Nyota Outsiders azigonganisha nne | Mwanaspoti

BAADA ya Stein Warriors, JKT, Savio na ABC kuibuka na kuitaka saini ya nyota wa UDSM Outsiders, Tryone Edward, mwenyewe amefunguka anachoangalia ni masilahi tu, kwake kambi popote, huku nyota mwenzake Josephat Petar akimaliza mkataba wake.

Timu mbalimbali zitakazoshiriki Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), zinaendelea kujiweka sawa kwa kusajili nyota wapya, huku pia maandalizi ya ligi hiyo yakianza kupamba moto.

Hata hivyo, moja ya matakwa ya nyota huyo ni kutafutiwa ajira na klabu yoyote itakayotaka kumsajili kwani hatategemea tu kucheza ili kuendesha maisha.

“Unajua miaka inaenda na huwezi kutegemea kucheza kikapu tu ili ikuendeshe maisha, ukifanya hivyo unaweza ukafeli,” alisema Edward na kuongeza kama zitashindwa kutekeleza mahitaji yake ataendelea kuichezea UDSM Outsiders.

Edward anayecheza nafasi ya shooting guard (namba 2) ni fundi wa kufunga katika maeneo yote ya uwanja na aliwahi pia kuzichezea Ukonga Kings, ABC na Pazi.

Kwa upande wa Petar aliyeichezea Dar City katika ligi hiyo, mwaka jana, alisema amemaliza mkataba wake na sasa milango ipo wazi kwa timu yoyote itakayomhitaji.

“Kwa sasa ni mchezaji huru, naruhusiwa kuchezea timu yoyote itakayonihitaji,” alisema Petar anayecheza nafasi ya point  guard (namba 1) na mwenye uwezo mkubwa wa kuasisti na kufunga eneo la pointi tatu.

Related Posts