BEKI wa Lubumbashi Sport ya DR Congo, Mtanzania Abdallah Shaibu ‘Ninja’ kuna jambo amejifunza kutokana na kupata nafasi ya kucheza nje kwa awamu mbili tofauti, linalompa nguvu ya kutoogopa changamoto anazokutana nazo.
Katika mahojiano yake na Mwanaspoti, Ninja anasema kwa mara ya kwanza alipoondoka nchini mwaka 2019 kwenda kujiunga na LA Galaxy II ya Marekani kwa mkopo, ilimjengea ujasiri na uthubutu.
“Baada ya kumalizana na Yanga msimu uliopita, timu nyingi za Ligi Kuu Bara zilihitaji huduma yangu, ila nilichagua kupata changamoto mpya nje, ndipo nikasaini Lubumbashi Sport na kuna timu nje na hii ambayo tulikuwa tunataka kwenda kucheza na Abdi Banda ambaye yupo Afrika Kusini ila mambo hayakwenda sawa,” anasema na kuongeza;
“Maisha bila uthubutu ni ngumu kusonga mbele, kwani kabla ya Yanga nilitoka Taifa Jang’ombe ya Zanzibar, kisha nikaonekana na timu ya MFK Vyškov ambayo ikanipeleka kwa mkopo LA Galaxy ya Marekani, nikitoka hapa naweza kwenda kwingine ama nikarejea nyumbani.
“Wakati natoka Marekani, niliwahi kwenda kufanya majaribio kuna timu moja huko Canada, kilichofanya nisifanikishe dili hilo ni baada ya kuingia kwa ugonjwa wa Covid 19, ilinibidi nirejee nyumbani.”
MAISHA YA DR CONGO
Anasema Congo vyakula ni gharama, tofauti na Tanzania akitolea mfano wa nyama kilo moja ni Shilingi 18000, mchele ule wa kupikia vitumbua ambao kwa Tanzania unaweza ukauzwa Sh1,600, Congo zikipimwa kilo tatu ni Sh10,000 hadi Sh12,000.
“Tanzania tumezoea mchele kupimwa kwa kilo, huku sijui wanapimia kitu gani, ukikadiria hicho kipimo ni kama kilo tatu,” anasema na kuongeza;
“Ili ule ushibe tena kwa kujibana siyo kujiachia mara matunda, mboga za majani kwa siku inaweza ikakugharimu 25,000, kila kitu bei ipo juu, nilipata changamoto wakati wa mfungo wa Ramadhani, nilikuwa nafunga peke yangu, hivyo wakati wa kufungulia kupata futari ilikuwa ishu, ila kwa sasa nashukuru Mungu, maisha mengine yanaendelea.
“Kimaendeleo maisha ya Tanzania tumepiga hatua kubwa, mfano huku muda mwingi naona yanatumika majenereta kutokana na kukatika umeme, ni nadra kukaa muda mrefu bila ya umeme kukatika, jambo jingine nililoliona huku ni askari wenye silaha unawakuta kila kona.
“Kuna mgahawa wa Kitanzania, huko wanaonyesha mechi za Ligi Kuu kupitia Azam, mara nyingi tunaenda kuangalia na wachezaji wenzangu, wanapenda jinsi ambavyo wachezaji wanapewa thamani, wanasaka fursa hizo za kuonekana na timu kwa hali na mali,” anasema.
WANAVYOISHI WACHEZAJI
Tanzania imezoeleka wachezaji wengi maarufu kuwa na wafuasi kwenye mtandao wa Instagram. lakini kwa ya DR Congo, ni tofauti, asilimia kubwa wanatumia Facebook, huko ndiko utakutana na watu maarufu mbalimbali.
“Wachezaji ambao nimecheza nao Yanga ambao walitoka Congo, tulikuwa tunawashangaa tukiona wanatumia Facebook, tukaanza kuwafundisha mambo ya Instagram ili kukutana na mashabiki wao,” anasema na kuongeza;
“Congo ndio wameanza kuamka sasa, kuanza kuona fursa zilizopo Insta, kuna wakati mwingine hata mitandao ya klabu zao, hawapo haraka kuweka taarifa zao huko.
“Nilianza kuwaonyesha kwenye mitandao ya Yanga na Simba inavyofanya kazi yake, walikuwa wanatamani kuona timu zao na zenyewe zinawapromoti wachezaji wao, kiufupi kama mchezaji hajatoka nje hawezi kuona thamani ya ligi yetu ilivyo juu.”
Anasema wakati anajiunga na Lubumbashi Sport kwa mara ya kwanza, wachezaji wengi walikuwa wanamshangaa, kutoka Ligi ya Tanzania inayoonyeshwa live na kwenda DR Congo ambako ni mechi chache ndizo zinazopewa uzito.
