Ujumbe wa Kwaresima wa Papa Francis kwa 2025

Dar es Salaam. Siku sita kabla ya kuanza kwa kipindi cha Kwaresima mwaka 2025, Papa Francis ametoa ujumbe kwa waumini wa Kanisa Katoliki ukiongozwa na kaulimbiu “Tembeeni pamoja kwa matumaini”, akisisitiza kuwa hakuna anayepaswa kuachwa nyuma. 

Kaulimbiu hiyo inawahimiza waumini kusafiri pamoja kama mahujaji wa matumaini kuelekea nchi ya ahadi, wakihakikisha hakuna anayeachwa au kutengwa, huku wakidumisha tumaini lisilokatisha tamaa. 

Machi 5, 2025 waumini wa Kanisa Katoliki kote duniani wataanza kipindi cha Kwaresima, ambacho ni hija ya kiroho ya kukumbuka mateso, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo msalabani.

Kipindi hiki cha siku 40 kitaanza kwa ibada ya kupakwa majivu kwenye paji la uso ambayo ni ishara ya toba na mwanzo wa safari ya kila mwaka ya Kwaresima, inayojengwa juu ya imani na matumaini. 

Kwa mujibu wa tovuti ya Vatican News, ujumbe wa Papa Francis ulitiwa saini jijini Roma katika Kanisa la Mtakatifu Yohane wa Laterano Februari 6, 2025 siku ya kumbukizi ya mashahidi wa imani Watakatifu Paulo Miki na wenzake. 

Wito wa kutembea pamoja 

Katika ujumbe wake, Papa amesema Kwaresima ya mwaka 2025 inapata maana ya kipekee kwa kuwa inaambatana na maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei.

Amesema:  “Katika kipindi hiki cha Kwaresima, ninapenda kushiriki nanyi tafakari kuhusu maana ya ‘kutembea pamoja kwa matumaini’ na wito wa uongofu ambao huruma ya Mungu inatualika kuuishi, si tu kama watu binafsi bali pia kama jamii.”

Papa ameeleza kuwa kaulimbiu ya Jubilei ya 2025 inayosema: “Mahujaji wa Matumaini” inahusiana moja kwa moja na safari ya wana wa Israeli kuelekea nchi ya ahadi. 

“Ni safari inayohitaji uvumilivu na imani, kwa kuwa kutoka utumwani kuelekea uhuru si jambo rahisi. Ni safari inayosimuliwa katika maandiko matakatifu, lakini pia ni safari halisi kwa kaka na dada zetu wengi wanaokimbia vita, umaskini na mateso, wakitafuta maisha bora kwa ajili yao na wapendwa wao,” amesema. 

Kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma 

Papa ameonya dhidi ya safari ya kiroho inayofanywa kwa ubinafsi, akisema kuwa Wakristo wanapaswa kutembea pamoja, wakisaidiana bega kwa bega. 

“Kutembea pamoja kunamaanisha kujenga mshikamano na umoja, tukizingatia kuwa sote ni wana wa Mungu (Gal 3:26-28). Tunapaswa kusonga mbele bila kumkandamiza mwingine, bila husuda au unafiki, bila kumwacha yeyote nyuma au kumtenga,” amesema. 

Amesema katika Kwaresima hii, waumini wanapaswa kutathimini iwapo wanatembea pamoja katika maisha yao ya kila siku kwenye familia, maeneo ya kazi, parokia na jumuiya za kitawa. 

“Je, tunasikilizana kwa upendo na uvumilivu? Je, tunaweza kushirikiana kama maaskofu, mapadre, watawa na waumini walei kwa ajili ya ufalme wa Mungu? Je, tunawakaribisha wengine kwa moyo wa ukarimu au tunawaweka pembeni?” Papa amehoji. 

Amesema ujumbe mkuu wa Jubilei ni kuhakikisha safari ya Kwaresima inatupeleka hadi ushindi wa Pasaka, akirejea mafundisho ya Papa Benedikto XVI katika waraka wa Spe Salvi, kwamba: “Wanadamu wanahitaji upendo usio na masharti.” 

Papa amehitimisha kwa kusisitiza kuwa ufufuko wa Kristo unatoa wito wa toba na mabadiliko ya kweli ya moyo. 

“Tujitafakari: Je, nina hakika kuwa Mungu husamehe dhambi zangu? Au naishi kana kwamba naweza kujiokoa mwenyewe? Je, ninaishi kwa matumaini yanayonisukuma kujitolea kwa haki, udugu na utunzaji wa dunia yetu, huku nikihakikisha hakuna anayeachwa nyuma?” amehoji.

Related Posts