DPP amfutia kesi Dk Slaa, aachiwa huru

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemfutia kesi mwanasiasa Mkongwe nchini, Dk Wilibrod Slaa (76) baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuieleza Mahakama kuwa hana nia ya kuendelea na shauri hilo dhidi ya mshtakiwa huyo.

Mshtakiwa huyo alikuwa anakabiliwa na shitaka moja la kusambaza taarifa za uongo katika Mtandao wa X kinyume cha sheria, tukio analodaiwa kulitenda Januari 9, 2025 katika Jiji la Dar es Salaam.

Uamuzi huo umetolewa leo Alhamisi Februari 27, 2025 na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga, baada ya upande wa mashitaka kuwasilisha maombi hayo.

Mshtakiwa huyo amefutiwa shitaka lake chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), sura ya 20, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Kabla ya kufutiwa shitaka hilo, mawakili wawili Waandamizi wa Serikali, Job Mrema na Clemence Kato waliieleza Mahakama hiyo kuwa DPP hana nia ya kuendelea na shauri hilo, hivyo wanaomba kuiondoa kesi hiyo.

Endelea kufuatilia mitandao ya kijamii ya Mwananchi

Related Posts