Mwanasiasa Mkongwe Tanzania, Dk Wilibrod Slaa (76) amesema anapigania kuondoka sheria zote mbovu, na ni kati ya watu wanaosimama ‘No reforms no elections’ na msimamo wake unajulikana.
Dk Slaa amezungumza hayo leo Alhamisi Februari 27, 2025 baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa hana nia ya kuendelea na shauri hilo dhidi yake.
Dk Slaa alikuwa anakabiliwa na shitaka moja la kusambaza taarifa za uongo kupitia mtando wa Kijamii wa X, tukio analodaiwa kulitenda Januari 9, 2025 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Uamuzi huo umetolewa leo Alhamisi Februari 27, 2025 na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga, baada ya upande wa mashitaka kuwasilisha maombi hayo.
Mshtakiwa huyo amefutiwa shitaka lake chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), sura ya 20, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Kabla ya kufutiwa shitaka hilo, mawakili wawili Waandamizi wa Serikali, Job Mrema na Clemence Kato waliieleza Mahakama hiyo kuwa DPP hana nia ya kuendelea na shauri hilo, hivyo wanaomba kuiondoa kesi hiyo.
Endelea kufuatilia mitandao ya kijamii ya Mwananchi