Ushirikiano mpya wa mashirika, viwanda vya kijeshi Afrika Mashariki

Dar es Salaam. Ushirikiano wa Mashirika na Viwanda vya kijeshi vya Afrika Mashariki katika kubadilishana teknolojia za uzalishaji vifaa na bidhaa mbalimbali ni miongoni mwa yaliyojadiliwa katika mkutano uliowaketisha watendaji wakuu wa Mashirika na Viwanda vya Kijeshi vya Jumuiya hiyo.

Huku ajenda ya matumizi ya teknolojia katika kuzalisha bidhaa za kilimo, magari ya kijeshi, mabomu, risasi, matrekta, korosho matunda, majiko, mashine, taa kwenye viwanda hivyo ikitawala.

Imeelezwa bidhaa hizo zinapaswa kuuziana kwa nchi wanachama kuliko kuagiza kutoka nje, hivyo teknolojia inapaswa kutumika ili kuzalisha bidhaa bora na za kisasa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano, Februari 26, 2025 baada ya kufungwa kwa mkutano huo uliofanyika kwa siku mbili jijini hapa kuanzia jana, Brigedia Jenerali Seif Hamisi amesema lengo ni kuweka pamoja viwanda vya kijeshi.

“Tunaangalia fursa gani tunazo na mambo gani tunaweza kubadilishana kwa mustakabali wa mashirika yetu. Kwa hapa nchini tuna shirika la Suma JKT, Nyumbu lililopo Kibaha na Mzinga lililopo Morogoro,” amesema.

Brigedia Jenerali Hamisi ambaye ni Meneja Mkuu wa Shirika la Mzinga amesema vikao hivyo hufanyika mara moja kwa mwaka katika kila nchi na  mwaka huu ilikua zamu ya Tanzania.

Awali, akitoa hotuba yake ya kufunga Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Luteni Jenerali Salum Othman amesema majeshi yanahitaji vifaa mbalimbali ili kutekeleza ipasavyo majukumu yake.

 “Ili kupata vifaa hivyo, ambavyo ni ghali kwa kawaida tunaingia kwenye soko la kimataifa kuvinunua hatuna budi kushirikiana.

“Ni ushahidi wa juhudi zetu za pamoja za kukuza kujitegemea kikanda na kuuza bidhaa na malighafi zetu ndani ya jumuiya lakini pamoja na mafanikio hayo, napenda kuwasihi tusiridhike bali tufanye kazi kwa bidii ili kupata uhuru na kutegemeana zaidi,” amesema.

Amesema maendeleo yoyote endelevu ya viwanda hayawezi kujitenga na uwekezaji katika sayansi na teknolojia, pamoja na Utafiti na Maendeleo (R&D), hivyo eneo hilo ni muhimu kuzingatiwa.

Jana, akifungua mkutano huo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo alisema kutokana na kasi ya ukuaji wa teknolojia duniani viwanda hivyo havina budi kuzalisha bidhaa zinazoendana na kasi hiyo.

Sillo alisema kutokana na teknolojia kubadilika kwa kasi ameshauri kutobaki nyuma katika uzalishaji wa bidhaa na huduma zitolewazo.

“Inapaswa kwenda sambamba na teknolojia kwani inabadilika kila siku hivyo tusibaki nyuma. Ni vizuri kwenda nayo sambamba tushirikishane kwenye uzalishaji wetu tusije kuzalisha vifaa vilivyopitwa na wakati,” alisema Sillo.

Related Posts