DTB yaadhimisha miaka mitano utoaji huduma za bima ikiahidi makubwa

Dar es Salaam. Benki ya Diamond Trust Bank Tanzania PLC (DTB) kupitia idara yake ya bima (Bancassurance) imesema itaendelea kuongeza ufanisi sokoni na kutanua wigo wa kuwahudumia zaidi wananchi.

Hayo yamesemwa na Meneja wa Idara ya Bima (Bancassuarance) wa benki hiyo, Raymond Salemba wakati wa hafla ya kusherekea miaka mitano ya huduma ya bima katika benki hiyo, tangu ilipozinduliwa mwaka 2020.

Salemba amesema ili kuwafikia wananchi wengi zaidi DTB imeongeza ushirikiano na kampuni za bima kutoka sita hadi tisa na kuanzisha huduma ya bima kwenye matawi yake 29 kote nchini.

 “Tunaposherekea miaka hii mitano ya utoaji wa huduma za bima tumeongeza mapato kwa asilimia 168, ambapo kwa mwaka 2023 tulipata Sh3.7 bilioni kutoka Sh1.4 bilioni mwaka 2020,” amesema.

Salemba amesema ukuaji wa huduma za bima katika benki hiyo umekuwa wa kasi kwa mwaka 2024 ambapo ulikuwa kwa asilimia 50.

Meneja huyo ameongeza kuwa bima ya maisha na afya ambazo zimeongezwa kama huduma mpya kwenye benki hiyo zimeonyesha mafanikio makubwa.

“Tunapoadhimisha miaka mitano ya ukuaji huduma za bima kibenki, tumejipanga kuendeleza upatikanaji wa bima na kuimarisha ushawishi wa soko ili kuhakikisha Watanzania wengi wanafaidika na bima, tutaendelea kubuni mbinu mpya ya kuwafikia na kuwahudumia wateja wetu ili kukidhi matarajio yao,” amesema Salemba.

Akielezea uanzishwaji wa Idara ya DTB Bancassurance, Salemba amesema ilitokana na utekelezaji wa kanuni za Bima 2019 (Bancassurance), ambazo ziliruhusu benki kuwa mawakala wa bima.

Ili kufanikisha matakwa hayo ya kisheria Salemba amesema DTB inatoka huduma mbalimbali za bima kuanzia ya magari, nyumbani, bima mizigo katika usafirishaji na za afya.

Mbali na hayo aliishukuru Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira) kwa kuendelea kusimamia benki hiyo pamoja na kudhamini mchango wa Chama cha Mawakala wa Bima za Kibenki Tanzania (TBAA) kwa kuendelea kuimarisha huduma hiyo.

“Kwa kusherehekea mafanikio haya, tunathibitisha tena dhamira yetu ya ubunifu na ushirikiano ili kuhakikisha bima inawafikia Watanzania wengi zaidi,”amesema.

Akimwakilisha kamishna wa Tira, Veronica Julius amesema ni muhimu benki kupanua huduma zao za bima na kuanzisha ambazo zinahitajika na hazijafika kwenye jamii.

“Tira inatoa wito kwa taasisi za bancassurance kupanua upatikanaji wa bima, kuongeza wigo wa soko, na kuanzisha bidhaa zisizojulikana na mshirikiane na wadau wengine kuleta ubunifu kwenye huduma zenu mnazotoa kwenye jamii,” amesema.

Related Posts