Bocco aukubali mziki wa Mzize, Ateba

NAHODHA wa zamani wa Simba na Taifa Stars ambaye kwa sasa anakipiga JKT Tanzania, John Bocco amemtaja Leonel Ateba (Simba) na Clement Mzize (Yanga) kuwa ni wachezaji halisi wa kati wenye uwezo wa kumiliki mpira na kufunga.

Bocco amesema Ateba ana uwezo mkubwa wa kufunga, kumiliki mpira na kulimiliki eneo la mbele vizuri kwa kujitegemea akiwa hamtofautishi sana na Mzize akicheza namba 9.

“Yaani wakitumika vizuri wanakupa kitu kikubwa sana, unajua aina za wachezaji zipo tofauti unakuta wachezaji wanacheza nafasi moja, ila aina ya uchezaji ni tofauti,” amesema na kuongeza:

“Tatizo linakuja ukija kuangalia kishabiki lazima shida ije maana utaangalia kitu unachokipenda au unachokijua wewe, ila ukienda kitaalamu

wala hutaangalia vingi utaangalia asili ya nafasi anayocheza ndio inavyotakiwa mtu acheze.”

Bocco amesema kuna tofauti ya aina anayotumia mchezaji kucheza na nafasi anayocheza inavyotakiwa kuchezwa, lakini Ateba ni suala la muda tu anaamini ni mshambuliaji mzuri.

“Ateba huu ni msimu wake wa kwanza ana vingi vya kujifunza na kuvizoea ili akupe angalau asilimia 90 ya uwezo wake. Tusubiri tuone,” amesema.

Bocco amezungumza hayo kwenye ukurasa wa mtandao wa kijamii ‘Instagram’ wa mchambuzi wa masuala ya mpira, Edo Kumwembe ambaye aliomba maoni kutoka kwa wadau wa soka juu ya uwezo wa mshambuliaji wa Simba, Ateba.

Ateba ambaye ni msimu wake wa kwanza kucheza soka Tanzania tayari amefunga mabao manane na kutoa asisti tatu za mwisho hivyo amehusika kwenye mabao 11 kati ya 35 yaliyofungwa na Simba.

Upande wa Mzize amehusika kwenye mabao 13 baada ya kufunga mabao 10 akiwa ni kinara wa upachikaji wa mabao 10 sawa na Jean Ahoua, pia ameasisti tatu.

Related Posts