BAADA ya kuvuna pointi nane katika mechi tano zilizopita katika Ligi Kuu Bara, wachimba dhahabu wa KenGold leo jioni itashuka tena uwanjani kuikabiliana na wenyeji wao, maafande wa JKT Tanzania, wakati Azam FC iliyotoka kuisimamisha Simba itaialika Namungo mechi zote zikipigwa jijini Dar.
KenGold iliyopanda daraja msimu huu sambamba na Pamba Jiji, katika duru la pili la Ligi Kuu imeonekana kuja kivingine kutokana na kujiimarisha kupitia dirisha dogo la usajili na hadi sasa usajili huo umeonekana kulipa zaidi kwa kuvuna alama nane kupitia mechi tano zilizopita, tofauti na ilivuna sita katika mechi 16 ilizocheza tangu Ligi ilipoanza Agosti 13 na kusimama Desemba 29 mwaka jana.
Licha ya kuwa ugenini, lakini KenGold inajivunia ushindi wa bao 1-0 iliyopata ikiwa nyumbani dhidi ya wapinzani wao hao wa JKT Tanzania ambao katika mechi tano ziliziopita za Ligi, imevuna pointi saba kupitia ushindi mara mbili na suluhu moja mbele ya Yanga, huku ikipoteza michezo miwili.
JKT inaialika KenGold ikiwa imetoka kushinda mechi mbili mfululizo zilizopita kwa mabao 2-0 kila moja dhidi ya Kagera Sugar na KMC iliyoibana KenGold katika mechi iliyopita na kutoka sare ya 1-1 baada ya awali kuizima pi Kagera kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.
Kwa hesabu za timu zote zilizoanza na mto duru la pili ni wazi leo kutakuwa na burudani kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, ambao awali ulikuwa mgumu kwa wageni kupata ushindi kabla ya Singida Black Stars kuvunja mwiko walipoilamba JKT kwa bao 1-0 mechi iliyopigwa Februari 13.
KenGold itaendelea kumtegemea Seleman Rashid ‘Bwenzi’ aliyefunga mabao manne katika mechi tano ziliziopita, mbali na nyota wapya walitua kupitia dirisha dogo kama beki Kelvin Yondani, kiungo Zawadi Mauya, washambuliaji Obrey Chirwa na wengine waliokuwapo kama Mishamo Davidi.
Hata hivyo, wageni hao wa ligi wanapaswa kuwa makini katika pambano hilo, kwani JKT ina mastaa wenye uwezo mkubwa wa kuamua mechi hiyo na ukuta mgumu unaolindwa na Wilson Nangu na Edson Katanga huku kipa Yakoub Seleman akiwa imara langoni kuhakikisha maafande hao hawafungwi kirahisi na kuifanya JKT iwe nafasi ya sita kwa sasa na pointi 26 kupitia mechi 21. Katika mechi tano zilizopita, JKT imefunga mabao matano na kufungwa matatu tu, huku mechi tatu Yakouv akiondoka na clean sheet, tofauti na KenGold katika mechi kama hizo, imefunga mabao sita na kufungwa manane.
KenGold inayoburuza mkia kwa sasa ikiwa na poiti 14 kupitia mechi 21 itakuwa na kazi ya kuwachunga kina John Bocco, Shiza Kichuya, Edward Songo, Hassan Dilunga na Najim Magulu ambao wamekuwa wakiibeba timu hiyo katika mechi zilizopita, ili isiendelee kuruhusu mabao mengi zaidi.
Makocha wa timu hizo, Ally Ahmad wa JKT na Omary Kapilima wametambiana kila mmoja akijinasibu kwamba mchezo utakuwa mgumu, lakini pointi tatu lazima zichukuliwe, hivyo dakika 90 zitaamua mtanange huo utakaoanza saa 10:15 jioni.
