Unguja. Zanzibar inakabiliwa na ukosefu wa mafuta ya Petroli kwa siku mbili mfululizo na kusababisha adha kwa wananchi wanaohitaji nishati hiyo.
Tatizo hilo limeanza Aprili 14, 2024 hadi leo Aprili 16, 2024 vituo vingi vya kuuzia mafuta vimeshuhudiwa vikiwa na idadi ndogo ya wafanyakazi kinyume na ilivyozoeleka.
Kutokana na kadhia hiyo, kumesababisha kupanga kwa gharama za usafiri wa bodaboda. Mwananchi Digital imeshuhudia ongezelo la Sh1,000 zaidi kwa njia za mjini kwa mfano kutoka Michenzani hadi Malindi Mjini kwa abiria analazimika kulipa Sh3,000 baada ya Sh2,000 iliyozoeleka.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) imekiri kuwepo kwa tatizo hilo na kusema vituo vyote vya Zanzibar vimekumbwa na changamoto hiyo, huku wakiwaomba radhi wananchi.
Kupitia taarifa yao kwa vyombo vya habari wamesema changamoto hiyo imesababishwa na kuchelewa kwa meli ya mafuta ambayo ilikwenda kupakia mafuta hayo katika Bandari ya Tanga, Tanzania na kuipeleka visiwani humo.
Wamesema tayari meli hiyo imeingia na wameanza mchakato kushusha kupeleka ghalani na badaye mafuta hayo yatasambazwa vituo vyote.
Ali Ismail, mtoa huduma za kubeba watalii visiwani humo amesema tangu jana Jumatatu ameshindwa kufanya kazi kutokana na kukosa mafuta kwenye gari yake.
Amesema katika kipindi hicho cha siku mbili alikuwa na kazi nne za kuchukua na kupeleka wageni hotelini, lakini ameshindwa kufanya kazi, huku wageni aliokuwa ameshafanya mawasiliano nao wakibaki wanamshangaa.
“Vitu kama hivi watu wasione ni vidogo vinatuharibia. Nchi kukosa mafuta maana yake unapunguza harakati za utafutaji wa fedha na kuongeza mapato kupitia kodi ni lazima wajipange kuondoa shida hii,’ amesema Ismail.
Amesema siku mbili ambazo hajafanya kazi amesababisha usumbufu mkubwa kwa wageni pamoja na hoteli ambazo anafanya nazo kazi.
Mmoja wa wamiliki wa vituo vya kuuza mafuta katika barabara kuu inayokwenda Fumba, amesema leo ni siku ya tatu huduma ya mafuta ya petroli inasuasua na kupatikana kwake hakuna uhakika.
Mmiliki huyo aliyeomba hifadhi ya jina lake amesema hali hiyo inampa ugumu hadi yeye, kwani wateja wengi wamekuwa wanakwenda na kurudi bila kupata huduma na kusababisha usumbufu kwa wateja wake.
Aidha amesema pamoja na usumbufu huo, unamuwia vigumu, kwani ana wafanyakazi ambao amewaajiri na kuwalipa kwa mwezi, hivyo inapotokea mazingira ya aina hiyo wafanyakazi hao hawafanyika kazi, lakini wanasubri mshahara wao mwisho wa mwezi kama kawaida.
“Si unaona hapa kuna idadi ndogo tu ya wafanyakazi, wengi wapo majumbani mwao hawana lakufanya wakija hapa, lakini mwisho wa mwezi wote wanahitaji kulipwa leo ni siku ya tatu wengine hawapo hapa na siwezi kulikwepa hili, kwani siwezi kukataa kuwalipa ama kuwakata kwa sababu hawakukataa kuja kazini,’ ’amesema.
Kwa upande wake, Ali Abdala amesema amechelewa kazini baada ya gari yake kuzima njiani ikikosa mafuta, kwani alipanga kuweka mafuta katika kituo cha Mtoni alipokuwa akitoka nyumbani kwake Kijichi.
Amesema kuna haja mamlaka kujipanga kuzuia hali kama hiyo isitokee ukizingatia watu wengi wapo na harakati za kwenda na kurudi kazini.
“Gari yangu nimeiacha pembeni ya ile sheli pale ukipita utaiona, nimeamua kupanda pikipiki ili niwahi kazini maana hawa mabosi nao hawaeleweki ukichelewa inakuwa ugomvi,” amesema.