Dar es Salaam. Siku nne baada ya kukamatwa kwa viongozi wa Umoja cha Walimu Wasiokuwa na ajira Tanzania (Neto) kwa kile kilichoelezwa umoja huo haujasajiliwa, wadau wameitaka Serikali kutafuta suluhisho la kukabiliana na ukosefu wa ajira badala ya kushughulika na watu wanaopaza sauti kuhusu changamoto hiyo.
Sintofahamu hii ilianza Februari 21, walipoibuka viongozi wa umoja huo ambao ni mwenyekiti wake Joseph Kaheza na katibu Daniel Edgar katika mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, wakitaka mambo kadha ikiwemo kusitishwa kwa usahili wa kada ya ualimu, utaratibu ambao Serikali imeanzisha hivi karibuni.
Hata hivyo, Februari 24 viongozi hao walikamatwa na Jeshi la Polisi kwa kile kilichoelezwa kuwa umoja huo haujasajiliwa.
Wakati hatima ya sakata hilo ikiwa haijajulikana, leo Alhamisi Februari 27, 2025 kwenye mitandao ya kijamii, limesambaa tangazo ka kuitisha mkutano wa waandishi wa habari na Umoja wa Vijana wasio na ajira (UYAM) Machi 2, 2025.
Tangazo hilo limekoleza mjadala wa suala la ajira na kuwaibua wadau wakisema Serikali inapaswa kutafuta suluhisho la changamoto ya ajira kabla bomu hilo halijawa na madhara makubwa.
Mjadala wa ukosefu wa ajira umekuwepo nchini muda mrefu na uliwahi kuwekewa uzito mara kwa mara na hayati Edward Lowasa, waziri mkuu wa zamani, kuwa lazima Serikali ihakikishe inatengeneza ajira kwa kuwa kila mwaka zaidi ya vijana 30,000 wanahitimu katika vyuo mbalimbali nchini bila ajira.
Alisema kuongezeka kwa vijana wanaopora watu katika maeneo mbalimbali ni ishara ya ukosefu wa ajira.
Akizungumzia tatizo hilo, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Karagwe, Benson Bagonza amesema kiini cha tatizo la ajira ni mfumo wa elimu unaowandaa watu kuajiriwa badala ya kujiajiri, hivyo hakuna sababu ya kuwabeza watu wanaolalamikia kukosa ajira.
“Hili ni bomu linalosubiriwa kulipuka na dalili za kulipuka kwake tayari zimeshaanza kuonekana kwenye sekta ya ualimu,” amesema.
Amesema tunakokwenda hata watengeneza majeneza wanaweza kuunda umoja na ukailetea nchi taabu.
“Sasa kuna vyama vitatu vya walimu natamani hili linaweza kutufanya kama Taifa tukae kuzungumzia changamoto ya ajira,” amesema.
Kutokana na hilo, Askofu Bagonza ameonya kama Serikali haitaweka mazingira mazuri kwa sekta binafsi ili iweze kutengeneza ajira, changamoto hiyo itaendelea kusumbua Taifa.
“Katika nchi yetu sekta binafsi imegeuzwa kuwa mshindani wa Serikali badala ya kuwa mdau. Tunahitaji kukaa meza moja kuzungumza juu ya jambo hili, kwa mfano Serikali iweke mazingira mazuri kwa wawekezaji wa ndani, iwasaidie wote wanaotoa ajira na si kuwawekea vikwazo.
“Sekta binafsi ikiwezeshwa na kupewa mazingira mazuri ya kuajiri itapunguza tatizo hili, ila linaweza kuendelea kama mtazamo wa watendaji na Serikali kwa ujumla hautabadilika. Naamini mawazo yapo yanayoweza kupunguza angalau nusu ya ukubwa wa tatizo,” amesema.
Si Askofu Bagonza pekee aliyezungumzia hilo, naye mdau wa elimu, Ochola Wayoga amesema hatua ya vijana wasio na ajira kujikusanya na kutengeneza umoja ni kengele kwa Serikali kuona ukubwa wa tatizo na kutafuta njia ya kuwawezesha kupitia vikundi hivyo.
“Nafikiri hiki kilichofanyika ilikuwa sababu tosha kwa Serikali kuwawekea vijana sera, zinazowaruhusu kukopa na kujishughulisha na mambo mengine, tofauti na kusubiri kuajiriwa.
“Wawekewe mifumo itakayowawezesha kuanzisha vitu vingine ambavyo wanaweza kuvifanya kwa mitaji au mikopo nafuu, kuwakamata si suluhisho,” amesema.
Kuhusu kukamatwa kwa viongozi wa Neto, Askofu Bagonza amesema ni kosa akisisitiza kuwa walipaswa kusikilizwa na badala ya kuwakamata kwa kuwa wameonyesha fukuto linaloendelea chini kwa chini.
