Raska Zone hesabu kali wakiitisha KVZ

WAKATI Raska Zone ikianza mazoezi kujiandaa na Ligi Daraja la Kwanza Kanda ya Unguja, mastaa wametamba kurejea uwanjani kwa nguvu mpya kutafuta kupanda Ligi Kuu msimu ujao.

Timu hiyo imekuwa na matokeo mazuri ikianza kufuzu 16 bora ya Kombe la Shirikisho, ipo nafasi ya pili kwa pointi 27 kwenye Ligi Daraja la Kwanza ikiachwa alama mbili na vinara Paje Stars wenye 29.

Raska Zone watakuwa kibaruani leo Alhamisi kuwakabili KVZ katika mchezo wa Kombe la Shirikisho hatua ya 16, mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mao Zedong A.

Nahodha wa kikosi hicho, Ramadhan Yussuf Isaa alisema licha ya kuwepo kwenye mapumziko ya mwezi mmoja lakini wamerudi wakiwa na nguvu na ari mpya na wapo tayari kuipambania timu hiyo.

Alisema malengo yao ni kuipandisha timu hiyo Ligi Kuu, kitu ambacho kipo ndani ya uwezo wao kutokana na mwenendo wa matokeo katika mechi zao na kwamba KVZ wasitarajie mteremko.

“Tunajua mchezo dhidi ya KVZ utakuwa mgumu sana lakini chochote kinaweza kutokea kwa sababu wote tunahitaji ushindi ili kufuzu robo fainali,” alisema na kuongeza:

“Sisi tunawaheshimu KVZ ni timu iliyotuzidi daraja, ila hili ni soka tumeshuhudia Simba SC wakiondoshwa na Mashujaa, wengi wao walikuwa hawaamini kama itatokea hivyo,” alisema.

Related Posts