NA WILLIUM PAUL, SAME.
WAJUMBE wa Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi mkoa wa Kilimanjaro wamewataka wakandarasi wa ukarabati wa skimu ya umwagiliaji ya Ndungu na Kihurio kuongeza kasi ili wananchi waweze kunufaika na fedha zilizowekezwa na serikali.
Kauli hiyo imekuja mara baada ya Kamati hiyo kufika katika skimu hiyo kukagua ukarabati wake ikiwa ni ziara ya ukaguzi wa Ilani ya uchaguzi katika wilaya ya Same.
Mjumbe wa Kamati hiyo, Best Simba alisema kuwa, lengo la serikali kutoa fedha za ukarabati wa skimu hiyo ni kuongeza tija kwa wananchi ambao ni wakulima.
Aliwataka wakandarasi ambao ni kampuni ya M/s Hemieri T Limited na M/s Ansil T Limited kuhakikisha mradi huo unakamilika kulingana na muda wa makubaliano yaliyopo katika mkataba.
Mradi huo wa ukarabati wa skimu ya umwagiliaji Ndungu na Kihurio unagharimu Bilioni 6.988 ambapo mradi huo umeanza kutekelezwa Novemba 8 mwaka 2024 na unatarajiwa kukamilika Mei 5 mwaka 2026 na mpaka sasa mradi umefikia asilimia 6.