TIMU ya Taifa ‘Twiga Stars’ imevuka raundi ya pili ya michuano ya fainali za Mataifa ya Afrika kwa wanawake (WAFCON) mwakani, nchini Morocco baada ya sare ya 1-1 dhidia ya Guinea ya Ikweta.
Mchezo wa kwanza Stars ilishinda mabao 3-1 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi kwa mabao ya Stumai Abdallah, Enekia Lunyamila na Diana Msewa yaliyoiweka hai Stars kuvuka raundi inayofuata.
Tanzania ikicheza ugenini ililazimisha sare ya 1-1 kwa wenyeji Guinea ya Ikweta na kuvuka kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-2, wakati Ethiopia ikisonga mbele baada ya kushinda kwa mikwaju ya penati 5-4 kupenya raundi ya pili mbele ya Uganda baada ya matokeo ya jumla kuwa mabao 2-2 kila timu ikishinda nyumbani.
Katika mchezo wa Twiga, timu hiyo iliyoshinda nyumbani jijini Dar es Salaam, ilisubiri kipindi cha pili kupata bao la Enekia Kasongo kuwakata maini wenyeji waliotangulia hadi mapumziko kwa bao 1-0.

Kwa upande wa Ethiopia ilipata ushindi wa 2-0 nyumbani kulipa kisasi cha Uganda ilichopewa wiki iliyopita na kufanya matokeo kuwa 2-2 na hivyo kulazimika kupigiana penalti na wenyeji kushinda 5-4.
Haya hapa mambo matatu yaliyoifanya Stars kuvuka raundi ya pili.
Ubora wa kikosi cha Stars ulichangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha ushindi wa timu hiyo inasakata rekodi nyingine ya kufuzu WAFCON.
Uwepo wa nyota mbalimbali wanaocheza soka la kulipwa na wale wa ligi kuu umechangia kwa kiasi kikubwa ushindi huo.
Nyota kama Clara Luvanga (Al Nasssr), Enekia Lunyamila (Mazaltan), Opah Clement na Julietha Singano (FC Juarez, Mexico), Diana Msewa (Trabzorpor, Uturuki), Stumai Abdallah, Donisia Minja , Naijat Abbas wa JKT Queens na Aisha Mnunka wa Simba Queens walikuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi hicho.
Ukiangalia wachezaji walioitwa kwenye kikosi hicho karibu wote wamekuwa tegemeo kwenye timu wanazochezea wakionyesha viwango hadi kwenye timu ya taifa.
Clara anayekipiga Saudi Arabia ndiye kinara wa ufungaji akiwa na mabao 12 akiwaacha waarabu kwenye mbio hizo, Stumai hadi sasa anaongoza kwa mabao ligi kuu akiwa na mabao 18, Naijat anaongoza kwa cleansheet ligi kuu akiwa nazo nane.
Sio jambo la kushanganza kuona nyota hao wakipambania vyema bendera ya Tanzania, bali ni jambo la kuwapongeza kwani wamekuwa na viwango bora kulingana na wale wa kigeni.
Wapo pia wale wachanga ambao Kocha Bakari Shime aliwachanganya kwenye kikosi hicho ili kuwapatia uzoefu wa kimataifa.
Hata hivyo, sio tu kuwaita bali nyota wawili wachanga, kiungo Elizabeth John na beki wa kulia Lidya Kabambo wa JKT Queens walianza kwenye kikosi hicho.
Kiwango bora walichoonyesha kwenye mechi zote mbili ni wazi Kocha Shime anaanza kuwaandaa vijana wapya watakaokuja kusaidia timu hiyo.
Michezo yote miwili Stars ilianza kwa kupambana kuanzia dakika za mwanzo hadi dakika 180 zinamalizika ikiondoka na ushindi.
Mchezo wa kwanza ambao Stars ilikuwa nyumbani hadi kipindi cha kwanza ilikuwa nyuma kwa bao 1-0 na iliporudi kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, nyota hao walibadili matokeo na kuipa ushindi timu hiyo.
Haikuishia hapo tu hata ilipokuwa ugenini mapumziko Stars ilikuwa nyuma kwa bao 1-0 na ilirejea kipindi cha pili na nguvu na bao la Enekia Lunyamila lilifanya mzani uwe sawa na kumalizika kwa sare ya 1-1.
Kutokana na ishu hiyo ya njaa ya mafanikio, inatoa taswira ya upambanaji kwa wachezaji wa Stars ambao wanatafuta rekodi nyingine ya kufuzu kila wanapovaa uzi wa timu hiyo.
Ndani ya kikosi hicho, safu ya ulinzi ya Stars inaongoza kuwa na ukuta mgumu na hata safu ya ushambuliaji ikiwa bora kutokana na viwango vya nyota hao wanaojua kutupia nyavuni.
Hadi sasa Enekia Lunyamila ndiye anayeongoza kwa upachikaji mabao kwa Stars akiwa nayo mawili, Stumai na Diana kila mmoja akiwa nalo moja.
Rasmi sasa Stars itakutana na Ethiopia kwenye mchezo wa raundi ya pili ambao wakishinda hapo wanafuzu moja kwa moja kucheza fainali hizo.
Kwa ukanda wa Afrika Mashariki Ethiopia ni miongoni mwa timu zenye ushindani mkubwa na kwa ubora haijapishana na Tanzania.
Tanzania inakutana na Ethiopia ambayo inaonekana kuwa bora hasa kwenye safu yake ya ushambuliaji ikiongozwa na straika, Loza Abera anayekipiga DC Power FC ya nchini Marekani.
Stars ikichanga karata zake vizuri kuanzia nyumbani Azam Complex Chamazi itakuwa rahisi kumaliza kazi ya kufuzu ikiwa ugenini ingawa Ethiopia ina rekodi nzuri za nyumbani.
Sio mpinzani mgeni kwa Tanzania kwani timu hizo zimeshakutana mara saba kwenye mashindano mbalimbali yake ya Stars na timu za vijana U-18.
Katika mechi sita za awali za timu hizo za michuano ya CAF ikiwamo ya CHAN na WAFCON, Tanzania imeshinda mara moja tu, wakati Wahabeshi wameshinda mara tatu na mechi nyingine mbili zikisha kwa sare tofauti.

Mara ya mwisho timu hizo zilikutana kwenye mechi za kuwania kufuzu CHAN zilizopigwa mwaka 2022 na mchezo wa kwanza ikiwa nyumbani Twiga ililazimishwa sare ya mabao 2-2 kisha kwenda kulala ugenini kwa mabao 2-1 na kung’olewa.
Hivyo mechi ya kwanza ya Oktoba 20 nyumbani, Twiga italazimika kushinda kwa idadi kubwa ya mabao kabla ya kwenda kurudiana na wapinzani wao wiki moja baadae, ili itinge raundi inayofuata ili kusaka tiketi ya fainali hizo za Wafcon 2026 zitakazopigwa Morocco.
Tanzania inaungana na Kenya ambao ilifuzu kwa kuichapa Tunisia bao 1-0 ugenini baada ya suluhu na itakutana na Gambia kwenye mchezo wa raundi ya pili.
Nyingine ni Angola watakaokutana na Malawi, Botswana vs South Afrika, Namibia vs Zambia, Burundi vs Burkina Faso, Algeria vs Cameroon, Egypt vs Ghana, Benin vs Nigeria, Guinea vs Mali na Senegal vs Ivory Coast.
Mechi zote za raundi ya pili zitapigwa kuanzia Oktoba 20 hadi 28 mwaka huu.