Serikali ya Tanzania kufuta leseni za utafiti wa madini zisizofanyiwa kazi

Dodoma. Serikali ya Tanzania inakusudia kufanya mapitio ya leseni za utafiti wa madini ili kuzifuta zitakazobainika hazifanyi kazi au hazijalipiwa, lengo likiwa ni kutwaa maeneo na kugawa kwa wachimbaji wadogo.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi, Aprili 18, 2024 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akijibu swali la papo kwa hapo la Mbunge wa Kishapu (CCM), Boniphace Butondo aliyehoji sababu za ongezeko kubwa la leseni za utafiti na hasa katika maeneo ya madini nchini na zimekuwa zikitolewa kwa wageni.

Amesema leseni hizo kwa sehemu kubwa zimekuwa zikihodhi maeneo makubwa ambayo wachimbaji wadogo wamekuwa wakifanya shughuli za kuendeleza maisha yao ikiwamo uchimbaji wa madini.

“Nini mpango wa Serikali wa kudhibiti maeneo makubwa yanayowanyima fursa wachimbaji wadogo wanaojishughulisha na shughuli za uchimbaji madini hapa nchini?” amehoji mbunge huyo.

Akijibu swali hilo, Majaliwa amesema kuna maeneo makubwa ambayo yamechukuliwa na watu wanaofanya utafiti lakini hakuna matokeo huku wengine wakiwa hawajalipia gharama za kumiliki na kutenda kazi hiyo.

Amesema wakati akichangia bajeti ya ofisi yake, Waziri wa Madini, Antony Mavunde alitoa maagizo kwa mikoa yote kufanya mapitio ya leseni za utafiti na maeneo makubwa yaliyogawiwa ambayo hadi leo hakuna kazi yoyote inayoendelea.

Amesema nia ya Serikali ni kuyatwaa maeneo yote yaliyokaliwa kwa muda mrefu  kisha kuyagawa kwa wachimbaji wadogo ili kupanua wigo kwa vijana kupata fursa ya uchimbaji wa madini.

Mavunde  amesema mpango wa Serikali ni kufanya mapitio ya maeneo hayo baada ya agizo la wizara kwa mikoa kutekelezwa.

“Na niwaagize sasa makamishina, mameneja wa mikoa wa madini wakamilishe kazi hiyo haraka sana ili tutambue maeneo makubwa yanayoshikiliwa lakini hayafanyi kazi na ambayo tumetoa leseni hayajalipiwa. Tutafuta leseni na kufanya mgawo upya kwa wachimbaji wadogo,”amesema.

Related Posts