Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemfutia kesi ya jinai na kumwachia huru Mwanasiasa mkongwe, Dk Willibrod Slaa (76), baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) kuieleza Mahakama hiyo hana nia ya kuendelea na mashitaka dhidi yake.
Kwa sasa Dk Slaa atakuwa uraiani kuendelea na mishemishe zake za maisha, baada ya kukaa gerezani kwa siku 48.
Dk Slaa alikuwa anakabiliwa na kesi ya jinai namba 993 ya mwaka 2025 yenye shitaka moja la kusambaza taarifa za uongo katika mtandao ya kijamii wa X.
Hadi anafutiwa kesi yake na kuachiwa huru, Slaa amekaa gerezani siku 48 kutokana na upande wa mashitaka kuzuia dhamana yake na hali iliyosababisha aendee kusota rumande.
Kesi hiyo ilipagwa kutajwa Machi 4, 2025 lakini leo Alhamisi Februari 27, 2025 mshtakiwa huyo aliletwa mahakamani hapo kwa hati ya dharura kutoka gerezani.
Mshtakiwa huyo amefutiwa mashitaka yake chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), sura ya 20, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.

Kwa mara ya kwanza, mshtakiwa huyo alifikishwa Mahakama ya Kisutu, Januari 10, 2025 na kusomewa shitaka lake.
Uamuzi huo wa kumfutia shitaka hilo umetolewa leo Alhamisi Februari 27, 2025 na Hakimu Mkazi Mfawidhi Franco Kiswaga , baada ya DPP kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashitaka dhidi ya mshtakiwa huyo.
Mawakili wa Serikali Waandamizi, Job Mrema na Clemence Kato, wameieleza Mahakama kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kutajwa, lakini DPP hana nia ya kuendelea na kesi hiyo.
Kabla ya wakili Mrema kuendelea na uwasilishaji wa maombi hayo, Hakimu Kiswaga ameieleza Mahakama kuwa kesi hiyo ilikuwa na pande mbili, kulikuwa kuna maombi ya kuzuia dhamana na kulikuwa na kesi ya msingi, hivyo alitaka upande wa mashitaka ueleze maombi yao yanajikita kwenye nini.
Akijibu maelezo hayo, Mrema ameomba Mahakama iweke kwenye kumbukumbu kuwa upande wa mashitaka waliwasilisha maombi ya mshtakiwa kutokupata dhamana.
“Lakini leo tunaiambia Mahakama kuwa upande wa mashitaka tunaomba kuondoa mapingamizi hayo,” amesema Mrema na kuongeza:
“Vilevile kwa niaba ya DPP, tunaomba kutoa taarifa kuwa hana nia ya kuendelea na shauri hili dhidi ya Dk Slaa, kwa kosa ambalo alishtakiwa nalo.”
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Kiswaga alimuuliza wakili wa utetezi Hekima Mwasipu, kuhusiana na maombi yaliyowasilisha na upande wa mashitaka, ambapo Mwasipu alijibu hana pingamizi juu ya maombi hayo kwa kuwa DPP ndio mwenye mamlaka ya kushtaki mtu na kufutia mashitaka.
Baada ya pande zote kuridhia, Hakimu Kiswaga amesema amekubaliana na hoja iliyotolewa na anaiondoa kesi hiyo chini ya kifungu hicho cha 91(1) cha CPA.
Akihojiwa na waandishi wa habari baada ya kuachiwa huru, Dk Slaa amesema yupo tayari kurudi Chadema amesema mwanzo alikuwa ni mwanaharakati lakini sasa yupo tayari kurudi kwenye chama hicho.
“Kile tulichokipigania wamekiweka wazi, kile kilichoniondoa mwaka 2015 kimeshafutika, sasa hivi sina tatizo lolote kufanya kazi karibu zaidi na Chadema kwa utaratibu wa Chadema,” amesema Dk Slaa.
Dk Slaa akiwa Katibu Mkuu wa Chadema mwaka 2015, alitangaza kujiweka kando.
Mikiki aliyopitia Dk Slaa
Januari 10, 2025 upande wa mashitaka uliwasilisha mahakamani hapo zuio la dhamana dhidi ya mshtakiwa huyo.
Wiki moja baadaye, mshtakiwa huyo kupitia mawakili wake, alifungua kesi Mahakama Kuu kuangalia uhalali wa hati ya mashitaka pamoja na mwenendo wa kesi hiyo.
