Mafua: Hadi Diamond aliwahi kukodi cheni kwangu

BURUDANI yake kubwa siku zote kwake imekuwa kupanda juu ya ulingo kama msaidizi wa bondia na ikishindikana kwa bondia wa ndani basi usishangae kumuona akiwa kwenye kona ya bondia mpinzani hata akiwa anatokea nje ya mipaka ya Tanzania.

Yaani yale masuala ya uzalendo ambayo serikali kupitia kwa Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Damas Ndumbaro aliwahi kusisitiza yapo hivyo na ni kutokana na kuwa hiyo ndiyo burudani yake.

Kwa kawaida huenda ukachukuliwa kama mtu asiyejielewa na mara zote amekuwa akitambulishwa na mwonekano wake na huyo ndiye Hamisi Mohamed Lukwale kwa majina aliyopewa na wazazi wake, lakini wadau na mashabiki wa mchezo huo wanamtambua zaidi kwa jina la Mafua au Mzee wa Macheni.

Kama ulikuwa hujui basi acha nikwambie kuwa Mafua ambaye mara zote amekuwa akimulikwa na Kamera za Azam Tv huenda ndiyo binadamu wa kwanza nchini kuvaa kilo nyingi za cheni za madini ya fedha (silver) katika shingo yake.

Mafua ambaye anatambulika kama shabiki wa mchezo huo mwenye kutumia mbinu nyingi kufikia ulingo, amefanya mahojiano maalum na Mwanaspoti kuhusu maisha yake katika mchezo huo pamoja na mtindo wake wa kuvaa cheni na pete nyingi kubwa ambazo anasema amekuwa akizikodisha kwa watu na wasanii, akiwamo Diamond Platnumz.

Mafua anasimulia kuwa yeye ni mdau mkubwa wa mchezo huo kwa kuwa aliwahi kucheza kucheza karate pamoja na mchezo wa ngumi akiwa na wakongwe kibao wa zamani katika mchezo huo, akiwemo bingwa wa zamani katika uzani wa juu Willy Isangura ambaye alifariki dunia mapema mwaka huu.

“Ngumi mimi ndiyo mchezo wangu ambao naupenda, sijui mambo ya mpira na hakuna mchezaji hata mmoja ambaye nafahamiana naye, nisiwe muongo na sina muda wa kufuatilia mchezo huo,” anasema.

“Nimeanza kuzipenda ngumi tangu nikiwa kijana mdogo na mazoezi nimefanya sana zamani pale Manzese Maguniani na wakongwe kama Willy Isangura, George Sabuni, Stanley Mabesi, Michael Yombayomba na Rashidi Matumla kwa sababu bondia kama Isangura na Sabuni nimewabebea hadi vifaa mwaka 1984.”

SWALI: Kwa nini umekuwa ukivaa cheni nyingi kwa wakati mmoja?

JIBU: Hiyo kwanza ndiyo sababu ya kuitwa Mzee wa Macheni, lakini suala la kuvaa cheni nyingi kwangu ni starehe kwa sababu napenda kuvaa hivyo ingawa kwa mtu ambaye siyo kawaida hawezi kuvaa hata iweje.

“Lakini ukiondoa hilo, cheni na pete zangu ambazo nimekuwa nikivaa gharama yake ni kubwa sana maana akivaa mtu mwingine bila kuwa na ulinzi wale vishandu (vibaka wanaotumia bodaboda) watapita na wewe.

SWALI: Zinaweza kuwa kilo ngapi?

JIBU: Hapa peke yake nimevaa gramu 4,000 (kilo 4) za cheni peke yake ambazo kila gramu moja thamani yake ni Sh10,000.

“Kiukweli cheni nipo nazo nyingi hadi nafanya biashara ya kuzikodisha. Hapa nyingine nimewakodisha wasanii wa Bongo Fleva ambao wameenda kutumia kwenye shoo zao ambazo zinafika gramu 7,000 (Kilo 7).

SWALI: Unakodisha kwa kiasi gani?

JIBU: “Kawaida kama msanii ni mshikaji wangu huwa natoa hadi kwa Sh50,000 wakati mwingine hadi elfu 70 ila kama hatuna urafiki huwa nachukua hadi Sh200,000 ambazo kiukweli huwa zinanisaidia kuendesha maisha yangu.

“Wasanii wanaokuja kukodi kwangu ni wengi mfano wakati Diamond Platnumz ndiyo aanza kutoka kimuziki, amekuja sana kwangu kuazima kwa ajili ya shoo tena wakati ule akiwa bado anakaa Tandale maana alikuwa jirani kwa kuwa ndiyo ninapoishi huko.

SWALI: Hizo cheni zote unazomiliki thamani yake shilingi ngapi?

JIBU: Huu mzigo una thamani kubwa unaweza kuchukulia kama uchafu lakini hapa zimelala Toyota Harrier mbili na Kirikuu moja kama nyongeza (anasema akicheka).

SWALI: Unaonekana upo karibu zaidi na kambi ya ngumi maarufu ya Nakoz ya kina Mfaume Mfaume.

JIBU: Pale mimi ndiyo rais wao, Nakoz walinichagua kwa kuniambia nitakuwa rais wao kwa sapoti kubwa ambayo nimekuwa nikiwapa kuanzia mabondia hadi mashabiki.

“Unaona hapa katika ofisi yangu ya kukata magari mabovu na kuuza vifaa vya magari hawa wote ni mashabiki wa ngumi ambao nimewaambukiza, hivyo hakuna tukio ambalo wanaweza kukosa na nikiwaambia wote wanatoa sapoti.

SWALI: Unaonekana kila mkoa ngumi zinapofanyika nani huwa anakugharamia?

JIBU: Kila kitu huwa natumia pesa yangu, mimi ni chizi ngumi na hata kuniona kwenye ulingo kama msaidizi ni kwa sababu nasapoti mabondia wote na hakuna kocha ambaye hanifahamu mimi ni nani, wapo hadi wakubwa nawasaidia mambo mengi ya kiuchumi wanapokuwa na mapambano.

SWALI: Hilo pengo limetokana na kitu gani?

JIBU: “Daah, hapa nilikuwa nafanya mazoezi ya kupigana (sparing) na Mfaume Mfaume ndiyo alinipiga ngumi kali ambayo iliondoka na meno yangu mawili, nimeyahifadhi kwangu.

“Unajua zamani ilikuwa bila ya kupigwa siwezi kulala yaani nikutane na Mfaume tupigane ndiyo naweza kujisikia sawa na siyo yeye peke yake mi nishapigana hadi Thomas Mashali (marehemu) ugomvi wa mtaani ila kwa sasa nimekuwa mtu mzima na hizo nguvu sina za kufanya hivyo.

SWALI: Kwa nini wanakuita Mafua

JIBU: Mafua ni jina langu la utani tangu nipo mtoto kwa sababu nilikuwa naumwa sana ugonjwa wa mafua ingawa nilikuwa sipendi sana na ulikuwa ugomvi ukiniita hilo jina ingawa kwa bahati mbaya usichokitaka ndiyo kinachokua zaidi ila sasa ni kawaida.

SWALI: Hizo simu zote zako?

JIBU: Ndiyo, namiliki simu nne kwa ajili ya mambo yangu ya kazi ingawa hapa moja nimeicha kwenye chaji ambazo kwa mwezi natumia Shilingi elfu 20 kwa ajili ya vocha

JIBU: Mke ndiyo ninaye na tuna watoto kumi, sita wangu na wanne wake ingawa kiujumla naishi na familia yenye watu 25 nyumbani kwangu ikiwa pamoja na wazee wangu.

Related Posts