Wanafunzi 30 waliolazwa kwa kuangukiwa na ukuta wa darasa Same, waruhusiwa

Same. Zaidi ya wanafunzi 30 wa Shule ya Sekondari ya Tumaini Jema, wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro waliojeruhiwa kwa kuangukiwa na jengo la darasa na kulazwa Hospitali ya Wilaya ya Same, wameruhusiwa jioni hii baada ya afya zao kutengemaa.

Wanafunzi hao wa kidato cha kwanza katika shule hiyo, waliangukiwa na jengo hilo Februari 25, 2025 wakati wakiwa darasani  na kusababisha majeruhi, huku mwalimu mmoja aliyekuwa akiwafundisha wanafunzi hao akijeruhiwa na kuzuia taharuki shuleni hapo.

Hata hivyo, baada ya kutokea maafa hayo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Kasilda Mgeni aliagiza kusitishwa kwa masomo katika shule hiyo kwa siku saba mpaka uchunguzi utakapokamilika.

Pamoja na kusitisha masomo katika shule hiyo, aliagiza Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) pamoja na wataalamu wa ujenzi wa halmashauri hiyo kufanya uchunguzi wa kina, kuhusu tukio hilo pamoja na kukagua ubora wa majengo ya shule hiyo.

Akizungumzia hali za majeruhi hao, Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk Alex Alexander amesema wanafunzi wote 31 tayari wameruhusiwa jioni hii na hali zao ni nzuri.

“Majeruhi wote ambao walikuwa wamelazwa Hospitali ya Wilaya ya Same ambao ni wanafunzi na mwalimu mmoja wote wameruhusiwa baada ya afya zao kurejea katika hali ya kawaida,”amesema Dk Alexander.

Hata hivyo, mkuu huyo wa wilaya amewataka wakuu wa shule binafsi kuhakikisha wanajenga majengo yenye kukidhi viwango ili kulinda usalama wa wanafunzi, pamoja na watumiaji wengine wa majengo hayo.

Related Posts