KLABU ya Azam inatarajia kufanya mabadiliko makubwa katika safu ya ushambuliaji mwishoni mwa msimu huu ikiwamo kumtema mshambuliaji wa kati, Jhonier Blanco aliyeshindwa kuonyesha kiwango cha juu tangu alipojiunga na timu hiyo.
Blanco, aliyesajiliwa kutoka Rionegro Aguila ya Colombia, alitarajiwa kuwa mchezaji muhimu katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo, lakini hadi sasa ameshindwa kumudu changamoto za Ligi Kuu Bara, akiwa na mabao mawili na asisti moja. Akiwa Colombia mwaka 2023 akiwa na timu ya Fortaleza alifunga mabao 21 katika mechi 35 kabla ya kutua Rionegro aliyoipandisha daraja akiifungia mabao 19.
Kushindwa kwake kutamba na Azam, kumeibua maswali kuhusu uwezo wake wa kuendana na mtindo wa soka la Tanzania, jambo ambalo limewafanya viongozi wa Azam kuanza kujadili uamuzi wa kumwacha mshambuliaji huyo.
“Blanco (Jhonier) amekuwa akionyesha changamoto katika kuonyesha makali yake katika timu yetu. Ingawa alikuja na matumaini makubwa, utendaji wake umekuwa chini ya matarajio, na sasa tunafanya tathmini ya mabadiliko ya mchezaji huyo,” alisema mmoja wa viongozi wa Azam FC aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina.
Kocha mkuu wa Azam, Rachid Taoussi anayefanya kazi na Blanco katika msimu huu, alieleza ana hitaji la mshambuliaji mwingine mwenye nguvu na uwezo wa kupambana na mabeki wa Ligi Kuu, akitaka mchezaji ambaye atakuwa na uwezo wa kuwa msaada kwa Nassoro Saadun katika safu ya mbele.
Kocha Taoussi alisema, ni muhimu timu kuwa na mshambuliaji mwenye ubora wa kimataifa ili kuwa na ushindani mzuri msimu ujao wa 2025/26.
“Msimu huu, tumekuwa na changamoto katika safu ya mbele. Tunahitaji mshambuliaji mwingine wa daraja la juu ambaye ataendana na mtindo wangu wa soka na kutoa mchango mkubwa kwa timu yetu. Siyo tu kwamba tunahitaji mchezaji anayefunga, bali pia mtu ambaye atasaidia kuimarisha mashambulizi,” alisema Taoussi.
Taarifa za ndani kutoka kwa viongozi wa klabu hiyo zinathibitisha kuwa Azam ipo kwenye mchakato wa kumaliza mkataba wa Blanco mwishoni mwa msimu huu, na tayari wameshaanza kutafuta mshambuliaji mpya mwenye uwezo wa kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji.
Mshambuliaji huyo mpya anatarajiwa kuwa na uwezo mkubwa wa kumalizia nafasi na kusaidia timu kupata ushindi kwenye mechi muhimu za ligi na michuano ya kimataifa.
“Azam ni klabu inayojivunia kuwa na wachezaji wa kiwango cha juu, na tumejipanga kuhakikisha kwamba tunapata mshambuliaji ambaye atakuwa na mchango mkubwa kwa timu,” alisema mmoja wa viongozi wa klabu.
Blanco, ambaye alijiunga na Azam FC akitokea Deportivo Pasto, amekumbwa na changamoto za kiufundi na kimazingira, jambo ambalo limeathiri ufanisi wake. Tofauti na mchezaji mwenzake wa Colombia, Yeison Fuentes Mendoza na Ever Meza ambao wamekuwa wakitumika mara kwa mara.
Mandoza ni beki wa kati anayetumika kikosi cha kwanza, wakati Ever ni kiungo mkabaji na amekuwa akiingia na kutokana kutokana na watu anaogombea nao namba eneo hilo kama Adolf Mtasigwa, James Akaminko, Yahya Zayd na Sospeter Bajana.