MANYARA KUTUMIA BAJETI YA SHILINGI BILIONI 302.9 KWA MWAKA 2025/2026

Na Mwandishi wetu, Babati

MKOA wa Manyara wenye Halmashauri zake saba imeomba kuidhinishiwa Sh302.9 bilioni za mpango wa bajeti kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake kwa mwaka wa fedha wa 2025/2026.

Katibu Tawala msaidizi (Mipango na Uratibu) wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Manyara, Lusungu Mwilongo, akisoma rasimu ya mpango wa bajeti ya mkoa huo mjini Bahati kwenye kikao cha kamati ya ushauri (RCC) amesema makisio ya bajeti ni Sh302.9 bilioni.

Mwilongo amesema fedha hizo zinajumuisha Sh224.1 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh78.7 bilioni kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

Amesema ofisi ya mkoa huo imepangiwa Sh10.8 bilioni, halmashauri ya mji wa Babati Sh32 bilioni, wilaya ya Babati Sh59.1 bilioni na Hanang’ Sh56.1 bilioni.

Amesema Kiteto imepangiwa kiasi cha Sh38.7 bilioni, wilaya ya Mbulu Sh38.7 bilioni, Mbulu mji Sh29.3 bilioni na Simanjiro sh37.5 bilioni.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amesema kupitia serikali ya awamu ya sita mkoa huo umepiga hatua kwenye sekta mbalimbali.

Sendiga amesema maeneo tofauti ya mkoa wa Manyara yamepiga hatua katika sekta ya elimu, maji, afya na miundombinu mbalimbali.

“Tunaishukuru mno serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna ilivyofanikisha miradi mbalimbali kwenye mkoa wetu wa Manyara”, amesema Sendiga.

Mkazi wa mji wa Babati, John Ombay amesema pamoja na kupitishwa kwa mpango huo wa bajeti, jamii inaona maendeleo yanayofanyika.

Ombay amesema shule mpya zinajengwa Manyara, vituo vipya vya afya na zahanati kwenye vijiji hivyo kuonyesha kwa macho maendeleo yanavyopatikana.

“Pamoja na kuwa bado kuna changamoto mbalimbali kwa jamii ila maendeleo tunaona ikiwemo suala la usambazaji maji hasa vijijini hivyo hatuna budi kuipongeza serikali kwa kutimiza vyema wajibu wake,” amesema Ombay.

Mkoa wa Manyara ulioanzishwa mwaka 2002 una ukubwa wa kilomita za mraba 44,522 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022 una watu 1,893,000 katika wilaya tano zenye vijiji 440.

 

Related Posts