Mpanga, Said Hamdani na Salum Nasir wameteuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kuchezesha mchezo wa kufuzu fainali za Kombe la Dunia baina ya Botswana na Algeria utakaochezwa Francistown, Botswana Machi 21, 2025.
Mara ya mwisho Arajiga kuchezesha mechi za kimataifa ilikuwa ni Januari 19, 2025 ambapo alichezesha mchezo wa Kundi B wa Kombe la Shirikisho Afrika kati ya RS Berkane ya Morocco na Stellenbosch ya Afrika Kusini. Pia amewahi kuchezesha mechi za Klabu Bingwa Afrika kati ya Red Arrows na TP Mazembe kwenye hatua za pili za Ligi ya Mabingwa, Septemba 14, mwaka jana.
Hii si mara ya kwanza kwa waamuzi wa Tanzania kuchezesha pamoja mechi ya kimataifa kwani Novemba 14, Arajiga akiwa kati na wenzake Frank Komba, Hamdani Said na Elly Sasii waliamua mchezo wa kufuzu AFCON kati ya Lesotho na Central African Republic.

Arajiga ambaye alikabidhiwa beji ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) mwanzoni mwa mwaka 2022 pamoja na kwamba kwenye ligi anaonekana kuwa mwamuzi bora, ameendelea kuwa bora kimataifa huku akizidi kupewa mechi mbalimbali za kimataifa.
Timu zote mbili tayari zimecheza michezo minne katika kundi G, ambapo Algeria ndiyo vinara wa kundi hilo wakiwa na pointi tisa sawa na Msumbiji huku Botswana ikishika nafasi ya tatu ikiwa na pointi sita sawa na Guinea na Uganda zinazoshika nafasi ya nne na tano, Somalia inaburuza mkia bila pointi.
Katika mchezo huo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Obert Itani Chilume, Francistown, Botswana itavaana na Algeria kwa mara ya kwanza katika mechi za kundi G huku ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza dhidi ya Waarabu hao, kwani mara ya mwisho walikutana kwenye makundi ya kufuzu fainali za AFCON 2025 ambapo Algeria ilishinda mechi zote mbili.