Dk Nchimbi atoa agizo Wizara ya Kilimo

Mbeya. Wakati Serikali ya Tanzania ikiendelea kutafuta ufumbuzi wa changamoto ya ardhi ya kilimo wilayani Mbarali, Wizara ya Kilimo imeagizwa kufanya mazungumzo na mmoja wa wamiliki wa mashamba makubwa ili kuachia moja ya maeneo yake kwa ajili wakulima wa Mlonga na Mnazi.

Agizo hilo limetolewa leo Alhamisi, Aprili 18, 2024 na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi wakati akizungumza na wananchi wa Mbarali katika Kata ya Ubaruku wilayani humo.

Katika mkutano huo wa hadhara wananchi walitoa kero zao kwa Dk Nchimbi hasa masuala ya ardhi kwamba kuna maeneo yamepigwa marufuku kufanya shughuli za kilimo ili kuhifadhi mazingira.

Awali, wananchi hao walimuomba Dk Nchimbi kuingilia kati suala la migogoro ya ardhi na mipaka wilayani humo inayosababisha kutofanya shughuli zao kwa ufanisi hasa za kilimo cha mpunga, wakidai mazuio yaliyowekwa na Serikali yanawapa wakati mgumu na kuwatia umasikini.

“Mheshimiwa katibu mkuu tupo chini ya miguu yako tunaomba ututetea kwa Rais Samia Suluhu Hassan atusaidie angalau sehemu ya ardhi wanayoililia wananchi waweze kulima na kupata kipato,” amesema Margreth Mwakipesile.

Naye, Zaire Mwanda mkazi wa Kijiji cha Madundasi ameyesema changamoto kubwa ya Mbarali ni suala la ardhi katika maeneo ya vijiji ambavyo wananchi wamezuiliwa kufanya kilimo huku vingine vikihamishwa kwa sababu vipo ndani ya hifadhi.

“Tunaishi maisha ya shida kila maeneo Serikali wanayachukua kwa ajili ya hifadhi tunaomba utusaidia Dk Nchimbi,” amesema.

Hata hivyo, mwaka 2023 Rais Samia Suluhu Hassan alitoa ruhusa kwa wananchi kulima kwa muda katika maeneo yaliyozuiliwa, ujumbe uliofikishwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana katika mkutano wa hadhara uliofanyika Chimala.

Sasa kwa agizo hilo la Dk Nchimbi litawezesha wananchi wa Mlonga- Madibira na Mnazi waliokuwa hawana mahali pakufanyia kilimo kwa misimu kupata maeneo shughuli za kilimo cha mpunga ambalo ndio zao kuu la biashara wilayani Mbarali mkoani hapa.

Wananchi wa Mlonga- Madibira na Mnazi waliokuwa wakifanya shughuli zao kihalali ni miongoni wa waathirika wa Tangazo la Gazeti la Serikali la mwaka 2008 (GN28) lililowazuia wao na watu wa maeneo mengine kutofanya maendeleo ya kudumu.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, wananchi hao walitakiwa kupisha maeneo hayo ili maji yatiririke vema katika Mto Ruaha na Bonde la Ihefu ili kutunza mazingira.

Akizungumzia suala la wananchi kupatiwa maeneo ya kulima, Dk Nchimbi amemuagiza Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kuanza mazungumzo mara moja na mwekezaji huyo ikiwa ni sehemu ya suluhisho la awali la kukabiliana na changamoto hiyo.

“Hapa kuna mtu anamiliki mashamba makubwa, wakati nipo hapa nimetuma watu waende wakamuulize kama yupo tayari kuzungumza na Serikali na amekubali.

“Sasa kupitia mkutano huu namuelekeza Bashe aanze mazungumzo na mmiliki huyo ili kuachia shamba moja kwa ajili ya wananchi, mazungumzo yaanze haraka na Serikali izingatie haki zake na wananchi wapate eneo la kulima,” amesema.

Hatua hiyo ilipokewa kwa furaha na baadhi ya wananchi wa Mbarali waliosema itawezesha kupunguza changamoto ya maeneo ya kulima mpunga,akisema shida ya sio fedha bali eneo la kilimo.

“Kwa kuwa huyu mtu ana mashamba makubwa tukipata moja litawasaidia wananchi wa maeneo husika ambao kwa muda mrefu wamekosa maeneo ya kilimo baada ya Serikali kuwazuia kutokana na GN 28,” amesema Saimon Mwakasege.

Mwananchi Digital limemtafuta mbunge wa Mbarali, Bahati Ndingo aliyesema ni jambo jema litakowawezesha wananchi wa Mnazi na Mlonga- Madibira kulima kwa wamekuwa muda mrefu kutofanya shughuli hizo kutokana na agizo la Serikali. Jitihada za kumpata Bashe hazijazaa matunda kwani simu yake ya mkononi iliipa pasina kupokewa.

Related Posts