IMEPITA misimu minane ukienda wa tisa tangu beki wa Simba, Shomari Kapombe alivyoweka rekodi 2015/16 akiwa Azam FC ambayo hadi sasa bado haijavunjwa na mabeki wazawa wala wa kigeni katika Ligi Kuu Bara.
Mchezaji huyo ambaye ni panga pangua katika kikosi cha wababe hao wa Msimbazi, msimu huu anaendelea kufanya yake kikosini ambako ni kama amejimilikisha namba upande wa beki wa kulia.
Lakini, Kapombe aliweka rekodi ya kufunga mabao manane katika Ligi Kuu, akifunga moja Azam FC ikishinda mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union, dhidi ya Ndanda FC 0-1, dhidi ya Toto Africans mawili pale Azam iliposhinda mabao 5-0, dhidi ya Mgambo Shooting 2-0, dhidi ya Stand United 0-1 na dhidi ya Kagera moja Azam ikishinda mabao 2-0.
Kapombe aliwahi kukiri sababu ya mafanikio ya mabao hayo ni pamoja na kuwepo kwa wachezaji wazuri kipindi hicho na Azam ilimaliza nafasi ya pili ikiwa na pointi 64, baadhi yao walikuwa Ivo Mapunda, Gadiel Michael, Aggrey Morris, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Didier Kavumbagu, Himid Mao, Mudathir Yahya, John Bocco na Ramadhan Singano.

Wakati Kapombe anajiunga na Azam msimu wa 2015/16, alitokea klabu ya Cannes ya Ufaransa iliyokuwa inacheza Ligi Daraja la Nne, ilimchukua kwa makubaliano maalumu kutoka Simba 2013/14, hata hivyo hakukaa muda mrefu akarejea tena Tanzania.
Ni kweli Kapombe hajaivunja ama kuifikia rekodi hiyo, lakini bado anaendelea kufanya vizuri kama Mwanaspoti lilivyokukusanyia data zake baada ya msimu wa 2015/16 ambao alimaliza na mabao manane na Januari 2016 alinyakua tuzo ya mchezaji bora wa ligi (MVP), na kukabidhiwa Sh1 milioni kutoka kwa wadhamini wa kipindi hicho.
Kuanzia msimu wa 2017/18, baada ya kujiunga Simba (2017/18, bao moja, asisti tano), (2018/19 asisti mbili), (2019/20 asisti tano), (2020/21 asisti saba), (2021/22 bao moja, asisti nne), (2022/23 bao mbili, asisti nane), (2023/24 asisti nne) na (2024/25 mabao matatu, asisti tatu hadi sasa).
Beki Lenny Kisu, akiwa Biashara United alijaribu kuisogelea rekodi ya Kapombe na alimaliza na mabao matano yakibaki matatu kumfikia.

Pia waliibuka mabeki wengine waliwahi kufunga mabao mengi ila siyo kwa idadi ya mabao manane ya Kapombe, akiwamo Juma Abdul msimu wa 2009/10 akiwa Toto Africans alifunga mabao sita, 2011/12 Said Swedi akiwa Coastal Union alifunga sita, 2012/13 Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Mbuyu Twitte kila mmoja alifunga mabao manne na 2013/14 Tumba Swedi alimaliza na matano.
Msimu huu kuna mabeki waliofunga mabao mengi, endapo wakikaza buti huenda wakaifikia rekodi hiyo, akiwamo Ibrahim Bacca wa Yanga (mabao manne), mabeki wa Singida Black Stars Hernest Malonga (mabao matatu) na Anthony Tra Bi (mabao mawili), huku Kapombe mwenyewe na Che Malone wa Simba kila mmoja akiwa na mawili na kiraka wa Namungo Erasto Nyoni (mawili).

Nahodha wa zamani wa Yanga, Cannavaro aliyehamishia makazi yake Marekani amesema: “Mabeki kufunga mabao mengi inategemea na mifumo ya makocha, aina ya wachezaji wanaokuwepo na upepo wa mchezaji mwenyewe, hivyo ikitokea hawajafunga mabao mengi haimaanishi hawafanyi kazi yao vizuri.”
Kwa upande wa Nyoni ambaye anaitumikia Namungo, amesema inapotokea mabeki wanafunga mabao mengi, wanakuwa wamefanya zaidi ya majukumu yao ingawa inategemeana.
“Kuna wakati mchezaji mnyumbulifu anaweza akafanya vitu vingi uwanjani, ila wakati mwingine inakuwa ni mifumo ya makocha, jambo kubwa na la msingi nidhamu ya mchezaji kufanya mazoezi ya kumweka fiti na kujitunza.”

Beki wa zamani wa Yanga, William Mtendamema anampongeza Kapombe kwa kazi kubwa anayoifanya, kutokana na kuwajibika zaidi ya majukumu yake kuisaidia Simba.
“Haijalishi hajavunja rekodi yake ama kuifikia, hayo siyo majukumu yake, pia amekuwa na mwendelezo wa kiwango ndiyo maana kila kocha anayekuja Simba anamtumia kikosi cha kwanza, hilo siyo jambo dogo, binafsi sijawahi kufunga mabao mengi na yanafika matatu nikiwa na Mlandege ya Zanzibar pia nilibadilishwa namba kutoka 4, 5 nikawa nacheza sita, hivyo beki wa aina yake ni kitu kikubwa kwa timu ya Taifa,” amesema.