Amiri wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, aliyekuwa ziarani mjini Tehran, Iran wiki iliyopita, alisisitiza mpango wa pamoja kati ya nchi yake na Iran wa kuchimba barabara ya chini ya bahari katika Ghuba ya Uajemi, ambayo itaunganisha Iran na Qatar.
Mradi huu wa kipekee pia unatarajiwa kuongeza muunganisho kati ya Asia ya Magharibi, Bahari ya Kaspi, na Bahari ya Mediterania.
Wazo la kujenga njia hii ya chini ya bahari, inayotarajiwa kuwa ndefu zaidi duniani, lilijadiliwa kwa mara ya kwanza wakati wa ziara ya aliyekuwa Rais wa Iran, Ebrahim Raeisi, nchini Qatar mnamo Februari 2022.Wakati huo, ilielezwa kuwa mradi huo ungeanza tu baada ya kamati ya pamoja ya Qatar na Iran kukamilisha tafiti na mazungumzo kuhusu mpango huo.
Katika mkutano wake na Kiongozi Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, Amiri wa Qatar alisema kuwa kamati ya mradi huo itaanza kufanya kazi hivi karibuni, jambo linaloashiria jinsi Qatar ilivyo makini katika kufanikisha mpango huu mkubwa.