii haitambuliki rasmi katika kada za afya,” amesema.
Aidha, Maria amesema hakuna mwongozo wa utoaji wa huduma za lishe kwa Watanzania kulingana na afya zao, hali inayochangia mkanganyiko wa ulaji ndani ya jamii.
Akizungumza katika mkutano huo, Ofisa Lishe Mwandamizi wa Wizara ya Afya, Idara ya Kinga, sehemu ya huduma za lishe, Grace Moshi, amesema wizara hiyo inatamani TNDA iwe na baraza lake la kitaaluma, hivyo wanachama wanapaswa kuongezeka ili kufanikisha jambo hilo.
“Takwa la kwanza la kuwa na baraza ni kuwa na chama chenye wanachama wa kutosha. Uwepo wa baraza utasaidia katika masuala ya masilahi na pia kudhibiti watu wanaojitokeza kwenye vyombo vya habari kama wataalamu wa lishe bila kuwa na sifa stahiki,” amesema.
Ameeleza kuwa mchakato wa kuanzisha baraza hilo unahusisha Wizara ya Afya kupeleka mapendekezo ya kutungwa sheria kwa ajili ya kuunda baraza hilo, huku idadi ya wanachama ikiwa kigezo muhimu katika ufanikishaji wake.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Lishe katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Luifrid Nnally, amesema ni muhimu kwa wataalamu wa lishe kuwa na bodi.
“Ni lazima kuwahamasisha wenzetu wajiunge na chama ili tuwe na bodi itakayowalazimu wanachama kuwa na leseni. Mtu yeyote anayejiita mtaalamu wa lishe bila sifa stahiki atafungiwa, hatua itakayosaidia kulinda taaluma yetu,” amesema.
Akizungumzia hali ya lishe nchini, Nnally amesema miaka ya 1960 Tanzania ilikuwa inakabiliwa na utapiamlo na upungufu wa vitamini mbalimbali, lakini hali imekuwa ikibadilika kadri muda unavyosonga.
“Sasa tumeanza kupata tatizo la lishe iliyozidi, linaloonekana kwa watu kupata kiribatumbo na unene kupitiliza. Kufikia mwaka 2050, tatizo la lishe duni litapungua, lakini tutakabiliwa na changamoto ya lishe iliyozidi, jambo ambalo litaongeza gharama za matibabu na kuathiri mifuko ya bima ya afya,” amesema.