Unguja. Mwakilishi wa Pandani, Profesa Omar Fakih Hamad amesema licha ya kauli za Serikali za kukusudia kukifungua kisiwa cha Pemba kupitia bandari inayoweza kutoa huduma za kimataifa, uhalisia wa jambo hilo bado haujaonekana.
Profesa Hamad amesema hayo wakati akiuliza swali leo Alhamisi Februari 27, 2025 katika mkutano wa 18 wa Baraza la Wawakiliahi.
“Ni kwa nini hadi kufikia sasa bandari za Pemba hazijaweza kufanya kazi kama ilivyoazimiwa na lini Serikali itapeleka kreni kwa ajili ya kupakua makasha moja kwa moja kwenda kwenye magari,” amehoji.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Nadir Abdullatif Yussuf amesema Serikali inaendelea na uwekaji wa mazingira mazuri kupitia sekta mbalimbali kwa upande wa Pemba ili kutoa huduma za kimataifa ikiwemo barabara, bandari, viwanja vya ndege, sekta ya afya na umeme.
“Hivyo, kauli za Serikali kukusudia kuifungua Pemba kupitia bandari zinaendelea kufanyiwa kazi ambapo kwa sasa masuala ya majengo, miundombinu na huduma zinaendelea kufanyiwa kazi kwa upande wa Kaskazini na Kusini Pemba,” amesema.
Amesema, bandari ya mkoani inaendelea na ujenzi wa jengo la abiria na ofisi na yatakamilika ndani ya miezi tisa kwa gharama za dola 5 milioni za Marekani, sawa na Sh12 billioni, chini ya kampuni binafsi ya Fumba Port.
Pia, amesema Bandari ya Shumba inaendelea na ujenzi wa awamu ya pili ya ujenzi wa jengo la abiria, ukuta pamoja na msikiti ambapo bandari hii itasaidia hadi safari za Mombasa, Kenya ukizingatia Micheweni ni eneo la uwekezaji.
“Bandari zinaendelea kufanya kazi ikiwemo ya Mkoani ya kushusha makontena inayoendeshwa na kampuni ya Fumba Port, na hadi sasa imeshashusha makontena 172 kwa meli sita zilizotia nanga bandarini hapo,” amesema Nadir.
Vilevile, amesema bandari hiyo inaendelea kutoa huduma na inategemewa kujengwa tena kupitia fedha za washirika wa maendeleo kutoka Serikali ya Jamhuri ya Korea (KOICA).
Sambamba na hilo, amesema kreni ya tani 90 ipo ila kwa sasa inatumika katika miradi ya maendeleo ya Serikali, ambayo awali ilisaidia kukamilisha ujenzi wa gati ya Shumba na inasaidia kukamilisha ujenzi wa uwanja wa Gombani.
Hata hivyo, kreni kubwa zitawekwa baada ya utanuzi wa gati, ambao umepangwa kufanyika ndani ya miaka miwili kwa mujibu wa mkataba wa uendeshaji baina ya Serikali na kampuni ya Fumba Port.