“Wenzetu kuonyeshwa kwa ligi, wanakichukulia kama fursa kubwa ya kuonekana na mataifa mengine, ukiachana na hilo maisha wanayoishi mastaa wa Yanga na Simba, wanayatamani hasa wanapoona Wacongo wenzao wanapopata umarufu mkubwa wakija Tanzania,” anasema.
ILIPOFIKIA LIGI YA DR CONGO
Kwa hatua ilipofikia Ligi ya Congo, kucheza mtoano (play offs) ili kusaka bingwa wa nchi, Ninja anasema ndio imeanza kuonyeshwa live, kila kitu kinachofanyika mashabiki wanatamani kujua kila hatua.
“Imefikia pagumu tunacheza kwa mfumo wa nyumbani na ugenini, atapatikana bingwa wa nchi, ambapo bingwa na mshindi wa pili zitacheza Ligi ya Mabingwa, mshindi wa tatu na nne Kombe la Shirikisho Afrika,” anasema na kuongeza;
“Timu zinazocheza mtoano ukanda wa Lubumbashi ni TP Mazembe, FC Lupopo, Lubumbashi Sport na Don Bosco na ukanda wa Kinshasa ni AS Vita, Maniema, AF Congo na Douphine Noir.
“Japokuwa wachezaji wa Congo wana vipaji vikubwa sana, ila uendeshaji wao ni mgumu, kwani viongozi wa klabu wengi ni viongozi wa serikalini, hivyo mpira ni kama unaendeshwa kisiasa.
“Changamoto nyingine, Ligi Kuu ya huku haina mdhamini, tofauti na Tanzania, hilo linafanya maisha ya wachezaji kiuchumi yasiwe juu kivile,” anasema.
Ukimuuliza baada ya kutembea katika nchi mbalimbali, ipi ni bora kwake, atakujibu: “Marekani imebakia kwenye kumbukumbu zangu, nilikutana na mastaa wakubwa duniani kama Zlatan Ibrahimovic ambaye kwa sasa amestaafu na timu yake ya mwisho ilikuwa ni AC Milan.”
Anaongeza: ”Nilipata muda wa kuzungumza na Ibrahimovic kuhusiana na maisha ya soka, jambo kubwa aliloniuliza unatoka nchi gani, nikamjibu Tanzania, aliniambia kama umeweza kufika hadi LA Galaxy una kipaji, amini kwenye kipaji chako bila kujali wengine wanavyokichukulia, jambo ambalo linanifanya hadi leo siogopi kuthubutu.
“Pamoja na ustaa alionao Ibrahimovic, anapomuona mchezaji mwenye hamu ya mafanikio hasiti kumpa moyo, hilo lilinifunza hata nikiwa na jina kiasi gani, haimaanishi nijione ni bora kuliko mtu mwingine.
“Maisha yangu yalikuwa mazuri, ndio maana wakati narudi Tanzania, niling’ara, nilijifunza vitu vingi vya kimaisha, ila hapa Congo, pia najifunza maisha kwa aina yake.”
Anasema wakati anacheza Yanga, mastaa wa Simba ambao alikuwa anawakubali kwa uwezo wao, anawataja ni Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Mzamiru Yassin, Kibu Denis na John Bocco.
“Lakini Bocco kwa sasa sijui kastaafu maana simuoni kucheza. Ila kwa upande wangu hao niliowataja wanajua sana mpira.”
ISHU YAKE NA FEI
Kuna kipindi kulikuwepo na uvumi wa kutemwa Yanga msimu ulioisha ilitokana na kitendo chake cha kuondoa vitu vya aliyekuwa kiungo wa timu hiyo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ bila ruhusa ya viongozi.
Anafafanua hilo: “Mchezaji kuondoka kwenye timu ni jambo la kawaida, siamini kama hiyo ni sababu na wala sikuona ubaya kumsaidia Fei Toto kumpelekea nguo zake, hivyo kutemwa kwa sababu hiyo ilikuwa ni uvumi tu, siyo kweli.
“Wakati Fei Toto anaondoka Yanga, nilikuwa Dodoma Jiji kwa mkopo, niliporejea kwenye chumba nilichokuwa nakaa, alikabidhiwa Tuisila Kisinda, hivyo nikampigia Fei akanielekeza ufungo ulipokuwa.
“Ikabidi nikitumie chumba alichokuwa anakaa, kisha akaomba nimsaidie kuhamisha vitu vyake, kwa kuwa nilikuwa na gari nikahamisha, ila nakumbuka kuna mtu aliniuliza vitu vya Fei vipo wapi nilimjibu nimempelekea mwenyewe, sikutaka stori nyingi nikaishia hapo, sijui sasa hayo mengine yanatoka wapi.”