Mbeya. Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza ndugu, jamaa na marafiki pamoja na majeruhi katika ajali iliyotokea mkoani Mbeya.
Ajali hiyo ilitokea juzi Februari 25 katika eneo la Shamwengo wilayani Mbeya ikihusisha gari la Serikali na basi la Kampuni ya CRN wakati wa hitimisho ya ziara ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi (CCM) Taifa, Fadhil Rajabu.
Katika ajali hiyo watu watatu walifariki dunia papo hapo wakiwa ni mwandishi wa habari, Furaha Simchimba, mjumbe wa kamati ya utekelezaji CCM Wilaya ya Rungwe, Daniel Mselewa na Utingo wa basi la CRN, Isaya Geazi kabla ya kifo kingine kuongezeka cha aliyekuwa dereva wa Mkoa wa Mbeya, Thadei Focus wakati akipatiwa matibabu.

Miongoni mwa majeruhi kwenye ajali hiyo ni waandishi Epimarcus Apolnali (Chanel Ten), Seleman Ndelage (Dream FM) na Denis George ambaye ni mwandishi wa kujitegemea wanaoendelea kupatiwa matibabu hospitali.
Akizungumza leo Alhamisi, Februari 27, 2025 wakati wa kuaga miili ya marehemu hao, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Patrick Mwalunenge amesema Rais Samia amepokea kwa mshtuko na simanzi kubwa vifo vya marehemu na majeruhi.
Amesema kutokana na kuguswa kwa misiba hiyo, amewasilisha rambirambi ya Sh5 milioni kwa kila familia iliyompoteza ndugu yao na Sh1 milioni kwa majeruhi wa ajali hiyo.
“Lakini pia CCM itaendelea kusimamia na kugharamia matibabu yote ya majeruhi katika ajali hiyo na iwapo watahamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili tutasimamia hizi ndizo salamu za Mwenyekiti wetu Taifa,” amesema Mwalunenge.

Mwalunenge ametumia nafasi hiyo kueleza namna alivyonusurika katika ajali hiyo, akieleza alikuwa sehemu ya gari hilo ambapo aliomba kuachwa huko Makambako ili afuatwe baadaye kwa ajili ya safari yake ya jijini Arusha kushiriki mazishi ya mama mzazi wa Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya, Langael Akyoo.
“Dereva aliniuliza sasa itakuwaje mwenyekiti tukuache hapa na ilhali wewe ndio kiongozi, nikamwambia nyie nendeni ila kuweni makini kwa kuwa hii njia ya Igawa Mbeya huwa si nzuri sana.
“Akaniambia nichukue basi chaja yangu ya simu, nikamwambia hapana iache humo nyie mtanikuta hapa Makambako ili tuongozane na wengine kwenda Arusha lakini baadaye ndio nikapata taarifa za ajali hii,” amesema Mwalunenge.
Akizungumza kwa niaba ya vyama vya upinzani, Mbunge wa viti maalumu Wilaya ya Rungwe (Chadema), Sofia Mwakagenda amesema ni masikitiko kupoteza nguvu kazi ya Taifa kutokana na marehemu wote kuwa na umri mdogo.
“Huu siyo msiba wa CCM wala familia moja, bali ni pigo kwa jamii na Taifa kwa ujumla kwa kuwa wote hawa walikuwa katika kuitumikia nchi, kwa mwaka mmoja naomba kulipia ada ya mtoto wa aliyekuwa mjumbe wa kamati ya utekelezaji CCM Rungwe,” amesema Mwakagenda.
Naye Mwenyekiti wa Wabunge Mkoa wa Mbeya, Olen Njeza amesema ni masikitiko makubwa kupoteza watumishi hao ambao walikuwa na mchango mkubwa katika Taifa.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa amelitaka Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani kuwa wakali sana kudhibiti mwendo kasi ili kuokoa maisha ya wananchi.
“Nitoe rai kwa askari wetu kikosi cha usalama barabarani kuongeza ukali katika kudhibiti mwendo kasi kwa madereva ili kuondokana na ajali kama hizi zinazojitokeza, kwa ujumla tumepokea kwa masikitiko makubwa vifo na majeruhi hawa,” amesema Malisa.
Walichokisema Rajabu, Mongella
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Fadhil Rajabu amesema alikuwa na ziara ya kukagua miradi inayotekelezwa mkoani Mbeya, lakini wakati wanamsindikiza alishtushwa na taarifa za ajali iliyosababisha vifo na majeruhi hao.

Naibu Katibu Mkuu CCM Bara , John Mongela (kushoto) akisalimina na baadhi ya wajane waliofiwa na waume zao katika ajali iliyotokea mkoani Mbeya wakati wa ziara ya CCM Taifa mkoani humo.
“Nitoe pole sana kwa familia zote zilizoguswa, lakini tuwe na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu, Serikali na chama kwa ujumla tutaendelea kuwa pamoja” amesema Rajabu.
Naibu Katibu Mkuu (CCM) Bara, John Mongella amesema pamoja na simanzi hiyo lakini wananchi waendelee kumuamini Mungu, akieleza kuwa kila mwanadamu safari ni moja na kwamba CCM imeguswa sana na ajali hiyo.
Amesema Rais Samia alitoa maelekezo kwa Katibu Mkuu, Dk Emmanuel Nchimbi ambaye naye alimuelekeza Mongella kufika Mbeya kwa ajili ya kushiriki kuaga miili hiyo akieleza kuwa hakuna namna nyingine zaidi ya kutoa pole.
“Rais Samia ametoa maelekezo pia huduma kwa majeruhi zitolewe, lakini kutokana na michango mingi iliyopo iratibiwe vizuri iwafikie walengwa, hili linatuhusu wote hivyo tuweke tofauti zetu pembeni.”
“Sisi wote tuko njiani na mfariji mkubwa ni Mungu, tunaahidi kwamba CCM itafanya lolote liwezekanalo kuhakikisha majeruhi wote wanapata huduma ili warejee kwenye afya zao na niwatoe hofu katika hili,” amesema Mongella ambaye ni mlezi wa chama wa mkoa huo.
Hata hivyo, kabla ya taratibu za kuagwa kwa miili hiyo, waandishi wa habari mkoani Mbeya waligoma kushiriki wakishinikiza kupata hatima ya wenzao ambao ni majeruhi wakidai kupata taarifa za kutopewa huduma.
Hali hiyo iliibua taharuki, ambapo Katibu wa Siasa na Uenezi Mkoa huo, Christopher Uhagile alitoa ufafanuzi kuwa CCM imeratibu na kusimamia huduma zinatolewa kwa majeruhi hao, bure lakini msimamo wa waandishi ulibaki vilevile.
Baadaye Spika wa Bunge na Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson aliingilia kati na kutoa msimamo wa chama hicho akitoa hofu kwa waandishi hao akieleza iwapo kuna changamoto yoyote CCM utaifanyia kazi. Ndipo shughuli za kuaga ziliendelea.