Oktoba 30, 2025 Mahakama Kuu ilitoa uamuzi kuhusiana na kesi mbili zilizofunguliwa na Dk Slaa.

Mwanasiasa mkongwe nchini na Katibu Mkuu wa zamani wa Chadema, Dk Willbrod Slaa, akitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kuachiwa huru. Picha na Hadija Jumanne
Hata hivyo, Oktoba 31, 2025 Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) aliwasilisha kusudio la kukata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi uliotolewa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, ambao ulielekeza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kushughulikia suala la dhamana ya mwanasiasa huyo pamoja na mambo mengine.
Notisi hiyo ya kupinga uamuzi huo iliwasilishwa Mahakama ya Rufani na kusajiliwa katika mfumo Januari 30, 2025 na ilikuwa inasubiri kupangiwa Jaji kwa ajili ya usikilizwaji.
Kutokana na DPP kuwasilisha kusudio hilo la kukata rufaa, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilifungwa mikono kuendelea na kesi ya msingi, mahakamani hapo.
DPP aliwasilisha kusudio la kukata rufaa kutokana na uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa na jaji Anold. Kirekiano, Januari 30, 2025, ambao ulielekeza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kushughulikia suala la dhamana ya mwanasiasa huyo, na kutoa uamuzi wa pingamizi la uhalali wa kesi ya jinai inayomkabili mahakamani hapo kwa haraka.
Mbali na maelekezo hayo kwa Mahakama ya Kisutu, pia kupitia sakata la dhamana ya mwanasiasa huyo, Mahakama Kuu ilitoa maelekezo maalumu kwa Mahakama zote za chini namna ya kushughulikia suala dhamana za washtakiwa wa kesi za jinai.
Katika maelekezo hayo, Mahakama Kuu ilizitaka mahakama hizo za chini yake kuweka kipaumbele cha kwanza kabisa kushughulikia dhamana kuliko masuala yoyote yanayohusiana na kesi hizo, huku ikisisitiza kuwa suala la dhamana linapaswa lishughulikiwe siku ya kwanza kabisa mshtakiwa anaposomewa mashitaka.
Dk Slaa alifungua mashauri mawili Mahakama Kuu kutokana na mwenendo wa kesi ya jinai inayomkabili katika Mahakama ya Kisutu.
Katika mashauri hayo, mbunge huyo mstaafu wa jimbo la Karatu alikuwa akiiomba mahakama hiyo iitishe na kupitia mwenendo wa shauri dogo lililofunguliwa na Jamhuri kupinga dhamana yake na wa kesi ya msingi, kujiridhisha na usahihi na uhalali wake.
Dk Slaa ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na mgombea urais kupitia chama hicho katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, alifungua mashauri hayo kutokana na mwenendo wa kesi ya jinai inayomkabili katika Mahakama ya Kisutu.
Hata hivyo, mashauri yote mawili yalisikilizwa na kutolewa uamuzi na Jaji Kirekiano.
Dk Slaa anakabiliwa na kesi ya jinai namba 993 ya mwaka 2025 yenye shitaka moja la kusambaza taarifa za uongo katika mtandao ya kijamii wa X.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo chini ya kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015.
Mwanasiasa huyo mkongwe anadaiwa kutenda kosa hilo, Januari 9, 2025 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Inadaiwa siku hiyo ya tukio, mshtakiwa kupitia jukwaa la mtandao wa kijamii wa X katika akaunti ya Maria Sarungi @MariaSTsehai aliandika ujumbe uliosomeka kama ifuatavyo.
“Wakubwa wametafutana, nikisema wakubwa namaanisha Mwamba na Samia, na wala hatuna maneno ya kumung’unya,….na kimsingi wamekubaliana Suluhu Samia amekubali atatoa pesa, Suluhu Samia amekubali ataongeza nguvu ya pesa ni dhahili atatoa pesa…hizo ni hela za Watanzania wanazichezea Samia na watu wake.”
Pia, aliandika maneno yalisomeka kama “Samia toka muda mrefu haangaikii tena maendeleo ya nchi anahangaikia namna ya kurudi Ikulu, na namna yake ya kurudi Ikulu ni kwa njia hizo kumsaidia mtu kama Mbowe,” wakati akijua taarifa hizo ni za uongo.