Watuhumiwa wa mauaji  Himo, wana kesi ya kujibu

Moshi. Mkemia Mkuu wa Serikali, Leonidas Michael, ambaye alifanya uchunguzi wa vina aba (DNA) wa mabaki ya mwili wa Josephine Mngara (30),  anayedaiwa kuuawa kwa kuteketezwa kwa moto, amesema uchunguzi umebaini kwamba kuna uhusiano wa vinasaba kati ya mabaki hayo, na sampuli ya damu kutoka kwa mama aliyedai marehemu alikuwa ni mtoto wake.

Mkemia mkuu amewasilisha ripoti hiyo katika kesi iliyoanza  kusikilizwa Februari 24, 2025 mbele ya Jaji Adrian Kilimi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi huku upande wa mashitaka ukiongozwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Kambarage Samson pamoja na Frank Ong’eng’a na Grace Kabu.

Mbali na mawakili hao, lakini utetezi katika kesi ya mauaji namba 3382/2024, inayowakabili washtakiwa wawili, Erasto Mollel na Samwel Mchaki, unawakilishwa na mawakili wa kujitegemea, Alfredy Sindato Silayo na Lilian Mushi.

Wawili hao kwa pamoja wanashtakiwa kwa kosa la kumuua kwa makusudi, mwanamke huyo eneo la Mtemboni, Mji mdogo wa Himo, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, Februari 19, mwaka 2023 kwa kumteketeza kwa moto.

Kwa mujibu wa upande wa mashitaka marehemu alikuwa akiishi na Mollel ambaye alikuwa ni mpenzi wake na aliuawa kikatili usiku wa kuamkia Februari 19, 2023 na mwili wake kuteketezwa kwa moto kwenye pagale kwa kile kilichodaiwa na Polisi kuwa ni wivu wa mapenzi.

Majibu ya Mkemia Mkuu wa Serikali

Akitoa ushahidi kwa  mkutano wa video mtandaoni (video conference), Mkemia huyo  ameeleza kuwa, Machi 15, 2023, alimpokea askari kutoka Ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Kilimanjaro, J3632 PC John, ambaye alimkabidhi vielelezo vinane vilivyokuwa kwenye kifurushi cha bahasha.

Ameeleza kuwa, kifurushi hicho kilikuwa na barua kutoka kwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Moshi, akiomba uchunguzi wa sampuli za damu (DNA) zilizokuwa ndani ya bahasha hizo.

Ameeleza kuwa, kifurushi A, kilikuwa ni sampuli ya damu ya mama wa marehemu Josephine, B ni mfupa wa nyonga wa marehemu, C mfupa wa mkono wa marehemu, D jino la gego la marehemu, E mpanguso wa damu sakafuni kwenye nyumba aliyokuwa akiishi marehemu, E1 mpanguso wa damu ukutani, E2 mpanguso wa damu sakafuni na E3 damu kutoka kwenye magome ya miti.

Amedai kuwa, baada ya kupokea na kukabidhiwa vifurushi hivyo, alivipa namba ya usajili wa maabara namba HQ023-00598.

“Nilianza uchunguzi wa awali ili kubaini kama kielelezo A, E, E1, E2 na E3 ni damu ya binadamu nilifanya uchunguzi wa vinasaba (DNA) kielelezo A-E3 tuliingiza kwenye mtambo, nili-search DNA kwa kila kielelezo, nikachukua majibu niliyopata na kulinganisha na hesabu za kitakwimu,”ameeleza Mkemia huyo

Amefafanua kuwa, “nilibaini kielelezo A kina mahusiano na vielelezo E, E1, E2 na E3 na pia nilibaini kuwa, kielelezo A kina mahusiano na kielelezo B, C na D.”

Baada ya shahidi huyo kutoa ushahidi wake, aliiomba Mahakama hiyo ipokee maelezo yake kama sehemu ya kielelezo katika ushahidi wa kesi hiyo.

Hata hivyo baada ya Jaji Kilimi kupokea kielezo hicho cha shahidi wa mwisho kwa upande wa Jamhuri, aliuliza upande wa utetezi kama wana pingamizi lolote kuhusiana na ushahidi huo ambapo walisema hawana.

 Alichokisema Jaji Kilimi

Baada ya upande wa Jamhuri kufunga ushahidi wake uliotolewa na mashahidi 12 mahakamani hapo, mahakama iliona washtakiwa hao  wana kesi ya kujibu na hivyo ikiwataka watoe utetezi wao na ambapo walikubali kuutoa kwa njia ya kiapo.

“Nimepitia maelezo yote ya mashahidi 12 na vielelezo vilivyowasilishwa hapa mahakamani, nimeona washtakiwa wana kesi ya kujibu,”amesema.

Related Posts