Morogoro. Mwanafunzi Hajirath Shaban aliyeuawa kwa kuchomwa kisu na watu wasiojulikana usiku wa Aprili 16 alipokuwa hosteli, anatarajia kuzikwa leo Aprili 18, 2024 kwenye makaburi ya Kola Manispaa ya Morogoro.
Mwanafunzi huyo aliyekuwa akisoma Chuo cha Mtakatifu Joseph kilichopo Manispaa ya Morogoro, aliuawa baada ya kuvamiwa akiwa hosteli za chuo hicho zilizopo Mkundi, Aprili 16, 2024, kisha akamchoma kisu sehemu mbalimbali za mwili wake.
Akizungumza na Mwananchi Digital, leo Aprili 18, 2024 Yassin Mashuubu, kaka wa rafiki wa marehemu amesema mazishi yatafanyika saa 10 jioni ya leo.
“Mazishi yatafanyika majira ya saa 10 jioni kwenye makaburi ya Kola hapa hapa Morogoro, kabla ya mazishi kutakuwa na kisomo.
“Mama yake mzazi na Hajirath alikuwa akiishi Mwanza lakini kwa sasa wako Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kushughulikia mwili wa marehemu pamoja na baba mzazi; na waliopo hapa ni wanafunzi wenzake aliokuwa akisoma nao,” amesema Mashuubu.
Mwananchi Digital imefika Mtaa wa Kihonda-Kilimanjaro katika msiba huo na kushuhudia mamia ya wanafunzi kutoka St Joseph wakiwa wamehudhuria.
Hajirath aliuawa na mtu ambaye hajafahamika jina lake usiku wa Aprili 16, kwa kuchomwa na kisu sehemu za mwili wake hali iliyosababisha kuvuja damu nyingi na kusababisha kifo chake.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limeeleza kwamba linaendelea na uchunguzi wa kifo hicho kwa kumsaka aliyehusika kutekeleza mauaji hayo.