BoT yanunua zaidi ya tani mbili za dhahabu

Mtwara. Wakati Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ikipanga kununua tani sita za dhahabu kila mwaka, tayari imenunua zaidi ya tani mbili tangu ianze mpango huo mwaka 2024.

Mpango wa kununua dhahabu ulianza Julai mwaka jana, lakini utekelezaji wake ukaanza Oktoba. Lengo ni kuwa na dhahabu kama sehemu ya akiba yake ya fedha za kigeni.

Hayo yamebainishwa jana, Februari 25, 2025 na mchambuzi wa masuala ya fedha wa Benki Kuu, Dunga Nginilla, katika semina kwa waandishi wa habari ambapo amesema BoT imepanga kununua tani sita za dhahabu kila mwaka, na itatumia Dola milioni 350 za Marekani (zaidi ya Sh905 bilioni).

Amesema kwa kipindi cha miezi mitano pekee, tayari wamefanikiwa kununua zaidi ya tani mbili, ambayo ni mafanikio na inaonekana kwa mwendo ulivyo watafanikiwa kufikia malengo.

Sheria ya Madini ya mwaka 2019 kifungu cha 59 sura ya 123, imeweka wazi kwamba anayetaka kuuza dhahabu nje lazima asilimia 20 iuziwe Benki Kuu.

Amesema lengo la kuanzisha mpango huo ni kuwa na dhahabu kama sehemu ya akiba ya fedha za kigeni ili kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza endapo kutatokea msukosuko wa fedha za kigeni.

“Hata hivyo, wakati tunaanza mpango huu, tulipata changamoto kubwa kwani haukuwa umeeleweka vyema, na masharti na mchakato wake ulikuwa mrefu, ambapo mtu alitumia zaidi ya siku mbili ili kukamilisha na kupata malipo yake, lakini sasa, ndani ya saa 24, mchakato unakamilika na mtu anapata fedha zake,” amesema.

Licha ya sheria kuweka wazi kwamba kila anayetaka kuuza dhahabu nje ya nchi, lazima aiuzie BoT asilimia 20, pia muuzaji anapata faida kadhaa ikilinganishwa na kuuza kwa kampuni binafsi.

“Kwa sasa, wengi wanavutiwa kutuuzia sisi kwa sababu mambo yamerahisishwa, halafu mtu anapunguza asilimia tatu, kwa hiyo anaona bora auze bila kupata kigugumizi,” amesema.

Amefafanua baadhi ya faida hizo ni pamoja na BoT kulipa bei ya soko la kimataifa, na imepunguza mrabaha kutoka asilimia sita anazolipa iwapo akiuzia kampuni binafsi hadi asilimia nne iwapo akiuzia BoT.

“Pia, sheria hii ya madini imepunguza bei ya ukaguzi, ambapo badala ya asilimia moja, hapa muuzaji halipi kitu chochote katika ukaguzi. Kwa hiyo, haya yote ni manufaa ambayo Serikali iliweka ili kuleta unafuu,” amesema.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo wa fedha, Serikali imeingia mkataba na viwanda vitatu katika kununua dhahabu ili kupata kiwango na ubora unaohitajika, ambavyo vipo Geita, Mwanza, na Dodoma.

Hata hivyo, amesema Tanzania ipo kwenye mpango wa kujenga kiwanda ambacho kitatambulika kuuza dhahabu ambazo zinatambulika kimataifa, ambapo kwa sasa kwa Afrika kuna kiwanda kimoja tu kilichopo Afrika Kusini.

Umuhimu wa kuwa na fedha nyingi za kigeni unamvutia mwekezaji kuwekeza akiwa na imani ya uhimilivu wa mtaji wake.

Akizungumzia sera ya fedha inayotumia riba ya Benki Kuu, Mchumi wa Kurugenzi ya Tafiti na Sera za Uchumi BoT, Dominic Mwita, amesema benki hiyo inaweza kutumia riba kubadilisha fedha zilizomo kwenye mzunguko.

“Lengo la kuweka riba ya BoT ni kudhibiti mfumuko wa bei na kuchochea shughuli za kiuchumi. Iwapo BoT itabaini kuna mfumuko wa bei utaongezeka, itaongeza riba; na ikibaini kuna kuzorota kwa shughuli za kiuchumi, itapunguza riba,” amesema.

Januari 2024, BoT ilianza kutekeleza sera hiyo, ambapo imeweka riba ya asilimia sita kutoka asilimia 5.5 iliyokuwapo awali.

Amesema faida za kuwa na mfumo mpya ni kuongeza uwazi.

Awali, Mkurugenzi wa BoT Tawi la Mtwara, Nassor Omar, amesema benki hiyo imeamua kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari ili kuongeza uelewa na kuwasaidia wananchi kupata elimu ya fedha.

“Waandishi wa habari ni kada muhimu; wanafikia watu wengi, kwa hiyo mkipata uelewa huu mtatumia kalamu zenu kuelimisha umma kuhusu masuala haya. Tutaendelea kushirikiana katika kuwafikia watu wengi,” amesema.

Related Posts