Tanzania mbioni matibabu, upasuaji kwa roboti

Dar es Salaam. Tanzania inakaribia kuingia katika teknolojia ya upasuaji kwa kutumia akili mnemba ‘roboti’ baada ya baadhi ya hospitali nchini kuanza maandalizi ya huduma hiyo kwa kutoa mafunzo kwa wataalamu.

Hospitali hizo ni pamoja na Taasisi ya Saratani Ocean Road ORCI, Hospitali ya Benjamin Mkapa BMH na Hospitali ya Saifee Tanzania.

Desemba 31, 2024 Hospitali ya Benjamin Mkapa ilitangaza mipango yake ya kuwekeza katika teknolojia ya upasuaji kwa kutumia roboti  ili kurahisisha kazi kwa wataalamu na kuboresha huduma za afya.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano, Februari 26, 2025 Meneja wa Saifee, Dk Hussain Saifuddin, amesema hiyo ni hatua kubwa ya kuhamasisha uvumbuzi wa afya nchini.

“Huduma hii inasaidia kuokoa muda, ni njia nzuri ya kuongeza usahihi na ukamilifu wa upasuaji, tafiti za upandikizaji na mengineyo ya kimaabara, kwa njia ya akili mnemba,” amesema na kuongeza:

“Mwaka huu tunaandaa mazingira wezeshi ya vifaa na kupata wataalamu, maana matumizi yake yanaendana na uelewa katika teknolojia ya akili mnemba. Mungu akijaalia, mambo yakiwa mazuri mwishoni mwa mwaka huu tutaanza matumizi ya awali.”

Mapema wiki hii, madaktari wa Tanzania wamepewa njia mpya ya kutoa huduma za kiafya kwa kutumia roboti,  ikiaminika kwamba ni njia salama, inaokoa muda na kuepusha makosa ya kibinadamu, elimu iliyotolewa na madaktari bingwa kutoka nchini India.

Washa hiyo iliyofanyika katika Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam, ilifungua mbinu za kiafya ambazo hazikuwa rahisi kufanyika na zenye hatari na kuzifanya kuwa salama zaidi  kwa njia ambayo haijawahi kuonekana kabla hapa nchini.

Daktari bingwa wa upasuaji kutoka India Dk Urvakish Bhota, amesema upasuaji kwa kutumia roboti,  ni njia bora na salama  na inaokoa muda na makosa madogo madogo ya kibinadamu wakati wa utendaji kazi wake.

“Kwa sasa tunaweza kutumia roboti katika kufanya shughuli zetu nyingi tu wakati wa utoaji wa huduma za kiafya kama upasuaji, utoaji wa dawa, kutambua magonjwa mwilini na kuua seli mwilini au kupunguza uvimbe,” amesema Dk Bhota.

Akitoa maelezo ya kufunga warsha hiyo mmiliki wa Hospitali ya Heameda iliyopo Bunju B jijini Dar es Salaam Dk Henry Mwandolela,  amesifia huduma hio kwa kusema ni bahati kwa Watanzania kama nchi inayoendelea kwa kutumia njia ya kisasa kwenye shughuli za kiafya.  

“Nafikiri mmechagua nchi kwa usahihi, tunahitaji teknolojia, hii ni ukweli, na sio hadithi, wachache wanatumia hii duniani. Ni kitu kipya nchini Tanzania na tuna furaha kukaribisha utendaji wake nchini,” amesema Dk Mwandolela. 

Related Posts