Dar es Salaam. Ajali ya helikopta imeondoa uhai wa Mkuu wa Majeshi ya Kenya Jenerali Francis Ogolla leo Aprili 18, 2024.
Mbali na Jenerali Ogolla, ajali hiyo pia imepoteza maofisa tisa, huku wengine wawili wakijeruhiwa.
Wengine waliofariki katika ajali hiyo ni Brigedia Swaleh Said, Kanali Duncan Keitany, Luteni Kanali David Sawe, Meja George Benson Magondu aliyekuwa rubani, Kapteni Sorah Mohamed, Kapteni Hilary Litali, Sajini Mwandamizi John Kinywa Muredhi, Sajini Cliffonce Omondi na Sajini Rose Nyawira.
Ajali nyingine kama hiyo ilitokea Juni 10, 2012, baada ya helikopta ya Polisi ya Kenya Eurocopter AS350 kuanguka kwenye kilima, ikisababisha vifo vya watu sita waliokuwamo.
Miongoni mwa waliopoteza maisha alikuwapo aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani wa Kenya, George Saitoti, na Waziri Msaidizi, Joshua Orwa Ojode.
Katika ajali nyingine, maofisa wawili wa kijeshi walipoteza maisha wakati helikopta ilipopata ajali katika kaunti ya Machakos, Mashariki mwa Kenya Julai 13, 2020.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la China, (Xinhua) maofisa hao walifariki dunia baada ya helikopta waliyokuwamo kuanguka katika kaunti ya Machakos, Mashariki mwa Kenya, ofisa wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya (KDF) alisema.
Helikopta hiyo ya kijeshi aina ya MD-530F iliyotengenezwa nchini Marekani, ilianguka saa 11.00 jioni katika kijiji cha Kanyonga.
Ilikuwa katika safari ya mafunzo ikielekea Garissa kaskazini-Mashariki mwa Kenya kutoka Nairobi, alisema msemaji wa KDF, Zipporah Kioko.
Agosti 2012 helikopta mbili za Jeshi la Uganda zilizokuwa zikielekea nchini Somalia zilipotelea nchini Kenya karibu na mlima wa Kenya kwa mujibu wa tovuti ya CNN.
Helikopta hizo zilikuwa miongoni mwa nne za Uganda zilizotakiwa kushuka Garissa nchini Kenya kwa ajili ya kujaza mafuta kwa mujibu wa msemaji wa Jeshi la Uganda, Kanali Felix Kulayigye.
Moja ilitua salama, alisema na kwamba maofisa wa Jeshi la Anga la Kenya walimwambia maofisa wengine watano walitoka salama baada ya helikopta yao kutua salama karibu na Mlima Kenya.
Helikopta hizo zilikuwa zinaenda kutoa msaada katika mpango wa Umoja wa Afrika nchini Somalia, huko Mogadishu, ambapo vikosi vya Uganda, Burundi na nchi zingine za Umoja wa Afrika vilikuwa vikipambana na Al-Shabaab, kundi linalohusishwa na al-Qaeda.
Upatikanaji wa helikopta Kenya
Huenda matukio ya ajali yakawa mengi nchini Kenya kutokana na upatikanaji wa helikopta za kukodi, mbali na za kijeshi.
Kwa mujibu wa mitandao, helikopta nchini humo hukodishwa kwa kati ya Sh3.9 milioni hadi Sh5.86 milioni kwa saa kutoka kwa mashirika binafsi.