Nyaya chini ya bahari kuimarisha matumizi ya kidigitali Zanzibar

Unguja, Zanzibar. Vodacom Tanzania PLC imetiliana saini makubaliano ya kimkakati na Shirika la Miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Zanzibar (ZICTIA), ili kuboresha huduma za mawasiliano na kuharakisha mabadiliko ya kidijitali visiwani Zanzibar. Mkataba huo, umesainiwa leo Alhamis 27, 2025 katika ofisi za Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, unairuhusu Vodacom kutumia miundombinu ya nyaya za chini ya bahari inayomilikiwa na serikali, hatua inayotarajiwa kuimarisha mawasiliano ya sauti na data katika visiwa hivyo.

Hafla ya utiaji saini imehudhuriwa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dk Khalid Salum Mohamed, Mkurugenzi Mkuu wa ZICTIA, Mhandisi Shukuru Awadh Suleiman na Mkurugenzi wa Mtandao wa Vodacom Tanzania, Andrew Lupembe, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dk Mohamed ameipongeza Vodacom Tanzania kwa juhudi zake za kupanua mtandao wa mawasiliano Zanzibar.

“Tunapongeza Vodacom kwa kuongeza idadi ya minara ya mawasiliano Zanzibar, hatua ambayo imeimarisha kwa kiasi kikubwa uwezo wa mtandao na huduma za intaneti. Tunatoa wito kwa wadau wengine kushirikiana nasi ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za mawasiliano kwa wananchi wote,” amesema.

Amesisitiza kuwa serikali imejidhatiti kusaidia waendeshaji wa mitandao ya simu kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa intaneti. “Tunashukuru ushirikiano wa Vodacom katika kutumia miundombinu ya ZICTIA, rasilimali ambayo serikali imewekeza ili kusaidia kufanikisha ajenda ya kitaifa ya Tehama kuhakikisha wananchi wanapata manufaa ya teknolojia ya kisasa,” amesema waziri huyo.

Ameongeza kuwa uwekezaji huo pia utahakikisha huduma za intaneti zinakuwa za haraka na za uhakika, ikiwamo ya serikali mtandao (e-government), elimu mtandao (e-learning), afya mtandao (e-health), na biashara mtandao (e-commerce).

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mtandao wa Vodacom Tanzania, Lupembe amesema dhamira ya kampuni hiyo ni kuboresha pia mawasiliano Zanzibar.

“Kama kinara wa teknolojia, tunaelewa kuwa mawasiliano ni msingi wa ukuaji wa uchumi na ubunifu. Kupitia ushirikiano huu na ZICTIA, tunahakikisha kuwa biashara, taasisi, na wananchi wa Zanzibar wanaweza kuwasiliana kwa urahisi, kupata huduma za kidijitali, na kufanya miamala bila usumbufu,” amesema.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa ZICTIA, Mhandisi Shukuru Awadh Suleiman, amesisitiza umuhimu wa waendeshaji wa mitandao, kutumia miundombinu ya kitaifa ili kuharakisha maendeleo ya Tehama.

“Mtandao wetu wa nyaya za chini ya bahari uliundwa kwa lengo la kuingiza Zanzibar katika zama ya kidijitali. Tuna furaha kuona Vodacom ikitumia rasilimali hii ili kuboresha huduma zake, hatua inayosaidia kufanikisha maono yetu ya jamii inayotegemea teknolojia kwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi,” amesema Suleiman.

Inaelezwa kuwa ushirikiano huo ni hatua muhimu katika mageuzi ya kidijitali Zanzibar, ukiimarisha nafasi ya visiwa hivyo kama kitovu cha mawasiliano na ubunifu.

Kwa kuunganishwa kwa miundombinu ya Vodacom na mfumo madhubuti wa Tehama wa ZICTIA, Zanzibar itanufaika na mfumo wa kisasa wa mawasiliano wa kasi ya juu.

Related Posts