Takukuru Geita yabaini kasoro kwenye miradi 1,800

Geita. Miradi 1,800 yenye thamani ya Sh7 bilioni iliyofuatiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Geita mwaka 2022/23 imebainika kuwa na kasoro zikiwamo za usanifu, ununuzi na baadhi ya fedha za miradi kuhamishiwa kwenye matumizi yasiyohusiana na mradi husika.

Hayo yamebainishwa leo Aprili 18, 2024 kwenye kongamano maalumu linaloendelea mjini Geita lililoandaliwa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) kwa kushirikiana na Takukuru Geita na kuwahusisha wadau wa taasisi za umma, wazabuni wanaopata zabuni mgodini humo na viongozi wa Serikali kuanzia ngazi ya vijiji.

Ofisa Takukuru Geita, Maganga Dominick amesema baadhi ya miradi iliyobainika kuwa na kasoro ni ile ya sekta ya afya, ujenzi, elimu, maji, umeme na kilimo na utawala.

“Katika mwaka 2022/23, Takukuru ilifuatilia matumizi ya rasilimali za umma kwenye utekelezaji wa miradi 1,800 yenye thamani ya Sh7.7  bilioni. Ufuatiliaji huu ulifanyika katika sekta za afya, huduma za jamii, fedha, ujenzi, elimu, maji, umeme, kilimo, majengo na usafirishaji na kubaini kasoro mbalimbali.

“Kasoro katika usanifu mfano baadhi ya miradi kutokuwepo kwa wataalamu wa ujenzi kama vile wasanifu, wahandisi wa ujenzi pia kasoro katika ununuzi, mfano kwa baadhi ya miradi malipo ya vifaa yalifanyika pasipo kufuata taratibu kama vile nyaraka zinazoonyesha kupokewa kwa vifaa husika,” amesema Dominick.

Ofisa huyo wa Takukuru ametolea mfano malipo katika baadhi ya miradi fedha za mradi zilihamishwa kwa matumizi yasiyohusiana na mradi husika.

Amesema kutokana na hali hiyo, Takukuru imeendelea kutoa elimu ya masuala ya rushwa kwa wazabuni ili wasijihusishe na vitendo vya rushwa na kuhakikisha miradi inayotekelezwa inakuwa na tija kwa jamii.

Dominick amesema pamoja na nia nzuri ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR), upo uwezekano wa kutumika vibaya kwa pande zote mbili.

“Tujiulize, je, kuna uwazi kwenye utekelezaji wa mradi husika? Kuna ushirikishwaji wa jamii? Je, miradi inayoibuliwa inagusa mahitaji halisi ya jamii? Kiasi kilichotajwa kutumika kwenye mradi kinaakisi thamani halisi ya mradi? Kama mtajiuliza yote haya lazima mradi ukikamilika utakuwa na tija kwa wananchi na hakutakuwa na malalamiko,” amesema Maganga.

Kwa mujibu wa Utafiti wa Hali ya Utawala na Rushwa nchini ya mwaka 2020, uelewa mdogo, kutaka kuharakisha upatikanaji wa huduma, upindishaji wa sheria kwa lengo la kupata upendeleo, adhabu ndogo inayotolewa kwa wanaothibitika kuhusika na vitendo vya rushwa ni miongoni mwa sababu zinazochangia rushwa kuendelea.

Akitoa elimu kwa wadau waliohudhuria kongamano hilo, mwakilishi wa GGML, Salum Haji amesema kampuni hiyo imeweka utaratibu na kanuni kwa kuzingatia mapambano dhidi ya rushwa ili kuepuka faini zinazotozwa endapo kampuni itabainika kujihusisha na rushwa.

Amesema maeneo hatarishi yanayoweza kuwa na mianya ya rushwa ni ya ajira, ununuzi na utoaji zabuni.

Mmoja wa washiriki wa kongamano hilo, Zubeda Omary amesema uwazi uliopo ndani ya mgodi huo utasaidia watu kupata zabuni bila upendeleo.

Related Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *