Kizungumkuti ununuzi magari ya ma-RC, DC

Dar es Salaam. Wakati Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Seriali za Mitaa (Tamisemi),  ikipanga kutumia Sh190.57 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa magari ya viongozi wa mikoa na wilaya, suala hilo limeibua hisia tofauti miongoni mwa wananchi, wengine wakiona ni mwendelezo wa matumizi mabaya ya fedha za umma.

Kwa upande mwingine, baadhi ya wakuu wa wilaya wameeleza adha wanazopata kwa kukosa magari.

Fedha hizo pia zitatumika kuendelea na ujenzi, ukarabati na ukamilishaji wa miundombinu ya mikoa, yakiwamo majengo ya utawala, Ikulu ndogo, makazi ya viongozi na watumishi wa mikoa, wilaya na tarafa katika mikoa 26.

Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais- Tamisemi kwa mwaka 2024/25 bungeni jijini Dodoma mwanzo wa wiki hii, Waziri wa wizara hiyo, Mohamed Mchengerwa alisema shughuli zitakazotekelezwa katika utawala bora ni pamoja na ununuzi wa magari tisa ya wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa katika mikoa ya Katavi, Njombe, Iringa, Kigoma, Mwanza, Singida, Dar es Salaam na Manyara.

“Ununuzi wa magari 56 ya wakuu wa wilaya na 47 ya wakurugenzi wa halmashauri,” alisema.

Ma-DC wasimulia adha kukosa magari

Wakati Serikali ikieleza hayo, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro ameeleza adha aliyopata alipokuwa Mkuu wa Wilaya ya Tunduru na hata sasa alikohamishiwa.

“Nimekaa Tunduru miaka mitano nikiwa mkuu wa wilaya, unaazima magari hadi wale uliopewa kuwasimamia wanakuchoka,” ameandika Mtatiro katika ukurasa wake wa Instagram akiwa safarini Beijing nchini China.

“Hebu fikiria Tunduru ina majimbo mawili ya uchaguzi, tarafa saba, kata 39, vijiji 157, vitongoji 1,179, watu 400,000, kilomita za mraba 18,776, sijui naeleweka? DC unazunguka kwenye hivyo vijiji kila kukicha kwa kuazima magari? Yaani mkuu wa idara ya elimu ana gari halafu DC hana gari.”

Akieleza uzoefu wilayani Shinyanga alikohamishiwa, Mtatiro amesema hajapewa gari na kueleza:

“DC hana gari, anaazima magari kila kukicha, Shinyanga ina majimbo mawili ya uchaguzi, halmashauri mbili, watu takribani 700,000, tarafa sita, kata lukuki, mitaa lukuki, vijiji lukuki, vitongoji lukuki na eneo la utawala ni kilomita za mraba 5,000 hivi.”

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro

Katika ukurasa huo, mmoja wa wachangiaji, Freddie_Jailos, amesema si kwamba wananchi wanapinga ununuzi wa magari ila wanahoji mambo matatu akiyataja kuwa:

“Thamani ya magari yanayonunuliwa haiendani na hali ya uchumi ya wananchi walio wengi. Ni kama mtu wa kijijini kule Tunduru ambaye anaishi kwenye maisha magumu sana lakini ‘anamcheza mwanaye’ ngoma ya Sh500,000 baada ya kuuza mazao yake! Hapa tatizo ni gharama ya gari ndiyo inayohojiwa.”

Ametaja pia mrundikano wa magari yaliyo na hitilafu kwenye halmashauri.

“Kuna gari zina chini ya miaka mitano, chini ya kilomita 400,000 ambazo zinachakaa kwenye viwanja vya halmashauri nyingi kwa sababu ya spares (vipuri) ndogondogo tu,”ameandika Freddie_Jailos.

“Gari lenye thamani ya Sh60 milioni linaoza kwa sababu ya matairi ya Sh2.4 milioni au kipuri cha Sh500,000. Gari linatelekezwa kwa miezi sita, baada ya muda kidogo linauzwa Sh3 milioni. Huu ni ufujaji wa mali za umma na kodi za Wagagagigikoko (wananchi)!”

Ametaja suala la tatu kuwa ni madereva kutojali magari hayo, hivyo kusababisha kuchoka mapema au kusababisha ajali.

Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, mkoani Dodoma, Dk Sophia Kizigo ambaye pia hana gari, amesema amekuwa akifanya kazi kwa kuazima magari ya halmashauri na ya makatibu tawala kitendo kinachowapa wakati mgumu kwenye utendaji kazi wanapotaka kutoka eneo moja kwenda jingine.

Akijibu maswali ya watu waliokuwa wakihoji ununuzi wa magari katika ukurasa wa X, Kizigo ameandika:

“Tunatumia magari ya kuazima halmashauri na kwa RAS (katibu tawala mkoa), leo hili kesho lile, mara umepanga ziara mwenye gari yake naye anataka kuitumia.”

“Mara ya mwisho nimetumikia ofisi yenye gari ya DC nilikuwa Namtumbo, nilipohamia Mkalama hakukuwa na gari, na hata hapa nilipo hakuna, changamoto ni kubwa and yes (na ndiyo), katibu tawala anaweza akawa na gari wakati DC hana.”

Mmoja wa makatibu tawala wa wilaya aliyebadilishiwa nafasi, aliyezungumza na Mwananchi Digital kwa sharti la kutotajwa jina, amesema ma-DC kukosa magari ni jambo la kawaida na huwa wanaazima ya idara.

“Unajua magari ya Serikali hayana kazi moja. Kama siku mkuu anataka gari, basi hiyo idara inabidi iahirishe kazi ya siku hiyo hadi gari likirudi, kwa hiyo kunakuwa na ucheleweshaji tu wa kazi, lakini hazikwami,” amesema.

Hata hivyo, amesema kwa sasa halmashauri zina magari mengi kiasi kwamba hata kama DC hana gari akiwaazima hawaathiriki sana.

“Unakuta mkurugenzi ana gari, ofisa mipango ana gari, idara ya elimu wa gari, mtu wa fedha ana gari, kwa hiyo mkuu akiazima, kazi zinaendelea tu,” amesema.

Mbunge wa zamani wa Tarime Vijijini na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, John Heche amesema hapingi magari kununuliwa bali kinachotakiwa ni kununua ya bei nafuu.

“Kuna sababu gani mkuu wa wilaya au mkoa kununuliwa Land Cruiser VX la Sh500 milioni? Kwa nini asinunuliwe Ford Ranger au Toyota Hilux za Sh100 milioni au chini yake?” amehoji.

Kuhusu wakurugenzi wa halmashauri, amesema hapingi kununuliwa magari kwa kuwa Serikali za mitaa zinapaswa kupewa nguvu ili wazalishe kupitia vyanzo vyao.

Hata hivyo, amesema ili kupunguza mzigo wa Serikali, kuna haja ya kuangalia jinsi ya kuwapata wakuu wa wilaya na mikoa ikiwa ni pamoja na kuzifanya nafasi hizo kuwa za kuchaguliwa.

Amesema vyeo vya wakuu wa wilaya na mikoa ni vya kikoloni akidai kwa sasa vinatumika kisiasa.

“Lazima tuwe na utaratibu wa kuwapata viongozi hawa, si kutegemea mtu mmoja awateue au awaondoe anapotaka,” amesema Heche.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda amesema kwa lengo la kupeleka madaraka kwa wananchi wakuu wa wilaya na mikoa wanaweza kuondolewa.

“Japo ukimwondoa mkuu wa mkoa, lazima atakuja gavana anayechaguliwa na wananchi na atarithi zile gharama, lakini DC akiondoka, anaweza kubaki meya aliyechaguliwa na wananchi,” amesema Dk Mbunda.

“Nakubaliana na wanaosema magari yanunuliwe ya bei nafuu na inatakiwa iwe ni sera ya nchi kununua magari hayo, kwa mfano Toyota Land Cruiser Hardtop. Yawe ni magari ya kazi si ya kifahari kiasi kwamba mtu anataka ahamie humo.”

Serikali imekuwa ikinunua magari ya viongozi kila mwaka. Kwa mfano katika mwaka wa fedha wa 2023/24, Ofisi ya Rais -Tamisemi ilitengewa Sh16.58 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa magari 81 katika Ofisi za Wakuu wa Mikoa.

Kati ya magari hayo, magari matano ni ya wakuu wa mikoa, mawili ni ya makatibu tawala wa mikoa na 74 ni ya wakuu wa wilaya.

Katika mwaka wa fedha wa 2022/23 ziliidhinishwa Sh2.08 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa magari katika Tawala za Mikoa.

Waziri wa Ofisi ya Rais, Tamisemi, Mohammed Mchengerwa

Magari mengine yametelekezwa

Wakati Serikali ikipanga kununua magari mapya, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2022/23 imebainisha kuwapo magari 127 katika halmashauri 13 yakiwa yameachwa bila kufanyiwa huduma za matengenezo au kuuzwa kulingana na taratibu za uuzaji wa mali za umma.

Related Posts