Mwamuzi wa Dabi huyu hapa!

PRESHA ya mchezo wa ‘Kariakoo Derby’ kwa mashabiki wa Yanga na Simba nchini tayari imeanza kupanda wakati zikibakia siku mbili tu kwa miamba hiyo kushuka kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumamosi hii ya Aprili 20 kuisaka heshima baina yao, huku jina la mwamuzi wa pambano hilo likiifikia Mwanaspoti.

Wakati mchezo huo ukisubiriwa kwa hamu taarifa za ndani zilizolifikia Mwanaspoti zimedaiwa pambano hilo la 112 kwa timu hizo tangu kuasisiwa kwa Ligi ya Bara mwaka 1965, limeachwa mikononi mwamuzi Ramadhan Kayoko kutoka Dar es Salaam, ikielezwa ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kutafsiri sheria 17 za soka kwa miamba hiyo itakayokutana na kuanzisa saa 11:00 jioni.

Chanzo makini kutoka Kamati ya Waamuzi ambaye hakutaka jina lake liandikwe, aliliambia Mwanaspoti Kayoko ndiye aliyepigiwa kura nyingi na wajumbe wa kamati ya waamuzi.

“Hadi sasa jina lililopendekezwa kwenye kamati ni la Kayoko kwa sababu wameangalia vitu vingi kutoka kwake, kikao bado kilikuwa kinaendelea cha kutoa maamuzi ya mwisho ila kwa kifupi kinachoendelea ni hicho,” kimesema chanzo hicho.

Chanzo hizo kinadokeza mbali na Kayoko, pia majina ya Jonisia Rukyaa, Emmanuel Mwandemwa ni kati ya marefa waliokuwa wakipigiwa chapuo kabla ya kura nyingi kumwangukia mwamuzi huyo kijana.

Chanzo hicho kilieleza mbali na Kayoko anayepewa nafasi kubwa ila waamuzi wa pembeni watakuwa ni Frank Komba kutoka Dar es Salaam na Janeth Balama wa Iringa huku mwamuzi wa akiba ‘Fourth Official’ akisimamia Hery Sasii kutoka Dar es Salaam.

Rekodi zinaonyesha Kayoko amechezesha michezo minne kati yao na kila mmoja imeshinda mmoja huku miwili ikiisha kwa sare.

Mchezo wa kwanza kwa Kayoko baina ya timu hizo ulikuwa wa nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Yanga ilifungwa mabao 4-1, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, Julai 12, 2020.

Baada ya hapo ukafuata wa fainali ya Ngao ya Jamii iliyowapa Yanga ubingwa wa michuano hiyo kwa ushindi wa bao 1-0, lililofungwa na aliyekuwa nyota wa timu hiyo, Fiston Mayele dakika ya 12, mechi ikipigwa Septemba 25, 2021.

Michezo yote ya Ligi Kuu Bara Kayoko aliyochezesha ni ule wa 0-0, Aprili 30, 2022 na sare ya bao 1-1, Oktoba 23, 2022 na Simba ilitangulia kupitia, Augustine Okrah dakika ya 15 kisha Yanga ikachomoa kupitia Stephane Aziz KI dakika ya 45.

Katika michezo 21 iliyocheza Yanga msimu huu hakuna mechi aliyochezesha Kayoko ila kwa upande wa Simba alichezesha wakati kikosi hicho cha Abdelhak Benchikha kilipolazimishwa sare ya kufungana bao 1-1, dhidi ya Azam FC, Februari 9, mwaka huu.

Kitendawili cha nani mbabe kitateguliwa Jumamosi hii ingawa Yanga inaingia katika mchezo huo ikiwa na morali kubwa hasa baada ya mechi yao ya mwisho iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Novemba 5, 2023 kuifunga Simba kwa mabao 5-1.

Katika mchezo huo wa mwisho mabao ya Yanga yalifungwa na Maxi Nzengeli aliyefunga mawili wakati Kennedy Musonda, Pacome Zouzoua na Stephane Aziz KI wakifunga moja kila mmoja, huku la Simba la kufutia machozi likifungwa na Kibu Denis.
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *