Mwamvua Mwinyi, Chalinze Februari 27, 2025
Shule ya Sekondari Kibindu, iliyopo Kata ya Kibindu, Jimbo la Chalinze, Mkoani Pwani, ina jumla ya mabweni manne ya wasichana, lakini idadi ya wanafunzi wanaoishi kwenye mabweni hayo haifikii nusu ya wanafunzi wa kike 300 wanaosoma shuleni hapo.
Aidha, shule hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa maji ya uhakika, hali inayowalazimu wanafunzi kutembea umbali wa kilomita nne kwenda na kurudi kutafuta maji, ambayo mara nyingi ni maji chumvi.
Hali hii ilibainika wakati maofisa wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya MAMA SAMIA kutoka Halmashauri ya Chalinze walipotembelea Shule ya Sekondari Kibindu kutoa elimu kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia, malezi bora, na sheria ya mtoto ya mwaka 2009.
Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Chalinze, Atuganile Chisunga, alisisitiza umuhimu wa wazazi kutambua hatari itakayowakumba watoto wa kike wanapokuwa nje ya shule.
Alieleza kuwa ,maeneo ya vijijini yanakuwa na vishawishi vingi kwa watoto, ikiwemo kupata mimba za utotoni, magonjwa ambukizi,vibanda vya video, mikusanyiko isiyofaa, biashara haramu za dawa za kulevya .
Chisunga alieleza ,suala la ukosefu wa mabweni ya wavulana ni changamoto inayohitaji kutatuliwa na mamlaka husika kwa kuwa wanafunzi wa kiume wanakosa makazi salama, hivyo wengi wao huishi mitaani jambo linalowafanya kuwa na changamoto ya kimaadili.
Nae Kaimu Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Laban Sagati Simon, alieleza mabweni ya wasichana ni manne, na wanafunzi wanatakiwa kulipa Sh. 75,000 kwa miezi mitatu ili kuishi kwenye mabweni hayo.
Vilevile aliongeza kuwa, wanafunzi wa kiume hawana mabweni, hivyo wengi wao huishi nyumba za mitaani jambo linalochangia kushindwa kufuatilia ratiba za masomo ya ziada
“Kitendo cha wanafunzi kupanga vijijini,mitaani nje ya shule, kinaathiri maadili yao kwani hawana wa kuwafuatilia mienendo yao, “Hawawezi kuhudhuria masomo ya ziada ya jioni au kujisomea usiku, hivyo matokeo yao kitaaluma yanashuka,” alisema Laban.
Akizungumzia changamoto ya maji, Laban alieleza kuwa shule inapata maji mara moja kwa mwezi, na hayo hayatoshi kwa idadi kubwa ya wanafunzi zaidi ya 600 na walimu.
“Tunatumia pipa kuleta maji kutoka umbali mrefu wa kilomita nne, lakini kutokana na wingi wa wanafunzi, hayatoshi,” alifafanua.
Baraka Kito, kaka mkuu wa shule hiyo, alisema kuwa kuna wanafunzi wanaoishi umbali wa kilomita 10 kwenda na kurudi, na kutokana na ukosefu wa mabweni ya wanafunzi wa kiume, wanaishi kwenye nyumba za kupanga kwa gharama za Sh. 5,000 hadi 15,000.
“Wengine wanalipiwa na wazazi wao, huku baadhi yao wakijilipia kutokana na wazazi kutokuwa na kipato cha kutosha.”
Mmoja wa wanafunzi anayeishi kwenye nyumba za kupanga (jina lake limehifadhiwa) alifafanua, mama yake hana uwezo wa kifedha na ameachwa na baba yake, Familia inamtegemea, hivyo anapokuwa likizo, hulazimika kujishughulisha na ajira ndogondogo ili aweze kulipa kodi ya nyumba na gharama nyingine za shule.
Diwani wa Kata ya Kibindu, Ramadhan Mkufya, alithibitisha kuwa hali ya wanafunzi kupanga vijijini ni changamoto kubwa, kwani wazazi wanawalipia nje zaidi ya 200,000 wakati shule wanatakiwa kulipa Sh. 75,000 kwa miezi mitatu kwa ajili ya malazi .
Mkufya alionya kuwa, maisha ya watoto hao vijijini yanaweza kuathiri maadili yao, jambo linaloweza kusababisha mimba za utotoni, kujiingiza kwenye magenge ya bangi, na vishawishi vingine vinavyoweza kuathiri mustakabali wao.