CDF wa Kenya afariki dunia katika ajali ya helkopta

Dar es Salaam. Rais wa Kenya, William Ruto amethibitisha kifo cha Mkuu wa Majeshi ya nchi hiyo (CDF), Jenerali Francis Ogolla aliyefariki dunia katika ajali ya helikopta iliyotokea leo Aprili 18, 2024 eneo la Algeyo katika Kaunti ya Marakwet.

Mbali na Jenerali Ogolla, ajali hiyo iliyotokea leo saa 8.20 mchana pia imesababisha vifo vya maofisa wanane, huku wengine wawili wakijeruhiwa.

Akizungumza leo usiku, kupitia vyombo vya habari nchini Kenya na taarifa kupatikana kwenye mitandao ya kijamii, Rais Ruto amesema Taifa hilo limepoteza watu muhimu.

“Jioni hii Taifa letu limepata msiba uliotokana na ajali ya anga iliyotokea katika eneo la Algeyo katika Kaunti ya Marakwet.

“Ninasikitika kutangaza kifo cha Jenerali Francis Omondi Ogolla, Mkuu wa Majeshi ya Kenya (KDF),” amesema Rais Ruto.

Amewataja waliofariki dunia pamoja na Jenerali Ogolla, kuwa ni Brigedia Swaleh Said, Kanali Duncan Keitany, Luteni Kanali David Sawe, Meja George Benson Magondu, aliyekuwa rubani, Kapteni Sorah Mohamed, Kapteni Hilary Litali, Sajini Mwandamizi John Kinywa Muredhi, Sajini Cliffonce Omondi na Sajini Rose Nyawira.

Akieleza jinsi ajali ilivyotokea, Rais Ruto amesema CDF Ogolla na msafara wake waliondoka Nairobi jana Aprili 17, 2024 na helikopta kwenda kutembelea vikosi vilivyopo kaskazini katika operesheni ‘Maliza Uhalifu’ na kukagua ukarabati wa shule unaoendelea.

“Ikiwa safari ya kikazi, aliarifiwa kuhusu hali ya usalama katika vikosi vilivyopo Kaunti ya Baringo na aliendelea katika Kambi ya Kainuti iliyopo Kaunti ya Turkana, ambako alihutubia vikosi akivitaka kuwa na uvumilivu na kufanikisha operesheni,” amesema Rais Ruto. 

Amesema msafara wa CDF Ogolla uliondoka Kainuki kwenda Chesegon katika Kaunti ya Pokot ya Magharibi ambako alizindua ukarabati wa shule ya wavulana ya sekondari ya Keptulel.

Amesema baada ya hapo aliondoka kuelekea Chesegon kwenye Shule ya Makuruta alikotarajiwa kukagua ujenzi katika taasisi hiyo.

Kwa mujibu wa Rais Ruto, kwa bahati mbaya helikopta ilianguka baada tu ya kuruka.

“Huu ni wakati wa huzuni kubwa, kipindi cha huzuni kwangu mimi kama Amiri Jeshi Mkuu, ni kipindi kigumu kwa Wakenya na majeshi ya Kenya na siku ya bahati mbaya kwa Taifa lote,” amesema.

“Nchi yetu imepoteza moja ya majenerali muhimu, na maofisa muhimu, watumishi wetu.”

Awali, taarifa zilizosambaa mitandaoni zilieleza Rais Ruto aliitisha kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Kitaifa (NSC) katika Ikulu ya Nairobi kujadili ajali hiyo.

Rais Samia Suluhu Hassan amesema: “Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Jamhuri ya Kenya, Jenerali Francis Omondi Ogolla na wanajeshi wengine tisa katika ajali ya helikopta iliyotokea leo katika Kaunti ya Elgeyo-Marakwet.”

“Natuma salamu za pole kwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya, Mheshimiwa William Ruto, wananchi wote wa Kenya, familia, ndugu, jamaa na marafiki wote waliopoteza jamaa zao katika ajali hiyo. Poleni sana,” amesema Rais Samia kupitia akauti zake za kijamii.

Katika utumishi wake, Jenerali Ogolla amekuwa CDF kwa kipindi cha mwaka mmoja pekee tangu alipoteuliwa na Rais Ruto Aprili, 2023.

Kabla ya kuteuliwa Ogolla alikuwa Makamu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi.

Ogolla aliteuliwa kujaza nafasi ya Jenerali Robert Kibochi aliyeondoka jeshini baada ya kufikisha miaka 62.

Jenerali Ogolla alijiunga na jeshi Aprili 24, 1984, akiwa Ofisa wa Kamandi ya Anga na kuanza kazi ya urubani wa ndege za kivita.

Kwa mujibu wa mtandao wa The Star wa Kenya, Jenerali Ogolla alikuwa mhitimu wa Chuo cha Kijeshi cha Paris, Ufaransa na Chuo cha Taifa cha Ulinzi cha Kenya.

Alihitimu Diploma ya Uhusiano wa Kimataifa na Sayansi ya Kijeshi kutoka Chuo Kikuu cha Egerton; Shahada ya Sanaa katika Sayansi ya Siasa, Migogoro ya Kivita na Mafunzo ya Amani; na Shahada ya Uzamili katika Uhusiano wa Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.

Alipanda ngazi hadi kuwa Meja Jenerali na akateuliwa kuwa Kamanda wa kamandi ya Anga ya Jeshi la Kenya Julai 15, 2018, wadhifa ambao alihudumu kwa miaka mitatu.

Pia amewahi kuwa Naibu Kamanda katika Kamandi hiyo, Kamanda wa Kambi ya Anga ya Laikipia.

Jenerali Ogolla alipenda kusoma vitabu na kucheza gofu. Ameacha mke, Aileenn Ogolla, watoto wawili na mjukuu.

Related Posts