Unguja. Licha ya huduma ya mafuta ya petrol kuanza kupatikana usiku wa kuamkia leo Jumatano, Aprili 17, 2024 kisiwani Unguja, bado hofu imeendelea kuibuka kutokana na kiasi kidogo kinachodaiwa kupatikana.
Kwa takribani siku tatu kuanzia Aprili 14 hadi Aprili 16 Unguja ilikabiliwa na upungufu wa petroli katika vituo vingi vya mafuta, kusababisha adha kwa wananchi na kukosekana huduma muhimu za usafiri.
Mamlaka ya Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (Zura) ilisema upungufu huo ulisababishwa na kuchelewa meli iliyofuata nishati hiyo katika bandari ya Tanga, hata hivyo, Aprili 15 meli hiyo ilitia nanga bandari ya Mtoni Unguja.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, baadhi ya wamiliki wa vituo vya mafuta wamesema utaribu uliotumika kugawa mafuta baada ya kuwasili, haujawahi kutumika kwa siku nyingi, ambapo kila mmiliki wa vituo vya kuuza mafuta amepewa lita 2,000, hata kama anahitaji lita 10,000 za mafuta kwa siku.
Mmoja wa wamiliki hao kisiwani hapa, ambaye hakutaka kutajwa jina, amesema lita 2,000 walizopewa haziwezi kumfikisha hata siku mbili kwa kuwa tayari kuna uhitaji mkubwa.
Amesema pamoja na kuwa wametakiwa kuchukua tena mafuta hayo pindi yatakapomalizika, jambo hilo sio zuri kibiashara na linawafanya watoe matumizi ya ziada ambayo yangeweza kuepukika.
‘’Sisi tunalipa hadi gari la kuleta mafuta hapa, sasa kwenda na kurudi kila siku kuchukua mafuta ni gharama za ziada ambazo zingeweza kuepukwa kama tungechukua mafuta mengi zaidi,’’ amesema mmiliki huyo.
Amesema kuna haja kubadili mifumo ambayo itaondoa changamoto kama hizo ili zisiweze kujirejea na kusababisha usumbufu.
Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Wenye viwanda na Wakulima Zanzibar (ZNCC), Hamad Omar Hamad amesema kukoseka kwa huduma ya mafuta kwenye nchi hata kwa dakika tatu, kuna changamoto kubwa ambazo zinajitokeza.
Amesema huduma ya mafuta ni muhimu kwa matumizi ya maisha ya watu kila siku, hivyo kuna ulazima wa kuwepo kwa mikakati madhubuti ambayo itaondoa changamoto hizo ambazo alisema zimekua zikijirejea kila baada ya muda.
Wakati hayo yakijiri, Chama cha ACT Wazalendo kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na Katibu wa Habari na Uenezi, Salim Abdalla Bimani kimeitaka Serikali kupitia mamlaka husika kutoka hadharani na kuwaeleza wananchi ukweli kuhusu changamoto hiyo.
Sambamba na hilo ameitaka pia Serikali kufanya mapitio ya mfumo uliopo wa uingizaji mafuta visiwani hapa ambao umekuwa sababu ya kuwepo kwa changamoto kila baada ya muda.
Ameitaka Serikali kujitathmini upya na kupunguza gharama za matumizi ya magari mengi yasiyokuwa na ulazima wakati wa ziara za viongozi ambazo hufanywa kila siku.
‘’Kuna idadi kubwa ya magari ya viongozi yamekuwa yakitumika bila uhitaji kufanya vile, ni kuongeza gharama na matumizi ya mafuta mabayo yangeingia kwenye mzunguko wa wananchi,” alisema.
Akizungumiza chanagmoto hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano Zura, Mbaraka Hassan Juma amekiri wamiliki wa mafuta kupewa lita 2,000 kila wanapohitaji, kinyume na ilivyozoeleka.
Amesema hali hiyo ni kutokana na kuongezeka kwa uhitaji wa huduma hiyo kwa vituo vyote, hivyo kuna ulazima wa kufanya hivyo na hakuna njia nyingine.
Amesema wamiliki wa vituo vya mafuta wanaruhusiwa kuchukua tena mafuta mara yatakapomalizika na hakutakuwa na changamoto yoyote ile, hivyo wanapaswa kuondoa wasiwasi.
‘’Ni lazima mafuta yatoke hivi kwa sababu uhitaji upo sehemu zote, hivyo yangetolewa kwa njia nyingine kuna maeneo yangekosa na kusingekuwepo kabisa huduma hii,” amesema.
Kuhusu idadi ya mafuta yaliyoingizwa Zanzibar amesema ni lita milioni 2 wakati mahitaji ni lita 200,000 kwa siku.
Alisema mafuta yaliongizwa yanaweza kutumika mpaka siku 10 lakini kabla ya kumalizika mengine yataingizwa kwa sababu meli ipo Tanga na hakuna foleni yoyote.
Kuhusu mkakati wa kuhifadhi mafuta mengi zaidi, amasema jambo hilo lipo na tayari Serikali imetenga eneo maalumu Mangapwani.
Hado sasa amesema tayari mapipa 21 yameshajengwa na wawekezaji wengine zaidi wamejitokeza kutumia fursa hiyo.