Sh750 milioni zatengwa kuwapa mitaji wakulima wadogo wa shayiri

Dar es Salaam. CRDB Bank Foundation (CBF) imetenga kitita cha Sh750 milioni ili kuwapa mitaji wezeshi wakulima wadogo wa shayiri kwenye mikoa ya Kaskazini.

CBF imebainisha hayo hivi karibuni wakati wa kusaini mkataba wa makubaliano (MoU) na kampuni ya Tanzania Breweries Limited (TBL) kwa ajili ya ushirikiano unaolenga kuwawezesha wakulima wadogowadogo wa zao hilo.

Mkurugenzi Mtendaji wa CBF, Tully Mwambapa amesema fedha hizo zinatolewa kama mitaji wezeshi kwa kundi la kwanza na shughuli itakuwa endelevu baada ya kuona matokeo kwa wakulima wa kundi la kwanza.

“Tayari tumekwishatoa mitaji wezeshi ya Sh232 milioni kwa wakulima wa West Kilimanjaro,” amesema.

Pia, amesema maombi ya Sh132.1 milioni yapo kwenye hatua za mwisho za kuidhinishwa ili kuwafikia wakulima hao.

“Pesa hizo ni kwa ajili ya kuwapa mitaji wezeshi ya pembejeo za kilimo ikiwamo mbolea, dawa sanjari na zana za kilimo,” amesema.

Amesema, CBF pamoja na mambo mengine, imejikita kusaidia kuongeza ujumuishi wa kiuchumi, kuboresha maisha na kukuza ustawi wa jamii.

“Tumekuwa tukibuni na kutekeleza programu mbalimbali za uwezeshaji kama vile programu ya IMBEJU ambayo hadi sasa imeweza kuwafikia wanawake na vijana zaidi ya 300,000 na kutoa mitaji wezeshi ya Sh5 bilioni.

Katika mwendelezo wa jitihada hizi, taasisi yetu ilifanya mazungumzo na wenzetu TBL kuona ni kwa namna gani tutashirikiana kuwawezesha wakulima wadogo wa zao la shayiri, hususani vijana,” amesema Tully.

Amesema, mazungumzo hayo yamefungua kurasa mpya kwa vijana wengi wanaojishughulisha na kilimo cha shayiri katika mikoa ya Kilimanjaro, Manyara na Arusha hasa maeneo ya Hai, Babati, Karatu na Monduli.

“Ili kuhakikisha ushirikiano huu unakuwa na manufaa makubwa kwa wakulima pamoja na jamii nzima kwa pamoja tumejiwekea malengo manne ambayo ni kuimarisha ajira kwa vijana na kusaidia kukuza maendeleo ya jamii,” amesema.

Malengo mengine aliyoyataja ni kuwa na kilimo endelevu cha zao hilo, kuwapa   elimu ya fedha na kuongeza uzalishaji na mapato kwa wakulima wadogo

“Ubia huu pia unalenga katika kuhamasisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo kwa wakati, matumizi bora ya teknolojia na mafunzo.

“Hii itasaidia kupata mavuno mengi na mapato bora kwa wakulima, familia zao na jamii zinazowazunguka, achilia mbali kuwepo na uhakika wa  soko kutoka kwa mbia wetu TBL,” amesema Tully.

Akizungumzia ushirikiano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Michelle Kilpin, amesema lengo ni  kuwajengea uwezo wakulima wadogo wa shayiri ili ifikapo mwaka 2025 wawe na ujuzi wa hali ya juu wa kilimo cha zao hilo.

Amesema watatoa fursa mbalimbali kwa wakulima wadogo wadogo, ikiwa ni pamoja na kuwahakikishia uhakika wa soko na kuimarisha ustawi wao wa kiuchumi.

Related Posts