“Hii kamatakamata sio sawa, hawa vijana wanahitaji kusikilizwa, wakikosa mtu wa kuwasilikiza shetani atawasikiliza na akiwasikiliza hatutapata mahali pazuri pa kukaa.
“Kinachoonekana, tuna walimu wengi wasioajiriwa kuliko walioajiriwa na hii si sawa. Nashindwa kuelewa mtu analalamika hana ajira unamkamata na kumweka ndani, sasa ukifanya hivyo ndiyo unakuwa umempa kazi?
“Shida zinaunganisha watu kuliko raha, sasa tuna chama cha walimu wasio na ajira, hii itakwenda kila sekta kama tatizo la ajira halitatatuliwa, natamani hili lituamshe ili tuanze kuzungumzumka kuhusu changamoto hii.
Tunatakiwa kujenga Taifa linalokubali maoni tofauti, si kwamba anayetoa maoni tofauti aonekane tatizo, tukubali tuna watu wenye karama ya kutoa maoni tofauti ya kulikwamua Taifa letu, unyampara hausaidii,” ameonya Askofu Bagonza.
Kwa mujibu wa tovuti ya Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) hadi kufikia Oktoba 2024, Tanzania ilikuwa na jumla ya walimu 274,541 kati ya hao, 180,325 ni wa shule za msingi na 94,216 wa shule za sekondari.
Mwishoni mwa mwaka jana katika awamu tofauti, Serikali ilitangaza ajira mpya za ualimu na hivi karibuni umefanyika usahili kuwapata waliokidhi vigezo vya kuajiriwa, hivyo idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka.
Akitoa maoni kupitia mtandao wa X, Jovith Modest amesema “Kama Serikali inawaacha kuwaajiri kwa sababu hawana vigezo hapo kosa ni la nani. Tuanze kujiuliza inakuwaje vyuo vinazalisha wasomi wasiokuwa na uwezo? Kama ni mjinga inakuwaje anahitimu na vyeti anapewa, basi waajiriwe hivyo hivyo maana ndiyo elimu waliyopewa,” amesema.
Naye @Mnarijunior ameandika; “Namna Serikali inavyokabiliana na hili suala kuna makosa inatakiwa kuyaepuka. Huwezi kutumia polisi au vyombo vya ulinzi na usalama kudhibiti madai ya namna hii kwa sababu inaweza kuchochea hasira na kuamsha makundi mengi zaidi.”
Ripoti ya APRM iligusia hili
Ripoti ya mwisho ya Mpango wa hiari wa nchi za Afrika kujitathmini (APRM) iliyotolewa mwaka 2013 ililitaja suala la ukosefu wa ajira miongoni mwa changamoto zinazotakiwa kutafutiwa ufumbuzi lakini hadi sasa utekelezaji wa pendekezo hilo haujafanyika kwa ufanisi, hali inayosababisha kuongezeka kwa kundi la vijana wasio na ajira.
Julai 11, 2024 wakati wa mkutano wa awali kabla ya kufanyika kwa tathmini nyingine ya APRM, Mkurugenzi wa Kituo cha Taarifa kwa Wananchi (TCIB), Deus Kibamba aliliambia gazeti hili kuwa Tanzania ina cha kujifunza kwa kilichotokea katika nchi nyingine za Afrika, ikiwa ni matokeo ya vijana kukosa ajira.
Alisema nchi inapokuwa na vijana wengi wasio na ajira ni rahisi kushawishika kufanya mambo yasiyofaa, akitolea mfano maandamano yaliyofanywa na vijana wa Gen Z nchini Kenya na yanayofanana na hayo katika nchi nyingine za Afrika.
“Ripoti ya APRM 2013 ilisema suala la ajira hasa kwa vijana ni bomu ambalo lisipotafutiwa ufumbuzi linaweza kutuharibia utulivu na amani ambayo tumekuwa nayo kwa miaka mingi. Sasa tunapoelekea kwenye maandalizi ya kufanya tathmini ya pili ni muhimu suala hili likapewa kipaumbele.
“Tujiulize tumefikia wapi katika kutatua changamoto hii ambayo inazidi kuwa kubwa siku hadi siku. Kila mwaka kundi kubwa la vijana linamaliza vyuo vikuu, hapo bado kuna wale wanaoishia ngazi za chini za elimu na wengine hawana elimu kabisa, hawa wote wanakwenda wapi na hakuna ajira?” amehoji Kibamba.
Amesema kama jitihada hazitafanyika kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo, upo uwezekano wa bomu hilo kulipuka kama ambavyo tayari imeshaonekana kwenye mataifa mengine ikiwemo jirani la Kenya.