Shinyanga. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema angependa kuona wananchi wa Kahama wanashirikiana na kuungana kwa pamoja katika shughuli za maendeleo ya wilaya yao.
Aidha, amewaasa kutoacha msingi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wa kuwaletea wananchi maendeleo.
Amesema Taifa linakitegemea chama hicho kiwahudumie na sio kuruhusu mipasuko miongoni mwao.
Dk Biteko ameyasema hayo jana Jumanne Februari 25, 2025 akiwa mjini Kahama, mkoani Shinyanga, aliposhiriki mkutano maalum wa CCM Jimbo la Msalala, uliolenga kuwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho ya mwaka 2020-2025.
Akizungumzia fursa za maendeleo zilizopo wilayani humo, Dk Biteko amesema Kahama ni Wilaya ya kimkakati ambayo ina bandari kavu iliyopo Isaka na Serikali inaenda kujenga kiwanda cha kuchenjua madini pamoja na uwepo wa barabara inayoounganisha nchi za maziwa makuu.
“Kutokana na uwepo wa fursa hizi, tukishindwa kuungana tukashughulika na maendeeo ya watu, basi watatushangaa. Nataka nitoe wito, pendaneni, shikamaneni Mungu amewapa kila aina ya utajiri, tumieni fursa hiyo kujiletea maendeleo kwenye wilaya yenu na msiruhusu mipasuko katika chama chetu,” amesema naibu waziri mkuu huyo.
Ametoa rai kwao kuwa baada ya mkutano huo watoke wakiwa wamoja na waweke mbele maslahi ya CCM na ya Watanzania.
Lakini pia amempongeza Mbunge wa Msalala, kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuhakikisha wananchi wa Jimbo hilo wanapata miradi ya maendeleo na hivyo kutatua changamoto walizokuwa nazo awali.
Katika hatua nyingine, Dk Biteko ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha nyingi katika Jimbo hilo ambazo zimetumika kutekeleza miradi mbalimbali ikiwamo ya maji, elimu, afya na miundombinu.
“Rais Samia amefanya makubwa katika nchi yetu, leo tunazungumza kuhusu miradi mingi na mikubwa hapa Kahama, tunazungumzia kujengwa kwa barabara ya Kakola kwa kiwango cha lami. Amefanya uchimbaji madini ubaki kwenye maendeleo yetu anataka uwepo wa miradi mingi zaidi ya barabara na maji, niwaombe tumuombee ili aendelee kutimiza haya kwa ajili ya Watanzania,” amesema Biteko.
Amesema Serikali bado ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha Watanzania wote wanapata maendeleo na kuishi katika mazingira bora zaidi.
“Wito wangu kwenu shikamaneni, pendaneni, vumilianeni tukijenge chama chetu, na wakati wa uchaguzi, basi chagueni anayefanya kazi mwacheni anayesema watu. Mbunge Iddi endelea kuchapakazi kwa maendeleo ya Jimbo lako,” amesisitiza Dk Biteko.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Msalala lililopo Mkoa wa Shinyanga, Iddi Kassim Iddi wakati akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa Jimbo hilo kwa Mwaka 2020/2025 amempongeza Dk Biteko kwa hatua ya kuendeleza sekta ya nishati kwa kusaidia vitongoji vyote vya Jimbo hilo kupata umeme.
“Serikali inaendelea na azma yake ya kusambaza huduma za umeme katika vijiji vyote nchini. Hapa tumejulishwa kuwa Msalala ina jumla ya vijiji 92, ambavyo vyote vimefikiwa na huduma ya umeme, kazi iliyobaki ni kupeleka umeme katika vitongoji,” amesema mbunge huyo.
Akizungumzia sekta ya maji, Iddi amesema mwaka 2020 hadi 2025, Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali zikiwamo Sh2 bilioni za miradi ya maji yatakayo sambazwa katika vijiji mbalimbali.
Amesema mafanikio ya miradi hiyo imesaidia Jimbo hilo na sasa wanaendelea kusambaza maji katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma hiyo hususan katika vitongoji.
“Wakati naingia madarakani, miradi ya maji ilikuwa kwa asilimia 25 pekee na sasa miradi ya maji imefikia asilima 95,” amesema Mbunge Iddi.
Akizungumzia sekta ya elimu, mbunge huyo amesema Serikali imeboresha kwa kutoa fedha zilizosaidia utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa madarasa, mabweni na maabara.
“Tumekuwa na shule nyingi, jambo linalotuwezesha kuwapatia watoto wetu elimu bora na ya kutosha. Vilevile, tumeanza ujenzi wa Chuo cha Veta ambacho, kitakapokamilika, kitatoa manufaa makubwa kwa jamii, hasa kwa vijana, kwa kuwapa ujuzi unaowawezesha kuajirika katika soko la ajira,” amesema Iddi.
Kadhalika, kuhusu sekta ya barabara, amesema katika kipindi cha miaka mitano, Jimbo hilo kwa kushirikiana na Tarura imefungua barabara nyingi, ikiwemo ya Kakola hadi Kahama, ambayo sasa inapitika vizuri.
Aidha, amemshukuru Serikali kwa kutekeleza Ilani ya CCM katika Jimbo hilo kwa asilimia 99.