Azam iliyotoka kuitibulia Simba wimbi la ushindi kwa kuchomoa bao jioni na kutoka sare ya 2-2 saa 1:00 usiku itakuwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi kuipokea Namungo katika mechi nyingine kali inayopigwa leo katika mfululizo wa Ligi Kuu Bara iliyopo raundi ya 22.
Hili ni pambano la 12 kwa timu hizo kukutana katika Ligi Kuu Bara tangu Namungio ilipopanda daraja msimu wa 2019-2020, huku rekodi zikiibeba zaidi Azam kwani katika mechi hizo imeshinda sita na kupoteza tatu na michezo miwili imeisha kwa sare tofauti.
Azam hata katika mechi nyingine bado imekuwa wababe wa Namungo kwani ilishaifyatua katika Kombe la Shiriksho kwa mabao 4-1 Mei 3 mwaka jana na zilipokutana kirafiki Januari 6, 2022 bado Wanalambalamba walishinda kwa bao 1-0 kuonyesha wanaijulia mno Namungo uwanjani.
Hata hivyo, bado pambano la leo halitabiriki kirahisi kama walivyosema makocha wa timu hizo, Juma Mgunda wa Namungo na Rachid Taoussi, kwani kila mmoja anahitaji matokeo mazuri kujiweka pazuri katika msimamo wa Ligi unaoongozwa kwa sasa na Yanga yenye pointi 55 baada ya mechi 21.
Azam ipo nafasi ya tatu kwa sasa ikiwa na pointi 44 katika mechi 21, wakati Namungo ni ya 12 ikiwa na pointi 22 kwa idadi kama hiyo ya mechi na mchezo uliopita ilibanwa nyumbani na Coastal Union kwa kutoka suluhu.
Timu hizo zinakutana, huku kila moja ikiwa haina matokeo mazuri kwani katika mechi tano zilizopita, Azam imeshinda mbili tu dhidi ya KMC na Mashujaa kwa kuzilaza 2-0 kila moja, huku ikipoteza moja kwa Pamba Jiji iliyowanyoa 1-0 na mbili zilizopita imetoka sare mfululizo dhidi ya Coastal na Simba.
Kwa upande wa Namuno katika mechi hizo tano, imeshinda mara moja tu kwa kuifyatua TZ Prisons ikiwa kwao jijini Mbeya, ikapoteza mbili mbele ya Simba na Tabora United na kutoka sare mbili pia na Coastal na Dodoma Jiji, huku ikiruhusu mabao saba na kufunga manne tu. Azam yenyewe imefunga mabao sita na kufungwa matatu.
Azam itaendelea kuwategemea Feisal Salum ‘Fei Toto’ mwenye mabao manne na asisti 11, Nassro Saadun mwenye mabao manne pia, Zidane Sereri ambaye aliingia dirisha dogo akitokea Dodoma Jiji na moto wake umeonekana kuchoma mapema, mbali na wakali wengine.
Namungo inamtegemea zaidi, Pius Buswita, Erasto Nyoni na Jacob Massawe ambao ndio vinara wa mabao, licha ya kuwepo kwa wakali wengine kikosini walioingia dirisha dogo akiwamo Saleh Karababa na Najim Mussa ‘Maestro’ aliyetokea Tabora United.
Katika mechi ya mwisho baina ya timu hizo, Azam ilishinda bao 1-0 ugenini likiwekwa kimiani na beki na nahodha wa timu hiyo, Lusajo Mwaikenda aliyemaliza kona ya Fei Toto, hata hivyo Namungo wamekuwa na zali la kuifyatua Azam ikiwa uwanja wa nyumbani kwani katika mechi tatu ilizoshinda mbele ya Matajiri hao wa Chamazi, mbili ilishinda Azam Complex na moja tu ilishinda Ruangwa Lindi.
Na hata sare mbili zilizopatiana baina ya timu hiyo katika Ligi tangu 2019, moja ilipatikana Chamazi, hali inayofanya pambano laa leo kushindwa kutabirika kirahisi hadi baada ya dakika 90.