Na Mwandishi Wetu
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM)kimeombwa kuunda chombo maalum kwa ajili ya kufuatilia tuhuma mbalimbali zinazotolewa na baadhi ya makada wa Chama hicho kwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Rorya Ongujo …pamoja na mbunge wa jimbo hilo Jafari Chege.
Kwa mujibu wa makada wa Chama hicho wamewaambia waandishi wa habari leo Februari 25,2025 jijini Dar es Salaam kuwa Mwenyekiti na Mbunge wamekuwa na mwenendo wa matukio yanayoashiria kuvuruga utulivu hasa wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.
Akizungumza kwa niaba ya makada wenzake,Kada wa Chama hicho kutoka Wilaya ya Rorya Baraka Otieno amedai viongozi hao wamekuwa wakitumia fedha na nafasi zao kuvunja katiba ya chama hicho na kuondoa utulivu uliopo .
“Tumeshuhudia Mwenyekiti na Mbunge wakigawa fedha kwa washiriki wa mafunzo ya utendaji yaliyoandaliwa na Chama hicho kwa ajili ya kuwajengea uelewa watendaji wa Chama chetu.
“Mafunzo hayo yaliyofanyika Februari 21 mwaka huu yaligharamiwa na Chama na yalitolewa maelekezo kwamba ni marufuku kwa mtu yeyote kutoa fedha au kitu chochote kwa washiriki lakini Mwenyekiti na Mbunge waligawa fedha Sh.50,000 kwa kila mshiriki na hii imetafsiriwa ni rushwa.
” Nipo hapa kwa ajili ya kukilinda, kukemea na kueneza chama hiki kwani chama chetu kinaaminiwa na watanzania na ndio maana kinapewa dhamana ya kuongoza nchi, hivyo tumekuja mbele yenu kueleza haya ambayo hatufurahishwi nayo na tunaomba kiunde chombo maalum kuchunguza haya tunayosema kwani ushahidi tunao.”
Kada huyo ambaye amewahi kufanyakazi Makao Makuu ya Chama katika idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa amedai pia Mwenyekiti huyo amekuwa akimnadi na kumpigia debe Mbunge wa Rorya Jafari Chege
“Mwenyekiti wa CCM Rorya amekuwa akitangaza hadharani kumuunga mkono mbunge na wakati anajua kufanya hivyo ni kinyume na Katiba yetu ya Chama kwani yeye kama kiongozi wa chama ndio baba wafamilia.
“Hatufanyi siasa za maji taka bali tumekuja na ushahidi clip mbalimbali na katika vikao na mikutano amekuwa akitangaza kumuunga mkono mbunge wa sasa.Pia Mwenyekiti huyo Wilaya ya Rorya amekuwa akitoa maelekezo ya kuwasimamisha na kuwafukuza baadhi ya viongozi wa mashina,tawi na kata ambao hamuungi mkono mbunge wa sasa na baadhi ya madiwani.”
“Kutokana na maelezo haya ndio
maana tunashauri au kuomba chama kuunda chombo maalumu kitakachofuatilia haya yote.WanaCCM wa Rorya wanakipenda Chama chetu lakini haya yanayoendelea yanasababisha chama kichukiwe.” Amedai kada huyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Rorya Ongujo amesema tuhuma zinazoelelezwa dhidi yake hazina ukweli wowote na anachokiona kuna vita ya ubunge na kufafanua anashangazwa na wanaotoa taarifa zisizo na ukweli wowote.
Kuhusu madai ya kutoa fedha kwa wajumbe walioshiriki mafunzo ya utendaji hayana msingi wowote na wala sio vibaya kutoa asante kwa mtu ambae anafanya vizuri na yeye amekuwa akishiriki na wana CCM katika masuala mbalimbali yanayohusu Chama na hakuanza leo wala jana ni muda mrefu.
“Kwanza siku ambayo kulikuwa na mafunzo kwa watendaji mbunge alikuwa msibani na mimi nilifika ukumbini mwishoni kuwasalimia washiriki wa mafunzo hayo.Mimi ni Mwenyekiti wa chama chetu Wilaya na ndio nasimamia Ilani.
“Kwa mujibu wa Katiba kwa nafasi yangu natakiwa kufanya kazi na viongozi waliopo na pale watakapokuja wengine nitashirikiana nao.Kwa sasa kuna madiwani na Mbunge hivyo siwezi kuacha kuwataja maana hakuna wengine.”