Yaliyofanywa na Serikali sekta ya ujenzi, uvuvi

Pangani. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema tangu Serikali ya awamu ya sita iingie madarakani Machi 19, 2021 imekamilisha ujenzi wa madaraja manane yaliyoanza kujengwa na awamu zilizopita.

Ulega ameyataja baadhi ya madaraja hayo kuwa ni Tanzanite la Dar es Salaam, Kitengule mkoani Kagera na Msingi la Singida ambayo kwa ujumla wake yamegharimu Sh381 bilioni.

Waziri Ulega ametaja takwimu hizo leo Jumatano Februari 26, 2025 katika mkutano wa hadhara wa Rais Samia uliofanyika wilayani Pangani mkoani Tanga.

Kabla ya mkutano, Rais Samia ameweka jiwe na msingi la ujenzi wa daraja la Pangani na barabara unganishi ya Bagamoyo- Pangani – Tanga utakaofadhiliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) ambayo imetoa Sh390.1 bilioni, huku Serikali ikitoa Sh58.47 bilioni.

Mbali na madaraja hayo, Ulega amesema wa Rais Samia alipoingia madarakani  alikuta barabara zinazoendelea kujengwa, kati ya hizo kilomita 1,366 zimekamilishwa kwa thamani ya Sh2.7 trilioni.

Baada ya kazi hiyo, amesema utekelezwaji wa miradi mipya ya madaraja makubwa unaendelea, likiwemo la Mto Pangani lenye urefu wa mita 525 sawa na viwanja vitano na robo vya mpira wa miguu.

“Pamoja na daraja hili, zitakuja kilomita 25 za barabara kama maungio ya daraja hili,” amesema Ulega.

Waziri Ulega amesema daraja hilo pia, litaambatana na uwekaji wa taa 440 zitakazowekwa katika barabara za Wilaya ya Pangani.

Amesema kilomita 2,031 za barabara zinaendelea kujengwa zikiwemo zinazotoka Bagamoyo-Mkange-Tungamaa-Pangani Tanga, ambayo ilipigiwa kelele na wabunge mbalimbali.

Ulega amesema jambo la kufurahisha ni kwamba makandarasi wa barabara hiyo hawaidai chochote Serikali, badala yake wao ndio wanadaiwa.

“Wizara ya Ujenzi ikiwa inamdai mkandarasi, inamwambia asicheke wala asi-relax (asipumzike) afanye kazi usiku na mchana hadi kieleweke Watanzania waendelee kupata matunda ya uhuru wa nchi yao,” amesema Ulega.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads),  Mohamed Besta amesema mradi wa ujenzi wa barabara ya Bagamoyo (Makurunge)  Mkange  – Pangani – Tanga  yenye urefu wa kilomita 256 unaojumuisha daraja la Pangani lenye urefu wa mita 525.

Amesema mradi huo ni sehemu ya barabara za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inayounganisha nchi mbili za Kenya na Tanzania kwa ukanda wa Pwani.

“Barabara hii ipo kwenye ushoroba wa Pwani ya Afrika Mashariki unaoanzia katika Mji wa Malindi na kupitia Miji ya Mombasa na Lungalunga kwa upande wa Kenya na Horohoro, Tanga, Pangani hadi Bagamoyo kwa upande wa Tanzania wenye urefu wa jumla ya kilomita 454,” amesema.

“Ujenzi wa Barabara hii ukikamilika utachochea ukuaji wa uchumi ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama na muda wa usafiri, urahisishaji wa kufanya biashara na kuwezesha wananchi kuchangamana kwa urahisi, kuwezesha kufikika kwa urahisi kwenye vivutio vya utalii,” amesema Besta.

Besta amesema barabara hiyo itakuwa kiungo kizuri kati ya Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mombasa na kuchochea uchumi wa Buluu.

“Barabara hii ikikamilika itakuwa kiungo kizuri na barabara za ushoroba wa Kaskazini mwa nchi yetu ya Tanzania, mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara pia kuunganisha shoroba nyingine za kati, kusini na magharibi,” amesema.

Amefafanua kuwa barabara hiyo pia itakuwa kiungo kizuri cha nchi za Kusini mwa Afrika pamoja na nchi za maziwa makuu ambazo ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Burundi na Rwanda.

Rais Samia agawa boti 35 Pangani

Awali, Rais Samia alizindua awamu ya pili ya ugawaji wa boti 35 mkoani Tanga ambapo Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Ashatu Kijaji amesema Sh11.5 bilioni zilizonunua boti 160 kwa awamu ya kwanza na kusambazwa maeneo yote yenye wavuvi ya ukanda wa Pwani, Ziwa Victoria, Tanganyika na Ziwa Rukwa.

“Kwa ukanda wa Pwani tulipeleka boti 88, Mkoa wa Tanga ulipata boti 14, Dar es Salaam tano, Lindi 32, Mtwara 18 na Pwani 19. Mheshimiwa Rais (Samia), naomba kusema mradi huu unaendelea vizuri na hapa Pangani wavuvi wameendelea kunufaika,” amesema Dk Kijaji.

Dk Kijaji amesema mradi wa boti za kisasa zinatolewa na Serikali zimesaidia kuwawezesha wavuvi kufanya shughuli zao kwa uhakika na kujiingizia kipato katika maeneo mbalimbali.

Dk Kijaji amesema baada ya mradi huo kuwa na maendeleo mazuri walipeleka mapendekezo kwa Rais Samia, mwaka 2024/25 Serikali iwaongezee fedha ili kuendelea na uwezeshaji wa boti.

“Mheshimiwa Rais tunashukuru Serikali ilitupatia tena Sh11.5 bilioni zilizonunua boti 120. Kwa maelekezo yako ulituambia tukawatafute wavuvi,  mwaka huu  tutawagusa wavuvi 1, 870.

“Tunakwenda kugusa maisha yao, mifuko yao, wanawake na vijana wanaohusika na miradi ya uvuvi. Katika boti 120, 70 zitakwenda ukanda wa Pwani na 29 Ziwa Victoria wakati 21 zitakwenda Ziwa Tanganyika na Nyasa,” amesema Dk Kijaji.

Related Posts