Papa ateua askofu msaidizi Jimbo Kuu Katoliki Tabora

Dar es Salaam. Papa Francis amemteua Padri Josaphat Bududu wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora, kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Februari 26, 2025 na Padri Charles Kitima, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Mteule Bududu alizaliwa Machi 26, 1977 wilayani Kaliua, Jimbo Kuu Katoliki Tabora.

Baada ya masomo na majiundo ya kipadri alipewa daraja takatifu la upadri Julai 9, 2009 jimboni humo alikohudumu katika nafasi mbalimbali za utume.

Amesema alitunukiwa Shahada ya Uzamili katika Fani ya Tasaufi, kutoka Taasisi ya Kipapa ya Mtakatifu Petro- Bangalore-India mwaka 2014.

“Aidha, taasisi hiyo ilimtunuku Shahada ya Uzamivu katika fani hiyo mwaka 2019,” imeeleza taarifa hiyo.

Askofu mteule Bududu tangu mwaka 2023 hadi sasa, amehudumu nafasi ya makamu wa askofu kwa watawa Jimbo Kuu Tabora na mwalimu katika Seminari Kuu ya Kipalapala.

“Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, linamwombea Mhashamu Askofu Mteule Josaphat Jackson Bududu afya ya mwili na roho katika utume huo mpya,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Related Posts