Mshery kama Aziz KI, aoa asamehe fungate

KIPA wa Yanga, Aboutwalib Mshery, jana amevuta jiko katika tukio ambalo halikuwa na mbwembwe nyingi, lakini leo asubuhi akashtua akiwa kwenye msafara wa timu hiyo ikiifuata Pamba Jiji.

Mshery anakuwa staa wa pili wa Yanga kufunga ndoa ndani ya Februari kisha kusamehe fungate akitanguliwa na kiungo Stephanie Aziz KI aliyemuoa Hamisa Mobetto.

Kama ambavyo ilikuwa kwa Azizi KI, ambaye baada ya kufunga ndoa tu siku hiyohiyo hakutaka kula fungate na mkewe badala yake akavua kanzu na kurudi kambini kuendelea na maandalizi ya mechi za Ligi na kesho yake akacheza mechi ya Ligi Kuu kama hakuwa na shughuli yoyote.

Mshery naye akafanya hivyo hivyo, hakutaka mambo yawe mengi akarudi kazini na leo ameondoka kwenda Mwanza kuwafuata Pamba Jiji watakaoumana nao keshokutwa, Ijuma.

Kipa huyo namba mbili wa Yanga, atakuwa sehemu ya kikosi cha timu yake, kitakachocheza mechi ya Pamba Jiji, mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Mastaa hao wawili hawakutaka hata kwenda fungate, wakirudi kazini haraka kuendelea kuipigania timu yao, inayotafuta taji la nne mfululizo la ligi.

Related Posts