Sababu Rais Samia kupewa shahada nne za heshima

Dar es Salaam. Uimara katika usimamizi wa sekta fulani na kuwa na mchango katika Taifa lake ni miongoni mwa sababu zilizotajwa na wasomi kuwa chachu ya Rais Samia Suluhu Hassan kutunukiwa shahada ya nne ya heshima ya udaktari.

Kwa mujibu wa wasomi hao, mara nyingi shahada hizo hutolewa kwa mtu aliyeonyesha mchango mkubwa katika Taifa lake na hata kuivusha nchi katika mambo magumu.

Pamoja na hayo, wanazuoni hao wameeleza wakati mwingine hutolewa kama mbinu ya Taifa husika kufanikisha mambo yake.

Mitazamo hiyo ya wasomi inakuja wakati ambao, Rais Samia ametunukiwa shahada nne za heshima za udaktari tangu alipoingia madarakani Machi 19 mwaka 2021.

Shahada ya kwanza ya heshima ya udaktari, alitunukiwa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Novemba 30, mwaka 2022.

Hiyo ilifuatiwa na shahada ya heshima ya udaktari wa falsafa kutoka Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru nchini India, Oktoba 10, 2023.

Tunu ya shahada hizo haikuishia hapo, mkuu huyo wa nchi alitunukiwa shahada nyinyine ya heshima ya udaktari ya Usimamizi wa Utalii na Masoko ya Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA), Desemba 28, 2023.

Kama hiyo haitoshi leo Alhamisi, Aprili 18, 2024, Rais Samia ametunukiwa shahada nyingine ya heshima na Chuo Kikuu cha Ankara nchini Uturuki.

Akizungumzia shahada hizo, mchambuzi wa masuala ya siasa, Buberwa Kaiza amesema kwa kawaida shahada hizo hazina ukomo wa nani apewe na nani asipewe, bali utashi wa chuo ndiyo unaoamua.

Lakini, duniani amesema wanaopewa ni wale waliofanya mambo makubwa kwenye nchi zao, mathalan viongozi waliozipitisha nchi zao kwenye mambo magumu.

“Shahada hizi zinaweza kutolewa kutoka kwa watu wenye masilahi na Tanzania, inakuwa kama njia ya kusukuma mambo yao,” amesema.

Hata hivyo, Kaiza amesema haoni kama shahada hiyo inaongeza lolote kwa Watanzania.

Mbali na Buberwa mwingine aliyezungumzia shahada hizo ni mchambuzi wa Sayansi ya Siasa, Dk Paul Loisulie akisema shahada ya heshima hupewa mtu pale anapotoa mchango mkubwa kwa nchi yake katika sekta fulani.

“Ni heshima ambayo chuo chenyenye huamua kumpa muhusika, na ni utaratibu uliopo duniani kote. Ni kama wameamua kumpa maua yake kwa kile anachokifanya kwenye eneo fulani,” amesema.

Hata hivyo, mwanazuoni huyo amesema kwa maana nyingine shahada kama hizo hutumika kama mbinu za nchi fulani kushawishi kufanikishwa kwa mambo yao.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Justine Kajerero amesema shahada hizo hubadili hadhi ya mtunukiwa kama ambavyo Rais Samia anatambulika kama Daktari kwa sasa.

“Kwa Taifa tumeona utendaji wake, na ni vizuri kwamba anatambuliwa ulimwenguni,” alisema.

Kajerero amesema mara nyingi kutolewa kwa shahada hizo kunahusisha majopo na kamati za vyuo husika yanayokaa kujadili kwa kina kama muhusika anastahili kabla ya kumtunuku.

“Hii inaweza kumfanya afanye mambo makubwa zaidi kwenye hiyo sekta ambayo imetambuliwa na kumfanya apate heshima hiyo,” amesema Kajerero.

Akizungumza baada ya kutunukiwa shahada hiyo, Rais Samia amesema ni heshima kwake na Taifa lake kutambuliwa na chuo hicho hadi kutunukiwa shahada hiyo.

“Hii ni heshima kwangu na furaha kwa nchi yangu. Ninachofurahi zaidi ni kuona mambo ninayoyafanya nchini kwangu yanaonekana na ulimwengu mzima,” amesema.

Katika hotuba hiyo, Rais Samia alisisitiza Tanzania na Uturuki kuimarisha uhusiano kwa masilahi ya kiuchumi kupitia uwekezaji.

Hata hivyo, ameeleza kuwepo kwa mwenendo mzuri wa uhusiano wa mataifa hayo, kwa kuwa hata urari wa biashara umeongezeka kutoka Dola 60 milioni  za Marekani mwaka 2012 hadi Dola 300 milioni mwaka 2022/23.

Ametumia juukwaa hilo, kueleza juu ya kuimarika kwa uchumi wa Tanzania na juhudi za Serikali katika kuweka mazingira bora na rafiki kwa wawekezaji.

Amesema leo wanatarajia kufanya mkutano wa kibiashara na jumuiya za wafanyabiashara jijini Istanbul nchini humo.

Hata hivyo, ameeleza aliingia madarakani katika kipindi ambacho dunia ilikuwa inakabiliwa na janga la Uviko-19 na vita vya Russia na Ukraine, lakini hatua mbalimbali zilichukuliwa kuhakikisha ustawi unaendelea.

“Nina furaha kueleza mwaka 2023 mfumuko wa bei ulibaki kawaida kwa maana asilimia 3.9 na pato la taifa lilifikia asilimia 5.2,” amesema.

Related Posts