Rais Mwinyi: Serikali zinaendelea kushughulikia changamoto za Muungano

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema Serikali zote za Tanzania na Zanzibar mbili zinaendelea kuchukua hatua mbalimbali kushughulikia na kupata ufumbuzi wa changamoto za Muungano zinazojitokeza.

Amesema utatuzi wa changamoto hizo umezidi kujenga imani kubwa kwa wananchi kuhusu uimara wa Muungano huo.

Kwa nyakati mbalimbali juhudi zimekuwa zikichukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kushughulikia hoja za Muungano.

Miongoni mwa hatua hizo ni kuundwa tume na kamati ya pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kushughulikia masuala ya Muungano iliyoundwa mwaka 2006.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Jumapili, Aprili 14, 2014 wakati akizindua maadhimisho ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar katika viwanja ya Dimani Nyamanzi Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar.

Dk Mwinyi amesema kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka huu wa 2024, hoja 25 zilipokewa na kujadiliwa ambapo kati ya hoja hizo, hoja 22 zimepatiwa ufumbuzi na kuondolewa kwenye orodha ya hoja za Muungano.

“Hoja zilizobaki zipo katika hatua mbalimbali za kupatiwa ufumbuzi na ni imani yangu kuwa, kwa utashi na dhamira ya dhati ya Serikali za pande zote mbili, hoja zilizobaki zitapatiwa ufumbuzi,” amesema Dk Mwinyi.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo inasema, “Tumeshikamana na Tumaimarika kwa maendeleo ya Taifa ya Taifa letu.”

Dk Mwinyi amesema utatuzi wa changamoto za Muungano, umeongeza imani ya Watanzania kwa Serikali zao na hivyo kuimarisha, kudumisha amani ya muda mrefu na utulivu wa Tanzania ambao ni tunu muhimu na fahari ya nchi.

Ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi wote kwamba Serikali zote zitaendelea kuchukua hatua ili nchi iendelee kupata maendeleo na ibaki kuwa nchi ya amani na utulivu.

Amesema katika kipindi hiki cha miaka 60, Tanzania imeendelea kubaki katika historia na mfano bora wa kudumisha Muungano barani Afrika na duniani kote na Muungano huo kuipa heshima kubwa katika Jumuiya ya Kimataifa.

“Hali hii imetokana na misingi thabiti ya umoja, amani na mshikamano iliyoasisiwa na viongozi wetu waasisi hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na marehemu Mzee Abeid Amani Karume pamoja na viongozi wenzao waasisi wa Muungano,” amesema Dk Mwinyi.

Pia, dhamira hiyo imechochewa na viongozi wakuu walioshika nyadhifa za uongozi kwa awamu mbalimbali za Serikali ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuendeleza maono hayo.

“Tunafurahia kuona umoja wa Watanzania unazidi kuimarika, ushirikiano baina yetu katika shughuli mbalimbali unaongezeka na amani ya nchi yetu inaendelea kudumu.”

Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk Selemani Jafo amesema Muungano una historia ndefu hivyo ipo haja kuhakikisha unazidi kulindwa kwani umeleta tija kubwa kwa wananchi.

Amesema mchakato wa Muungano ulianza Aprili 22, 1964 baada ya waasisi wa Muungano huo hayati Nyerere na Karume walipoanza vikao vya kuunganisha mataifa hayo mawili kisha

Aprili 25 vyombo vya kutunga sheria vililidhia makubaliano na hoja hiyo ikatungiwa sheria namba 22 ya mwaka 1964 ikijulikana Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kabla ya Oktoba mwaka huohuo kupitisha sheria namba 61 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

“Aprili 28, Baraza la Mawaziri la kwanza liliapishwa likiwa na mawaziri 23, Oktoba 28 bunge lilipitisha sheria namba 61 ya kubadilisha kuwa muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Zanzibar,” amesema Dk Jafo.

Amesema muungano umesaidia kukuza lugha, mawasiliano na vyama vya ukombozi vya Tanu na ASP.

Dk Jafo amesema katika Muungano huo ziliibuka hoja 25 ambazo Serikali zote mbili zikishirikiana kuzitatua na mpaka sasa zimetatuliwa hoja 22, hoja 15 kati ya hizo zimetatuliwa katika kipindi cha utawala wa Serikali ya awamu ya sita na nane.

Mwaka 2010 zilitatuliwa hoja mbili, mwaka 2020 zikatatuliwa hoja tano na kufika jumla ya hoja saba.

Dk Jafo amesema ili kuendelea kutoa elimu ya Muungano kimetengenezwa kitabu kinachoeleza masuala mbalimbali ambapo kitabu hicho pamoja na maeneo mengine kitatumika kufundishia shuleni hususani sekondari.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema haikuwa kazi rahisi kufikia hapo lakini ni kutokana na Serikali zote kujidhatiti kuhakikisha Muungano huo unaendelea kuwapo kwa manufaa ya mataifa yote mawili.

Hemed amesema wapo watu ambao hawajui jinsi Muungano huo unavyonufaisha watu, hivyo wataendelea kutoa elimu kuhakikisha kila mmoja anatambua umuhimu na tija yake.

“Wapo watu hawajui jinsi Muungano unavyotuunganisha, lakini wengine wanajizima data, na kutaka kupotosha ukweli, hatutakubali jambo hilo litokee tutahakikisha tunaendelea kutoa elimu ili kila mmoja atambue umuhimu wake,” amesema Hemed

 “Hawa wazee walifanya jambo kubwa lazima wnanchi tuzidi kuendela kuulinda kwa wivu mkubwa muungano wetu.”

Nao baadhi ya wananchi waliohudhuduria katika hafla hiyo, walipongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali kuhakikisha Muungano unalindwa na kunufaisha wengi.

“Binafsi naona matunda mengi, kwanza kuna muingiliano wa wananchi kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine bila kubughudhiwa, kuna watu wanakwenda Tanzania bara kufanya biashara na wengine wanakuja huku,” amesema Maryam Abeid Haji mkazi wa Mtoni.

Kilele cha sherehe hizo itakuwa Aprili 26, 2024 katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam huku mgeni rasmi atakuwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika uzinduzi wa maadhimisho hayo, umeambatana na burudani za wasanii wa wa ngoma za asili, taarabu na bongo fleva akiwemo Harmonize na Riko Single na bendi ya TOT.

Related Posts